Raia wawili wa Burundi wameuawa kwa kupigwa risasi na polisi
katika machafuko yaliyotokea leo huko Bujumbura mji mkuu wa Burundi.
Machafuko hayo ya leo yametokea katika maeneo mengi ya mji mkuu
Bujumbura, wakati watu walipoandama kupinga hatua ya Rais Pierre
Nkurunziza wa nchi hiyo ya kuamua kugombea urais kwa muhula mwingine wa
tatu. Watu walioshuhudia wameongeza kuwa mmoja wa waandamanaji katika
machafuko ya leo huko Bujumbura ameuawa katika wilaya ya Ngagara na
mwingine katika wilaya ya Musaga huko huko Bujumbura. Habari zinasema
kuwa polisi wa Burundi walitumia silaha za moto, gesi ya kutoa machozi
na maji ya kuwasha ili kuwatawanya waandamanaji. Leonce Ngendakumana
Kiongozi wa upinzani kutoka chama cha Frodebu amesema kuwa, wameitisha
maandamano ya amani, hata hivyo polisi na wanamgambo wa chama tawala cha
Burundi wamewafyatulia risasi hai waandamanaji.
No comments:
Post a Comment