Saturday 14 November 2015

Ubelgiji yashauri raia wake waondoke Burundi

Burundi
Raia wa Burundi wamekuwa wakitoroka mitaa mingi ya mji wa Bujumbura
Ubelgiji imewashauri raia wake kuondoka Burundi, huku Muungano wa Ulaya nao ukipunguza maafisa wake wanaohudumu huko kutokana na kuongezeka kwa machafuko.
Balozi wa EU nchini humo Patrick Spirlet amesema hatari ya kutokea mapigano zaidi imeongezeka.
Hayo yamejiri huku idara ya Amani ya Usalama ya Muungano wa Afrika ikikutana mjini Addis Ababa kujadili mpango wa kutuma walinda amani nchini humo.

Kamishna wa Amani wa AU Smail Chergui amesema atatuma maafisa nchini Uganda kuandaa mazungumzo kati ya Rais Nkurunziza na upinzani.
Watu zaidi ya 200 wameuawa tangu Aprili Rais Nkurunziza alipotangaza kuwa angewania urais kwa muhula wa tatu. Alishinda uchaguzi mwezi Julai.
Mnamo Alhamisi, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kauli moja lilipitisha azimio lenye mapendekezo mengi yakiwemo uwezekano wa kutumwa kwa walinda Amani, na kuwekwa kwa vikwazo.
Kiongozi mmoja wa upinzani nchini Burundi tayari ameuhimiza Umoja wa Mataifa kutuma walinda usalama nchini humo.
Charles Nditije, mkuu wa kundi la upinzani la UPRONA, ameambia shirika la habari la Reuters kwamba wanafurahishwa na juhudi za UN kuhimiza mashauriano lakini wamevunjwa moyo na kutoumwa kwa walinda Amani na kutoafikiwa kwa maelewano kuhusu vikwazo.

No comments: