Monday 3 August 2015

Watu milioni 1.6 wamdhamini Lowassa

Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa akipungia
Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa akipungia wananchi wakati akiondoka kutoka makao makuu ya Chadema Kinondoni, Dar es Salaam jana, baada ya kurudisha fomu ya kugombea urais kupitia chama hicho

 Naibu katibu mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu alisema idadi hiyo ya wadhamini inaashiria ushindi wa kishindo, kwa maelezo kuwa inakaribia idadi ya kura alizopigiwa katibu mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa alipogombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.


Kada mpya wa Chadema, Edward Lowassa jana amerejesha fomu ya kuwania urais, huku akifanikiwa kupata wadhamini milioni 1.6, zaidi ya nusu ya kura za urais ambazo chama hicho kilipata kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.
Naibu katibu mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu alisema idadi hiyo ya wadhamini inaashiria ushindi wa kishindo, kwa maelezo kuwa inakaribia idadi ya kura alizopigiwa katibu mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa alipogombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Katika Uchaguzi huo, Dk Slaa alishika nafasi ya pili baada ya kupata kura 2,271,941 sawa na asilimia 26.34, huku Rais Jakaya Kikwete akipata kura 5,276,827 sawa na asilimia 61.17.
Lowassa alipochukua fomu za kuomba kuteuliwa kuwania urais kwa tiketi ya CCM, kabla ya kuhamia Chadema, alidhaminiwa na wanachama 870,000 nchi nzima.
Dk Slaa, ambaye hajaonekana hadharani tangu Lowassa ajiunge Chadema, jana hakuwapo kwenye ofisi za chama hicho wakati mbunge huyo wa Monduli alipokuwa akirejesha fomu.
Hakuna kiongozi aliyekuwa tayari kuzungumzia suala lake, lakini baadhi ya maofisa wa Chadema walisema wanaendelea kuchapa kazi.
Kama ilivyokuwa juzi katika hafla fupi wakati Lowassa akichukua fomu, umati mkubwa ulifurika na kusababisha Mtaa wa Ufipa uliopo Wilaya ya Kinondoni kufungwa, watu walijazana tena na safari hii umati huo ukiwa umebeba mabango ya kumsifu Waziri Mkuu huyo wa zamani.
Katika hafla ya jana, makamu mwenyekiti wa Chadema-Bara, Profesa Abdallah Safari alieleza jinsi Chadema ilivyojipanga kuchukua nchi na siyo kushinda ubunge na udiwani pekee na kwamba Lowassa amebakiza hatua mbili tu kuingia Ikulu, jambo walilodai kuwa limeichanganya CCM.
Wakati Lowassa ambaye alitangaza rasmi kujiondoa CCM na kujiunga na Chadema Julai 28 mwaka huu akisubiri kupitishwa na Mkutano Mkuu wa chama hicho utakaofanyika Agosti 4, habari za ndani zinaeleza kuwa vigogo kadhaa wa CCM watatambulishwa katika mkutano huo.
Habari hizo zinaeleza watakaotambulishwa siku hiyo ni wenyeviti wa CCM wa mikoa, wilaya na waliokuwa wabunge wa chama hicho ambao wanamuunga mkono Lowassa.
Jana Lowassa, aliyekuwa amevaa shati jeupe na suruali nyeusi na aliyekuwa katika gari aina ya Toyota Land Cruiser VX, alifika makao makuu ya Chadema saa 9:35 alasiri akiwa pamoja na familia yake na alipokewa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali.
Baadhi ya ujumbe huo ni “Chini ya Lowassa umaskini haupo”, “Kwa Lowassa hata maskini atapata ajira” na “Kingunge Ngombare-Mwiru karibu Ukawa”. Kingunge ni kada mkongwe wa CCM na anamuunga mkono Lowassa.
Mbali na kubeba mabango, watu hao walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za kumsifu Lowassa na kushangilia pale ilipokuwa ikitajwa mikakati ya chama hicho kushika dola.
Kura milioni 1.6
Akieleza taratibu na kanuni za kudhamini mgombea urais, mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa chama hicho, Benson Kigaira alisema mgombea urais anatakiwa kudhaminiwa na wanachama wasiopungua 200.
“Naamini fomu za Lowassa zitakuwa na idadi hiyo ya wadhamini. Ila baada ya mgombea kuchukua fomu jioni yake wanachama wa Chadema, wapenzi na Watanzania walifurika katika ofisi za Kanda, mikoa na majimbo nchi nzima wakiomba kumdhamini,” alisema Kigaira.
Alisema wanachama hao walidhani fomu hizo zimepelekwa kila mkoa, kutokana na kuepuka kuwanyima fursa hiyo chama hicho kilipeleka fomu ili wanachama wamdhamini na kupewa masharti kuwa lazima wawe wamejiandikisha kupiga kura, wataje namba zao za simu.
Huku akionyesha fomu chache za wadhamini kutoka mikoa mbalimbali nchini, Kigaira alitaja idadi ya watu waliomdhamini Lowassa katika mikoa yote 32 kuwa ni 1,662,397.
Akizungumzia udhamini wa wanachama Mwalimu alisema: “Lowassa alitakiwa azunguke mikoani kusaka wadhamini ila siku zilikuwa zimebaki mbili. Tuliwataka wanachama wanaotaka kumdhamini (Lowassa) wafike makao makuu, siku uliyochukua fomu. Wanachama 700 walikuja kukudhamini.”
Alisema kitendo hicho kiliiibua malalamiko kutoka kwa wanachama wa mikoa mbalimbali nchini, hivyo kuagizwa fomu za udhamini zipelekwe mikoani.
Safari ya Lowassa haitavurugwa
Katika maelezo yake, Mwalimu alisema CCM inafanya vikao ili kuivuruga Chadema, lakini akasema kuwa hilo halitafanikiwa na hakuna wa kuivuruga safari ya Lowassa.
“Tunajua kuna mikakati na vikao vinavyoendelea kwa nia ya kumzuia Lowassa katika safari hii ya Chadema na Ukawa, lakini tunawaambia Lowassa kuja Chadema ni mpango wa Mungu. Hatujamuokota barabara, ni Mungu amemuongoza kuja chama chetu kwa sababu Mungu ameshakiandikia neema chama hiki kutokana na falsafa inazokisimamia tangu kuanzishwa kwake.”
“Njama zozote za kishetani, kihafidhina na kifedhuli zitalegea na kupotezwa. Lowassa amebakiza hatua mbili, ya kwanza ni kumaliza mchakato wa ndani ya chama kupitia Mkutano Mkuu na hatua ya pili ni kuapishwa.”
Mwalimu alisema Chadema inaunga mkono kauli ya Lowassa ya kuuchukia umaskini, kwamba nchi imeshindwa kupata maendeleo kutokana na kuongozwa na viongozi wa CCM wenye fikra za kimaskini, za kuamini ili uwe kiongozi lazima uwe maskini.
Alisema baada ya Lowassa kupitishwa na Mkutano Mkuu chama hicho, atazunguka mikoa mbalimbali nchini kuanzia Dar es Salaam Agosti 9.
Lengo ni kuchukua nchi
“Kuna watu walidhani Lowassa hawezi kurejesha fomu. Safari ya kuelekea uchaguzi mkuu imefikia hatua muhimu. Kinachofuata ni Kamati Kuu kupitisha fomu hizi. Naamini hakuna pingamizi lolote maana mpaka sasa hakuna aliyejitokeza kuchukua fomu za kugombea urais kupitia Chadema na Ukawa,” alisema Profesa Safari.
Alisema wapo wanaosema mwaka huu wapinzani wataambulia wabunge na madiwani tu siyo rais, jambo alilodai kuwa si kweli na kwamba lengo lao ni kushinda kiti cha urais.
“Wazanzibari wana msemo wao kwamba goli unafungwa, lakini chenga twawala. Sisi chenga tutapiga na magoli tutafunga,” alisema.
Vigogo CCM
Habari za ndani kutoka chama hicho zinaeleza kuwa vigogo wa CCM watatambulishwa kabla ya kuanza kwa Mkutano Mkuu wa chama hicho, wakiwemo wabunge mashuhuri.
“Siku ya mkutano mkuu watatambulisha wabunge na viongozi wa CCM. Ni wengi na wengine watawashangaza watu kwa kweli kwa sababu si watu wanaotarajiwa kuihama CCM, “ alisema mpashaji habari wetu.
Mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye ndiye anayeambatana na Lowassa na amehudhuria hafla zote za uchukuaji na urejeshaji fomu, mara zote akiulizwa amekuwa akijibu kuwa ni mshauri wa mbunge huyo wa Monduli wa masuala ya kupambana na rushwa.
Chizii agoma kuzungumza
Naye kada mkongwe wa CCM, Matson Chizii ambaye naye amekuwa bega kwa bega na Lowassa tangu ahamie Chadema, alipoulizwa kama amehamia katika chama hicho kikuu cha upinzani nchini alisema hana cha kujibu, kusisitiza kuwa atajibu suala hilo siku mbili zijazo.

No comments: