Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea amesema atamfikisha mahakamani Spika wa Bunge, Job Ndugai kwa kuvunja kanuni baada ya kuwaingiza polisi ndani ya ukumbi wa chombo hicho.
Polisi hao waliingia ndani ya ukumbi huo wiki iliyopita wakati Rais John Magufuli alipofika kwa ajili ya kuhutubia Bunge.
Kubenea
alisema kitendo cha askari kuingia ndani ya Bunge kwa mara ya mwisho
kilitokea nchini Uingereza mwaka 1930 na hakijawahi kutokea tena
isipokuwa nchini.
Alisema kuwa kesi hiyo anatarajia kuifungua Mahakama Kuu wiki ijayo kwa ajili ya kutaka tafsiri ya kanuni hiyo.
Hata
hivyo, mkurugenzi wa shughuli za Bunge, John Joel alisema hakuna kanuni
iliyovunjwa kwa askari hao kuingia ndani ya Ukumbi wa Bunge.
Wakati Kubenea akiandaa mpango huo, Kamati ya Wabunge CUF imesema Spika Ndugai ndiye chanzo cha yaliyotokea bungeni.
Ijumaa
wiki iliyopita wakati Rais akiingia kutoa hotuba ya kuzindua Bunge,
wabunge hao walipiga kelele wakitaja jina la mgombea urais wa Zanzibar
kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kuonyesha msimamo wao dhidi
ya uamuzi wa kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa visiwa hivyo.
Walipiga
kelele hizo wakati Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed Shein akiingia kwenye
ukumbi huo na baadaye wakati Dk Magufuli akiingia ukumbini na wakagoma
kunyamaza hadi walipotakiwa kutoka nje na askari kuitwa ndani.
Wabunge
wa upinzani wanadai kuwa Dk Shein si Rais wa Zanzibar, wala makamu wake
wa pili, Balozi Seif Ali Iddi na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu
Ameir Kificho kwa madai kuwa muda wao uliisha Novemba 2, baada ya
Uchaguzi Mkuu.
Jana
wabunge wa CUF chini ya Mwenyekiti wake, Juma Hamad Omary walitoa tamko
lililokemea na kutoa tahadhari kwa mambo mawili huku wakimtaka Ndugai
kutoyumbishwa na Serikali.
No comments:
Post a Comment