Monday, 20 April 2015

Lowasa amshinikiza Kikwete asaini kunyongwa kwa wauaji wa maalbino

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ameitaka jumuiya ya albino nchini kuisukuma Serikali ili Rais Jakaya Kikwete asaini utekelezaji wa hukumu ya kuwanyonga wauaji wa albino.
Kauli ya Lowassa imekuja wiki moja tu baada ya Rais Kikwete kusema hajapelekewa majina ya watu 16 waliohukumiwa kifo kutokana na mauaji ya albino kutokana na mlolongo mrefu wa kisheria uliopo kabla ya kumfikia.
Rais Kikwete alisema hayo wakati wa ibada maalumu ya kuwekwa wakfu Askofu Liberatus Sangu kuwa Mhashamu Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga.
Hata hivyo, jana Lowassa aliyekuwa mgeni rasmi katika kampeni ya matembezi kupinga mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) yaliyoandaliwa na Klabu za Mbio za Pole ya Temeke na kushirikisha vikundi mbalimbali vya Dar es Salaam, alisema: “Ninampongeza Rais Kikwete kutokana na jitihada zake za kukemea mauaji ya albino. Pia, nimesikia kuna watu sita wametakiwa kunyongwa lakini kwa maelezo ya Rais hukumu hizo hazijamfikia, hivyo nawaomba mfanye msukumo ili Rais asaini.”
Kutokana na kukithiri mauaji hayo, Lowassa aliiomba Serikali kuunda kamati maalumu itakayokuwa ikichunguza mauaji ya walemavu hao bila kutegemea kamati za mikoa ili kuongeza ufanisi wa kuilinda jamii hiyo.
Mwanasiasa huyo anayetajwa kutaka kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu ujao, aliuambia umati uliokusanyika katika viwanja vya TCC Chang’ombe kuwa suala la ulinzi wa albino si la Serikali pekee bali la wananchi wote.
Mapema Machi mwaka huu, Mahakama Kuu ya Tanzania iliwahukumu watu wanne kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na kosa la kumuua Zawadi Magindu (32) mwenye ulemavu wa ngozi, mkazi wa Kijiji cha Nyamaruru, Wilaya ya Geita.
Kifungo cha CCM
Awali wakati akitoa hotuba yake Lowassa alisema kutokana na kifungo alichowekewa na CCM hawezi kuzungumza mambo mengi kwa sababu yatamletea balaa.
“Kule CCM bado nina kifungo, nikisema mengi nitaleta balaa,” alisema huku akishangiliwa na kundi la vijana waliokuwapo uwanjani hapo.
Lowassa yupo kifungoni na makada wengine watano ambao ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Januari Makamba, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Mbunge wa Sengerema William Ngeleja, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Stephen Wasira na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye.
Aliyekuwa mbunge wa Temeke (CCM), John Kibaso alisema Lowassa alikubali kuwa mgeni rasmi baada ya kumuomba aridhie ombi hilo kutokana na mambo yake ya kisiasa yanayomkabili.
“Awali mgeni rasmi ilibidi awe mbunge wa Ilala, Mussa Zungu lakini ikabidi tumuombe Lowassa aliyetuambia kuwa anaogopa CCM kwa kuwa haijaruhusu mambo hayo.
Hata hivyo, ndani ya wiki moja mzee wetu alikubali kushiriki nasi kama mlivyomuona,” alisema Kibaso.
Katika maandamano hayo Lowassa aliviongoza vikundi mbalimbali vya mbio za pole katika matembezi ya haraka kutoka Uwanja wa Taifa hadi viwanja vya TCC Chang’ombe.
Pia aliongozana na Mbunge wa Temeke (CCM) Abbas Mtemvu, Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan na Zungu.
Mwenyekiti wa chama cha watu wenye albino Tanzania (TAS), Ernest Kimaya alisema ukataji wa viungo na kuuawa kwa watu wenye ualbino umetia doa nchi jambo ambalo linapaswa kukemewa na wadau mbalimbali.
Alisema mauaji hayo yameongezeka kwa kasi kuanzia mwaka 2006 ambapo hadi sasa watu wenye ulemavu huo wameuawa 75, waliojeruhiwa kwa kukatwa viungo ni 35 na makaburi 15 yalifukuliwa na kuchukuliwa viungo vya mwili.

No comments: