Mapya yameibuka
sakata la kukwama kufungwa kwa ndoa ya Samwel Mwakalobo na Ginen Mgaya, baada
ya kubainika kuwa moja ya sababu ni Bibi harusi mtarajiwa kuendeleza uhusiano
na mzazi mwenzake.
Bwana harusi, Samuel Mwakalobo alitoweka muda mfupi kabla ya
kufunga ndoa na Ginen Mgaya katika Kanisa
la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Isanga jijini Mbeya.
Mwakalobo (26) alizua taharuki hiyo Ijumaa ya Desemba 16, baada ya kutoonekana
kanisani kufunga ndoa mbele ya Mchungaji Andagile Mwakijungu.
Habari zimedai kuwa kabla ya mpango wa kufunga ndoa hiyo,
Mgaya tayari alishapata mtoto kabla hajaolewa, na Bwana harusi kubaini dakika
za mwisho kuwa wawili hao walikuwa bado wana uhusiano wa karibu.
Habari hizo za ndani kutoka familia ya Bibi harusi, zilidai
kuwa kilichofanya Bwana harusi amtelekeze Bibi harusi ni wasiwasi aliokuwa nao
juu ya uhakika wa ujauzito wa mkewe huyo mtarajiwa, kuwa ni wake kweli au wa
mpenzi wake huyo wa zamani.
“Hofu hiyo ilijengeka kutokana na taarifa alizoziamini Bwana
harusi kuwa Bibi harusi anaendeleza uhusiano na mzazi mwenziwe. Ni hofu tu
ambayo angeifanyia kazi na angegundua kuwa haina ukweli wowote,” kilidai chanzo
hicho.
Chanzo hicho kiliendelea kudai: “Unajua muda mwingine
binadamu tunahitaji kufanya uamuzi kwa kutafakari … maana shemeji yetu (Bwana
harusi) alipigiwa simu na mzazi mwenza wa Bibi harusi na kuelezwa maneno ya
‘shombo’ na yeye bila kufanyia utafiti, akaamua kususa harusi.”
Wakati taarifa hizo zikibainisha hayo, familia ya Bwana
harusi imeendelea kufanya jitihada za kuhakikisha suala hilo linamalizika
kistaarabu.
Anayeelezwa kufuatilia suala hilo kwa karibuni ni kaka yake,
ambaye hadi jana jitihada za kumtafuta mdogo wake zilikuwa zimeshindikana
kutokana na kutopokea simu yake ya mkononi mara zote.
“Anayeongoza familia ya Bwana harusi ni kaka yake.
Inasemekana pia kuwa wawili hao waliingia kwenye mgogoro dakika za mwisho kabla
ya harusi na ndiyo maana baada ya kutoweka hataki hata kupokea simu,” kilieleza
chanzo kingine.
Awali, mpambe wa Bibi harusi alieleza kuwa siku mbili kabla
ya harusi hiyo, Bwana harusi alikuwa kwenye migogoro ya kifamilia na ndugu zake
kuhusu fedha za sherehe na mpaka siku ya sherehe, suala hilo walikuwa
hawajalitatua.
“Lakini tunashukuru kaka yake ni mstaarabu, aliamua kuonesha
upendo kwa mdogo wake na amekuwa akilifuatilia suala hilo ili limalizike kwa
amani, lakini mdogo mtu hapatikani,” alisema mpambe huyo.
Alisema jitihada za Bibi harusi kumtafuta Bwana harusi
hazijazaa matunda, kwani hadi juzi alikuwa hapatikani hata nyumbani kwake,
ingawa redio ilikuwa inasikika ndani ya chumba hicho kilichofungwa kufuli kwa
nje.
Simu ya Bwana harusi ilikuwa ikiita muda mwingi bila
kupokewa, lakini hatua zingine zilidai kuwa Bwana huyo ambaye ni mfanyabiashara
kwenye kituo cha mabasi yaendayo Chunya eneo la Isanga jijini Mbeya hajafungua
duka lake.
No comments:
Post a Comment