Waziri
wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amerejea kauli yake ya kwamba
Serikali ya Marekani inamtaka awe mrithi wa Rais Jakaya Kikwete mwakani.
Tangu
mwaka 2012, Nyalandu amekuwa akisisitiza kuwa Rais Barack Obama pamoja
na uongozi mzima wa Marekani, wanataka ashike nafasi hiyo kubwa kwa kile
anachosema wanaridhishwa na kipaji chake cha uongozi.
Awali,
waziri huyo anayetajwa kuwa wakala wa taifa hilo lenye ushawishi mkubwa
duniani, alitoa kauli hiyo kwenye hafla iliyoshirikisha watu walio
karibu naye.
“Wakati
huo tulidhani anatania, lakini sasa amekuwa akipita huku na kule nchini
akisisitiza kuwa Rais Obama amenuia kuhakikisha yeye (Nyalandu) anakuwa
Rais wa Tanzania mwaka 2015,” amesema mmoja wa watu walio karibu naye.
Akiwa
mkoani Mbeya hivi karibuni, Nyalandu amenukuliwa akijipigia debe la
urais kwa kusema: “Watanzania wahakikishe wanapata rais aliyeandaliwa na
Mungu ili kuweza kuwavusha kutoka walipo kuelekea kwenye nchi ya neema
kutokana na utajiri mkubwa wa rasilimali tulizo nazo.”
Mgombea
huyo kwa sasa anakabiliwa na shinikizo linalotokana na utendaji kazi
wake mbovu, amebuni mpango wa kuwapoza wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kwa kuwaandalia safari nje ya
nchi.
Hata
hivyo, taarifa zinasema wajumbe kadhaa wa Kamati hiyo waliokutana wiki
iliyopita jijini Dar es Salaam walipinga kwa nguvu zote mpango huo,
wakisema hiyo ilikuwa ‘rushwa’ ili wasiweze kuhoji utendaji kazi mbovu
wa Nyalandu.
Miongoni
mwa wajumbe ambao chanzo chetu kinasema walikuwa mstari wa mbele
kupinga mpango huo ni Mbunge wa Viti Maalum, Esther Bulaya (CCM).
"Esther
alitoa hoja nzuri sana. Alihoji iweje waziri kabla ya kuwasilisha
ripoti yake kwa wajumbe aanze kuwapa ‘habari njema’ ya kuwapa safari za
nje ya nchi. Wajumbe wengi waliunga mkono hoja hiyo na mwisho wa siku
ikawa safari hizo zimekataliwa na wajumbe,” mmoja wa wabunge ameiambia waandishi wa habari.
Kwa upande wake, Bulaya ameulizwa na waandishi wa habari na kusema: “Siwezi kusema mengi, lakini ni kweli mjadala ulikuwa mkali.”
Ripoti
ya Wizaya hiyo ambayo Nyalandu alikuwa aiwasilishe kwenye kikao hicho,
ilikwama kuwasilishwa baada ya wabunge hao kuipinga wakisema ni nyepesi
mno.
“Ilikuwa ripoti ya ajabu sana, ilikuwa shallow (haikuwa ya kina) sana, haikuwa na mambo mazito ambayo tulitarajia kuyaona,” alisema mjumbe mwingine.
Habari
za uhakika zilisema Nyalandu alikuwa amerejea Dar es Salaam kutoka nje
ya nchi saa kadhaa kabla ya kwenda kuwasilisha ripoti hiyo kwa wabunge,
hatua ambayo ilionekana wazi kwamba hata yeye alikuwa hajui kilichomo.
Kama
ilivyotarajiwa, Mwanyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi,
Maliasili na Mazingira, James Lembeli, alijaribu kumtetea Nyalandu
akiwasihi wajumbe watulie wajue kilichomo. Madai yake yakawa kwamba hata
kama kuna kasoro, hilo lilikuwa kosa la wasaidizi wa Waziri kwa hiyo wa
kulaumiwa ni wao.
Kauli
hiyo ilipingwa na wajumbe ambao walisema ilimradi ripoti hiyo inayo
saini ya Nyalandu, basi yeye ndiye anayewajibika kwa upungufu wote.
Mjumbe
mwingine (jina tunalo) akasema wajumbe wanataka maelezo kuhusu kashfa
ya uuaji wanyamapori 704 kwa kutumia Leseni ya Rais ambayo Nyalandu
alimwamuru Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori awape rafiki zake
Wamarekani.
Walitaka
maelezo kuhusu kashfa ya kujigawia vitalu vya miti inayomkabili Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahmoud Mgimwa, na walitaka kujua
matumizi ya fedha zinazodaiwa kutumiwa na Nyalandu kuwahudumia wasanii
anaokwenda nao ughaibuni. Matumizi ya fedha kwa ajili ya malipo ya
hoteli za kitalii Dar es Salaam na Arusha; mgongano wa kiutumishi kati
yake na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Maimuna Tarishi, na mengine mengi.
“Ile
ripoti haikuwa na kitu, ilikataliwa na akatakiwa aondoke. Ilipofika
kwenye saa nne tukaahirisha kikao. Akaondoka na wataalamu wake.
Aliagizwa ajipange upya awasilishe ripoti inayolingana na uzito wa
Wizara na tuhuma zinazowakabili,” kimesema chanzo chetu.
Chanzo
kingine cha habari kinasema Nyalandu alisema anaandamwa kwa fitina na
magazeti mawili (hakuyataja) kwa sababu ya utendaji wake wa kazi, hasa
kwa kuwa amewadhibiti majangili na mafisadi. Hata hivyo, utetezi huo
ulipingwa na mmoja wa wajumbe aliyehoji: “Unasema unaandamwa na magazeti
kwa mambo yasiyo ya kweli! mbona magazeti yanaandika na kutoa
vielelezo? Kwanini wewe usitoke ukazungumza na waandishi wa habari na
wewe ukatoa vielelezo vyako vya kukanusha kama kweli ni ya uongo?
Pamoja
na kubanwa kwa swali hilo, Nyalandu akaendelea kusisitiza kuwa
anaandamwa kwa sababu amegusa maslahi ya mafisadi ambao amewafutia kile
alichokiita 'ulaji wa rasilimali za nchi'.
Hata
hivyo, Nyalandu ndiye anayehusishwa mno na matumizi mabaya ya madaraka
pamoja na utoro kazini. Mara nyingi amekuwa akisafiri nje ya nchi, na
hata anapokuwa nchini, amekuwa akitumia muda mrefu Dar es Salaam na
Arusha. Wiki mbili zilizopita, katika kuonesha ‘wizara ina waziri’
alitumia ndege kuzuru maeneo kadhaa yakiwamo ya Mbeya, Njombe, Singida,
Tabora, Arusha, na Kilimanjaro. Pia alikwenda Serengeti kinyemela kupata
taarifa za kuuawa kwa ndovu kadhaa.
Amejitahidi
kuzima habari zinazohusu matukio ya kuuawa kwa ndovu kwa kile
kinachoelezwa kuwa ni kutaka kuuhadaa umma kwamba amefanikiwa kwenye
mapambano dhidi ya ujangili.
“Hakuna
habari ya kuuawa ndovu ambazo utaziona; mtasikia habari za kukamatwa
pembe tu. Magazeti hayaandiki. Mitandao ya kijamii (ukiwamo mtandao
maarufu nchini) haiandiki tena habari za kashfa za Nyalandu, na hata
zile zilizokuwamo zimefutwa au kufungwa kabisa. Amehakikisha kila mahali
anadhibiti,” kimesema chanzo chetu.
mwandishi wetu aliripoti kwa kina juu ya Nyalandu kuwa na safari na wasanii wawili, Aunty Ezekiel na Kassim Mganga.
Licha
ya Aunty Ezekiel kukanusha juu ya ziara hiyo ya kikazi ya Nyalandu,
lakini Mganga kwa upande wake ameibuka na kuthibitisha kwamba safari
hiyo iliratibiwa na Nyalandu.
Mganga
aliyekwepa kuzungumza Ijumaa iliyopita, siku moja kabla
taarifa zake zilisomeka kwenye gazeti la HabariLeo, toleo Na. 02864 la
Alhamisi ya Oktoba 23, mwaka huu.
Katika kurasa za katikati za gazeti hilo linalomilikiwa na Serikali, Mganga amesema walipelekwa Marekani na Nyalandu.
Msanii
huyo aliyerejea hivi karibuni kutoka huko Ughaibuni katika tamasha
aliloliita ni la kutangaza utalii wa Tanzania nchini humo, anasema
ametengeneza mtandao kwa ajili ya kazi za nje.
Mganga
anasema huko alifanya kazi kama ya kutoa burudani, akiwa na Msanii wa
maigizo Aunt Ezekiel na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu
ambaye ndiye aliyewapeleka.