Mkazi wa Mtaa wa Mateka, Manispaa ya Songea, Denis Komba
(26) amefariki baada ya nyoka wake aliyekuwa amembeba kwenye mfuko wa
jaketi kuuawa na wananchi.
Komba alifariki dunia katika hospitali ya Rufaa Songea
mkoa wa Ruvuma (Homso) ambako alilazwa baada ya watu wenye hasira kumuua
kwa mawe na fimbo nyoka wake huyo.
Mashuhuda wanaeleza kuwa kabla ya wananchi kumuua nyoka
huyo, Komba aliwasihi wasifanye hivyo kwa kuwa wakimuua na yeye
angekufa, lakini ombi lake hilo halikusikilizwa.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, siku ya tukio Komba
alikodi pikipiki ya Kassian Haule (24) ambaye ni mkazi wa Mpitimbi,
yenye namba za usajili MC 724 AKB ili apelekwe nyumbani kwake mtaa wa
Mateka.
Akisimulia tukio hilo, alisema alipofika katika eneo la
Benki ya Posta ya zamani barabara kuu ya Sokoine, dereva wa pikipiki
alihisi kuna kitu kinamtekenya na kumgonga gonga kwa nyuma, ndipo
alipogeuka nyuma na kumwona abiria wake amebeba nyoka mkubwa huku
amesimamisha kichwa.
Haule alisema, baada ya kumuona nyoka huyo aliruka kutoka
kwenye pikipiki na kuanguka pembeni mwa barabara na abiria wake
alimwachia yule nyoka ambaye alikimbilia kwenye kalavati la maji.
Aliongeza kuwa ndipo alipopiga kelele za kuomba msaada na
kundi la vijana waendesha pikipiki wenzake walifika eneo hilo la tukio
kwa lengo la kumsaidia mwenzao juu ya maswahiba yaliyompata hadi
kumfanya apige kelele.
Alisema kabla ya vijana hao hawajafanya jambo lolote,
Komba aliwaomba vijana hao na watu wengine waliofika katika eneo hilo
wasimpige nyoka wake kwani iwapo watampiga na kufa yeye pia atapoteza
maisha. Kutokana na maneno hayo, Haule alimtoa nyoka huyo ndani ya
kalavati na kwa kushirikiana na vijana wenzake walianza kumpiga nyoka
huyo hadi kufa.
Alisema wakati wanampiga nyoka huyo, Komba ambaye ndiye
mmiliki wa nyoka huyo naye alianza kulegea kisha akaanguka chini huku
akitokwa na mapovu mdomoni na puani.
Habari zinasema kuwa,baada ya Komba kuanguka alikimbizwa
hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu; hata hivyo juhudi za madaktari
na wauguzi wa hospitali za kuokoa maisha yake zilishindikana kwani
Komba alifariki.
No comments:
Post a Comment