Jana kulikuwa na habari iliyomuhusu mwanamke mmoja wa Dodoma
ambaye alikuwa amepelekwa kituo cha afya cha Muungano wilayani Chamwino
kwa ajili ya kujifungua, lakini akakutana na vitendo vya kikatili
vilivyochangia mtoto afie tumboni.
Kwa mujibu wa habari hiyo, muuguzi aliyekuwa zamu
siku hiyo aliamua kumchapa viboko mjamzito huyo baada ya kumuona
anashindwa kujikakamua ili kumsukuma mtoto atoke na alikuwa akifanya
hayo akidai kuwa mwanamke huyo ni mzembe na anadeka ndio maana alikuwa
anashindwa kujifungua.
Muuguzi mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma
alikiri kuwapo kwa taarifa za mama huyo kuchapwa viboko akiwa chumba cha
kujifungulia na kwamba wameagiza uchunguzi ufanyike ili kupata taarifa
sahihi za tukio hilo na hatua zichukuliwe.
Wakati uchunguzi huo ukifanyika, hatutaki kuamini
kuwa kifo cha mtoto huyo kimesababishwa na kupigwa kwa mama yake, lakini
kinachotushangaza ni jinsi mama huyo alivyoshughulikiwa hadi kupoteza
kiumbe hicho alichokitunza tumboni kwa miezi tisa.
Muuguzi huyo ni mmoja tu kati ya wengi ambao
wamekuwa wakiwafanyia vitendo visivyo sahihi wagonjwa wanapoenda
hospitalini kwa ajili ya kupata tiba, hasa wajawazito ambao hulundikiwa
mzigo wa maneno kuanzia wanapofika hadi wanapojifungua. Imekuwa ni
kawaida kwa kina mama wajawazito kusimangwa, kutolewa maneno machafu na
kucheleweshewa huduma na matokeo yake baadhi hujikuta wakipoteza watoto
na wengine kulazimika kujifungua kwa kufanyiwa upasuaji.
Wengine wamekuwa wakilalamika kuwa wauguzi huwaomba rushwa na wasipotoa, hufanyiwa vitendo hivyo vya kikatili na kudhalilisha.
Mambo hayo husababisha wanawazito wanaoishi kwenye
maeneo ya nje ya miji, kuona ni heri kujifungulia majumbani au kwa
waganga wa jadi ambako wanaona hakuna unyanyasaji kama wanaofanyiwa
hospitalini na matokeo yake hukumbana na athari kubwa zaidi.
Tunatambua kuwa wauguzi wanafanya kazi katika
mazingira magumu kutokana na Serikali kutotenga fedha za kutosha kwenye
sekta hiyo, lakini hatuamini kuwa hali hiyo ndiyo inayosababisha wauguzi
wafanye vitendo vya unyanyasaji kwa wagonjwa, na hasa wajawazito.
Tunaamini kuwa katika mazingira hayo magumu, bado
wauguzi wanaweza kuonyesha moyo wa upendo, kufanya kazi kwa weledi na
maadili angalau kwa kiwango kinacholingana na mazingira waliyonayo ili
juhudi za kuhimiza kina mama wajifungulie hospitalini au kwenye vituo
vya afya zizae matunda.
Itakuwa ni kitu cha ajabu kama Serikali inapiga
kelele kuhimiza wananchi kwenda kwenye vituo vya afya au hospitalini
wakati wauguzi nao wanafanya vitendo ambavyo vinakatisha tamaa wananchi
kwenda sehemu hizo.
Wakati mama huyo akiendelea kupata matibabu kwenye
Hospitali ya Mkoa ya Dodoma, ni vizuri kwa uongozi wa mkoa kufanya
uchunguzi wa kina kama ulivyoahidi ili kupata taarifa sahihi za tukio
hilo lililotokea Aprili 3 mwaka huu, takriban siku 20 zilizopita.
Imekuwa ni kawaida kwamba tukio lolote baya
likiripotiwa na vyombo vya habari, wahusika huwa wepesi kusema
wanafuatilia kupata taarifa kamili na wanapoona hali imepoa, nao
wanachana nalo na hakuna hatua zinazochukuliwa. Matokeo yake ni vitendo
hivyo kuendelea kuwa sugu.
Hatutarajii kwamba uongozi wa mkoa wa Dodoma utaingia kwenye
mkumbo huo wa kusubiri hali ipoe, bali utatekeleza ahadi yake ya
kufanyia kazi taarifa hizo ili wahusika wachukuliwe hatua.
Na kwa kuwa huduma duni ni tatizo sugu hospitalini
na kwenye vituo vya afya na hospitalini, Serikali haina budi kufuatilia
vitendo hivyo ili kuvikomesha.
No comments:
Post a Comment