Rais
Jakaya Kikwete ambaye pia amiri Jeshi mkuu wa majeshi ya ulinzi na
usalama amewaongoza maelfu ya watanzania katika sherehe za maadhimisho
ya miaka 51 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika katika
uwanja wa uhuru jijini dar es salaam.
Katika maadhimisho hayo yaliyohudhuriwa na maelfu ya
watanzania,mabalozi,viongozi wa serikali na vyama vya siasa,Rais Kikwete
aliingia uwanjani hapo akiwa katika gari la wazi akiwa na mkuu wa
majeshi ya ulinzi Janerali Davis Mwamunyange na kuzunguka uwanja wa
uhuru akiwapungia mkono watanzania.
Rais kikwete kisha alipanda katika jukwaa maalum lililoandaliwa na
kisha mizinga 21 ilipigwa pamoja na wimbo wa taifa na hatimaye alikagua
vikosi mbalimbali vya majeshi ya ulinzi kabla ya kupanda katika jukwaa
kuu nakusalimiana na viongozi waandamizi wa serikali ya jamhuri ya
muungano na serikali ya mapinduzi ya Zanzibar.
Aidha vikosi mbalimbali vya majeshi ya ulinzi vilipita mbele ya
jukwaa kuu na kuonyesha ukakamavu na utayari wa kukabiliana na
changamoto mbalimbali zitakazojitokeza.
Wakizungumza na waandishi wa habari baadhi ya viongozi wastaafu
walioshuhudia mkataba wa muungano mwaka 1964 akiwemo Spika Mstaafu Pius
Msekwa wamewataka vijana kuuenzi muungano Tanzania na Zanzibar huo
hususani katika kipindi hiki taifa linapokabiliwa na uchaguzi mkuu
pamoja na mchakato wa katiba pendekezwa.
Burudani mbalimbali zilipamba sherehe hizo ikiwemo vijana na
halaiki kuchora maumbo na kuandika maeneo mbalimbali,huku kikosi cha
vijana wengine wakionyesha ukakamavu wa kupita kwenye moto pamoja na
kutambaa katika kamba,pamoja na ngoma za asili zilikuwa kivutio kikubwa
uwanjani hapa.
No comments:
Post a Comment