Sunday 16 August 2015

Msafara wa Lowasa wapigwa mabomu jana jijini Arusha

Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward
Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa akizungumza na polisi kwenye Daraja la Nduruma mjini Arusha, baada ya kufunga Barabara ya Sabasaba wakati akitokea kwenye Uwanja wa Tindigani. Polisi walimkubalia kupita barabara hiyo na kuzuia msafara wake
 
Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema na Ukawa, Edward Lowassa jana kwa mara ya kwanza alikumbana na joto la upinzani baada ya msafara wake kushambuliwa na mabomu ya polisi.
Tukio hilo, ambalo lilifanyika mbele ya msafara wa Lowassa, lilitokea jana eneo la Daraja la Nduruma katika Jiji la Arusha na kusababisha umati wa watu kutawanyika na wengine kutelekeza magari yao.
Wakati Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akimkaribisha kwenye chama hicho wakati wa mkutano mkuu alimwambia; “Mzee huku inabidi uwe unafanya mazoezi kidogo, kuna mabomu huku.”
Lowassa alikumbwa na kadhia hiyo, akiwa njiani na mgombea mwenza, Juma Duni Haji na viongozi wengine wa Ukawa, wakitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), huku wakiwa wamesindikizwa na umati wa watu na magari.
Tamko la polisi
Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema kuwa polisi walilazimika kupiga mabomu ya machozi ili kutawanya watu waliokuwa wakiwarushia mawe polisi na wengine kufunga barabara.
“Kwa hali ile, tungefanya nini? Wanatupa mawe kwa polisi na wamefunga barabara na kuzuia magari mengine yasipite…ikumbukwe kulikuwa hakuna kibali cha maandamano na hata kingekuja, matamko ya kuzuia maandamano yameshatolewa,” alisema Sabas.
Katika tukio hilo, idadi kubwa ya polisi walikuwa kwenye magari na silaha mbalimbali ambao baadaye walianza kurusha mabomu kutawanya watu na magari kwa eneo la daraja hilo.
Hata hivyo, katika tukio hilo, lililotokea saa nane mchana hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa na kutokana na nguvu hiyo ya polisi watu walitawanyika, na barabara hiyo ya Arusha- Moshi ilifunguka baada ya kutopitika kwa saa tano kuanzia saa nne asubuhi.
Ukawa walaani kupigwa mabomu
Akizungumza katika mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Tindigani, Mbunge wa jimbo la Arusha, Godbless Lema alisema wamesikitishwa na kitendo cha polisi kumpiga mabomu Lowassa na msafara wake.
“Tunajua polisi wamepata maelekezo na sasa wanataka kuwatisha wananchi, lakini tunasema leo ndiyo mwisho hatutakubali tena kunyanyaswa,” alisema Lema.
Kuwasili Lowassa
Lowassa aliwasili KIA saa 3:20 asubuhi akiwa ameongozana na viongozi wa Ukawa, Mbowe, Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia na Mwenyekiti wa NLD, Emmanuel Makaidi, Kaimu Mwenyekiti wa CUF taifa, Twaha Taslima na viongozi wengine.
Kwenye Uwanja wa KIA, shughuli mbali mbali zilisimama katika eneo la kushuka viongozi mashuhuri (VIP), ambapo mawaziri kadhaa walikuwa katika eneo hilo.
Baadhi ya viongozi hao ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Juma Hassadi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Dk Mary Nagu, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tzeba.
Baada ya Lowassa kutua KIA, alikwenda moja kwa moja kwenye Hoteli ya KIA Lodge na mgombea mwenza wake, Juma Duni Haji kwa mapumziko mafupi.
Baada ya kupumzika saa 5:30 msafara ulianza kuelekea uwanja wa Tindigani Kimandolu na ulifika saa tisa na kukutana uwanja ukiwa tayari umefurika maelfu ya watu.
Akihutubia mkutano huo Lowassa alitahadharisha viongozi wa polisi, kuacha kutumia nguvu kupita kiasi, kwani anaweza kuwafikisha Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) iliyopo The Hague nchini Uholanzi.
Lowassa alisema alikuwa akiiamini polisi, lakini alichokiona jana cha kupigwa mabomu ni jambo baya.
Kuhusu suala la Babu Seya aliyefungwa kifungo cha maisha gerezani alisema atafuatiliwa kwa kutumia suala la utawala bora kwa kuangalia vyombo vya sheria na hatua zingine zitafuatwa.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema wanachama wanaojiunga sasa wana haki sawa na mwasisi wa chama hiki Edwin Mtei mwenye kadi namba moja.
Alisema mara baada ya wanachama wapya kujiunga, kwa kipindi cha wiki moja nilipokea matusi mengi kuliko niliyowahi kutukanwa baada ya kupokea wanachama wapya.
Kaimu Mwenyekiti wa CUF, Taslima alisema kuna watu ambao wamejenga desturi ya kuwabeza watu wanapohama vyama kwa hiari kwa kuwaita oili chafu au makapi anavunja Katiba.
Alisema Ibara ya 20 ya Katiba ya mwaka 1977 inasema kila mtu yeyote ambaye ni Mtanzania, yuko huru kujiunga na mtu yeyote, chombo chochote, taasisi yoyote atakayopenda na hatazuiliwa.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema; “Mabomu yamepigwa katika mkutano wa Chadema, watu wakafa Arusha, Arusha tunayoitegemea kwa uchumi leo hii zaidi ya asilimia 19 ya pato ya taifa linatokana na utalii, lakini leo (jana) tunaingia Arusha alipozaliwa Lowassa tunapigwa mabomu, ukweli utatuweka huru.

No comments: