Sunday 26 April 2015

Chadema yajipanga kuifanyia kufuru CCM

Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) kimeweka mkakati utakaowafanya makada wake wavamie majimbo yanayoshikiliwa mapema na CCM, huku wakichelea kuingia kwenye majimbo yaliyo chini ya chama hicho kikuu cha upinzani.
Mkakati huo ulitangazwa jana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Mongella mjini hapa, mkutano ambao ulifurika maelfu ya watu.
Mbowe alitangaza kupiga marufuku wanachama wa Chadema kuanza kutangaza nia kwenye majimbo ambayo wenzao wanayashikilia hadi hapo Bunge la Jamhuri ya Muungano litakapovunjwa.
Lakini alisema wanachama wa Chadema wanaruhusiwa kuanza purukushani kwenye majimbo ambayo yanashikilia na vyama vingine hasa chama tawala cha CCM ambacho kinashikilia majimbo mengi.
“Naomba ifahamike Chadema ni zaidi ya ubunge, tunahitaji amani na siyo kuharibu chama. Chadema itasimamisha watu makini kwenye maeneo yote katika uchaguzi huu,” alisema mwenyekiti huyo ambaye yuko kwenye ziara ya mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Mbowe ambaye hakugusia suala la Ukawa katika mkutano huo, alisema kuwa utaratibu utaandaliwa wa kupata wagombea na kwamba hata waliokuwa wabunge, wasijihakikishie kuwa watapitishwa tena kwenye maeneo yao wanayoyaongoza sasa.
“Tutakuja na utaratibu mwingine. Hata wabunge wa Chadema waliokuwa katika maeneo hayo, wasidhani kwamba watabakia hapo. Tutasimamisha mtu anayekubalika na watu wote, na utaratibu ukiwekwa, hata aliyekuwa mbunge anaweza kuondolewa,” alisema Mbowe.
Alisema kuwa Chadema inaamini kuwa katika kila eneo kuna mtu wake ambaye ni makini na ni wazi atashinda.
Vyama vinne vya upinzani, Chadema, NLD, NCCR-Mageuzi na CUF vimekubaliana kusimamisha mgombea mmoja kuanzia kwenye uchaguzi wa madiwani hadi rais. Vyama hivyo, vilivyo chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vimekubaliana kuwa kila chama kipate mgombea wake na baadaye vitachambua anayekubalika na wengi.
Ainanga Nec
Akizungumzia mwenendo wa uboreshaji wa Daftari la Wapigakura, Mbowe alisema Taifa kwa sasa liko kwenye giza nene kutokana na maandalizi mabovu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi(Nec).
Mbowe alisema kucheleweshwa kwa kazi ya uandikishaji wapigakura ni sehemu ya njama za CCM kupitia Serikali yake inayotamani kutumia nafasi hiyo ili kuendelea na hujuma katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Mbowe, ambaye aligombea urais mwaka 2005, alisema Nec inachelewesha kazi hiyo ili kuibeba CCM katika uchaguzi mkuu kwani kukamilika kwa daftari hilo kunaonekana kunaitia hofu CCM.
“Kuna wananchi wengi, zaidi ya milioni 26 wanatakiwa kuandikishwa na muda uliobakia ni mfupi. Walichelewesha kwa makusudi ili kuisaidia CCM iendelee kututawala kwa nguvu ya watu wachache watakaokuwa na sifa za kupiga kura, “ alisema.
“Kwa njama hizo, tunamuomba Rais (Jakaya) Kikwete amalizie muda wake kwa amani na asituharibie amani ya nchi yetu kwa kutengeneza hujuma. Bora amalize muda wake ili akapumzike kijijini kwao.”
Mbowe alisema mpaka sasa Rais Kikwete ndiye wa kulaumiwa kwa maandalizi hayo ya Uchaguzi Mkuu kutokana na dalili zinazoonekana kwa sasa.
“Kampeni ni siku 72 kabla ya Uchaguzi Mkuu na mpaka sasa ni miezi mitatu tu imebakia kabla ya kuanza kampeni, lakini hakuna dalili za maandalizi yoyote. Haya yote yamechangiwa na Serikali yenye maandalizi mabovu,” alisema Mbowe.
Mbowe pia alishangazwa na kitendo cha Serikali kutumia fedha nyingi katika mchakato wa Katiba bila mafanikio yoyote yale, lakini hakuna kiongozi aliyewajibishwa kwa hasara hiyo.
Katika hatua nyingine, Mbowe alifafanua kuhusu urais nafasi ya urais kupitia Ukawa akisema, kwa sasa lengo lao kwa pamoja siyo bora kupata urais, bali ni kuangalia kiongozi gani atakayesimama kuwakilisha Ukawa katika nafasi hiyo.
“Kwa hivyo CCM na watu wengine wasidhani kwamba Ukawa tutagombana kwa sababu hiyo, tumejipanga na dhamira yetu ndiyo nguvu ya Watanzania walioridhia kuungana kwetu. Tunaamini CCM lazima ing’oke katika uchaguzi huu,” alisema Mbowe.
Katika hatua nyingine, Mbowe pia aliwaonya baadhi ya wanasiasa wanaounda Ukawa, kuanza kutangaza nia kwenye majimbo yenye wabunge kwa sasa. Alisema nafasi hiyo ya kutangaza nia itapatikana baada ya Bunge kuvunjwa.
Mafunzo ya FP200
Akizungumzia mkakati wa kutoa mafunzo kwa vijana wa chama hicho FP200, Mbowe alisema kuwa hata kama IGP ataweka pingamizi, lazima watatekeleza azimio hilo. Alisema IGP, akitaka kuwakachukulia hatua basi, yeye atakuwa muhusika namba moja.
“Hata Jeshi la Polisi wakizuiua lazima mafunzo yatafanyika na kama wanataka kuchukua hatua basi Mbowe akamatwe,” alisema Mbowe.

No comments: