Balozi wa zamani wa Tanzania kwenye ofisi ya Umoja wa Mataifa
(UN), Dk Augustine Mahiga amesema anafuatwa na makundi ya watu
wanaomshawishi achukue fomu kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano kwa
tiketi ya CCM, lakini hajatoa jibu.
Balozi Mahiga anaingia kwenye orodha ya watu ambao
wamejitangaza au wanatajwa kuwania nafasi hiyo ya juu kwenye siasa
wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba utakaochagua Serikali ya Awamu ya
Tano.
Tayari makada 21 wa chama chake wanatajwa kuwamo
kwenye kinyang’anyiro hicho cha kumrithi Rais Jakaya Kikwete ambaye
anamaliza muda wake wa miaka 10 baada ya kuongoza nchi kwa vipindi
viwili, ambavyo ndio kikomo kwa mujibu wa Katiba.
Tayari makada 21 wa chama chake wanatajwa kuwamo
kwenye kinyang’anyiro hicho cha kumrithi Rais Jakaya Kikwete ambaye
anamaliza muda wake wa miaka 10 baada ya kuongoza nchi kwa vipindi
viwili, ambavyo ndio kikomo kwa mujibu wa Katiba.
Dk Mahiga,(pichani) ambaye pia alikuwa mwakilishi
wa Katibu Mkuu wa UN nchini Somalia, alisema makundi hayo yalianza
kumfuata baada ya Rais Kikwete kutangaza kwenye sherehe za maadhimisho
ya kuzaliwa kwa CCM zilizofanyika Songea kuwa kama wanachama wanaona
kuna mtu anafaa kugombea urais na hajajitokeza, wamfuate na kumshauri
achukue fomu.
“Nimepata makundi ya watu na mtu mmoja mmoja
wakinishauri nichukue fomu ya kuwania urais baada ya Rais Kikwete kutoa
kauli kule Songea mkoani Ruvuma, lakini bado sijakubali wala kukataa
ushawishi huo,” alisema mwanadiplomasia huyo alipoongea na Mwananchi
mara baada ya kuzungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya
Tosamaganga iliyopo Iringa.
Lakini akaongeza kuwa kushawishiwa kuchukua fomu
kwa ajili ya kuwania nafasi hiyo nyeti kwa Taifa, ni jambo moja, lakini
kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho ni jambo jingine akisema kuwa CCM
ina mchakato na masharti ambayo ni lazima yatimizwe.
Hata hivyo, Dk Mahiga hakusita kumwaga sera zake iwapo atajitosa kuwania nafasi hiyo na kuchaguliwa kuongoza nchi.
“Nitaimarisha demokrasia, kuongeza uwajibikaji,
kuimarisha maadili, kuboresha mwelekeo wa uchumi, kilimo, kuimarisha
reli na kupambana na rushwa,” alisema balozi huyo ambaye ni mhitimu wa
shahada ya umahiri ya sanaa.
Kuhusu sifa za mgombea urais, Dk Mahiga alisema ni
vema Rais ajaye akawa na sifa zinazoenea na kuelezeka ili kuweza
kupokea kijiti kutoka kwa Rais Kikwete wa sasa na kulipeleka mbele Taifa
katika kipindi cha miaka mitano mingine. Alisema Rais ajaye anatakiwa
kuwa kiongozi wa watu, aliye tayari kujifunza, kuchukua uamuzi mgumu,
uwezo wa kutawala hasira na kuwa na marafiki.
Pia alisema anatakiwa kuwa na uwezo wa kutatua changamoto ambazo hazijaweza kutatuliwa kwa sasa ikiwemo ya ugaidi.
Nyingine ni kuwaunganisha Watanzania kuwa kitu
kimoja, muadilifu na mwenye mtazamo wa mbali kwa Watanzania na Taifa,
kuhimili mfadhaiko, awe mchapakazi, subira ya kupima mambo na kuwa juu
ya yote kama hasira, wivu na fitina.
Akizungumzia hali ilivyo kwa sasa katika mbio za kuelekea Ikulu,
Dk Mahiga alisema kumekuwepo na hali ya wanaowania nafasi ya urais
kutumia fedha na kuonya kuwa suala hilo linaweza kulifikisha Taifa
mahali pabaya kwa kumpata mtu asiyestahili.
Dk Mahiga aliwahi kuongea na Mwananchi wakati wa mchakato wa Katiba akielezea msimamo wake kuhusu muundo wa Muungano.
Dk Mahiga alisema wakati huo kuwa suala la muundo
wa serikali tatu kwenye Muungano limekuja wakati muafaka kwa kuwa
umekuwa ukilalamikiwa na wananchi wa pande zote kwa muda mrefu na kwamba
Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Kamati ya Mabadiliko iliyokuwea
chini ya Jaji Joseph warioba ilikuwa na jibu la kero za Muungano.
Dk. Mahiga pia amepata kuwa Mwakilishi wa Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini Liberia wakati wa vita vya wenyewe
kwa wenyewe wakati akifanya kazi ya kuongoza shughuli za Shirika la
Kuhudumia Wakimbizi la UN (UNHCR).
Akiwa balozi wa kudumu UN, Balozi Mahiga alisifika
kwa kurejesha heshima ya heshima ya nchi kiasi cha kuwa mojawapo ya
zilizounda Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Katika kipindi cha kati ya mwaka 1980 hadi mwaka
1983, Mahiga alikuwa kaimu mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, nafasi
ambayo ilimpa fursa ya kuifahamu Tanzania nje na ndani.
Dk Mahiga alizaliwa Agosti 28, 1945, ameoa na ana watoto watatu.
Alihitimu shahada yake ya sanaa mwaka 1971 kwenye
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na shahada yake ya uzamili aliipata Chuo
Kikuu cha Toronto. Alipata shahada yake ya uzamivu katika masuala ya
Uhusiano wa Kimataifa kwenye Chuo Kikuu cha U of T mwaka 1975.
No comments:
Post a Comment