Saturday, 6 December 2014

Danny Sserunkuma (Simba) na Emerson Oliveira wawakuna wengi

Simba yamnasa Danny Sserunkuma.
katikati ni Dany sserukuma
Usajili wa nyota wapya wa kigeni umegeuka kete ya ushindi kwenye mechi ya Nani Mtani Jembe 2 baina ya Simba na Yanga inayotarajiwa kuchezwa Desemba 13 jijini Dar es Salaam.
Jana, viongozi wa klabu hizo walitambiana, wakiwataja nyota wao wapya, Danny Sserunkuma (Simba) na Emerson Oliveira kuwa ndio wataziwezesha klabu zao kuibuka na ushindi.
Wakizungumza kwenye ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Simba ilijinasibu kuwa imesajili mtambo wa mabao, wakati Yanga ikijibu kuwa itamweka mfukoni kupitia kiungo wao, mpya Mbrazili Emerson.
Msemaji wa Simba, Humphrey Nyasio alisema: “Sisi ndiyo mabingwa watetezi wa Nani Mtani Jembe, tulishinda mabao 3-1 mwaka jana, hivyo kwa mwaka huu tutatoa kipigo kikali zaidi kwani tumesajili mtambo wa mabao ambao utaanza kazi siku hiyo, tumemsajili Sserunkuma, kazi kubwa iliyomleta hapa ni kufunga mabao, hivyo Yanga wajiandae kuona moto wake,” alisema msemaji huyo.
Meneja masoko wa Yanga ambaye aliiwakilisha klabu hiyo, George Simba alijibu: “Sisi tutahakikisha pesa zote, Sh80 milioni tunazoshindania tunazipata, pia, tunapata kombe na ushindi kwenye mchezo huo.
“ Pia, mashabiki wetu wajiandae kupata vionjo vipya vya Kibrazili na ujio wa Emerson utaigaragaza Simba na kuandika historia mpya,” alisema meneja huyo.
Wakati hayo yakiendelea, wapenzi wa Yanga wamewafunika wale wa Simba kwenye upigaji kura za kuwania Sh80 milioni za kampeni ya Nani Mtani Jembe ambayo hukamilika kwa mchezo baina ya Simba na Yanga.
Matokeo yaliyotangazwa jana na meneja wa bia ya Kilimanjaro, Pamela Kikuli yanaonyesha kuwa Yanga tayari wamejinyakulia Sh70 milioni wakati Simba wanazo Sh10 milioni.
Naye Meneja Udhamini wa TBL, George Kavishe alisema: “Tayari, Simba na Yanga zimesaini makubaliano ya kucheza mechi ya Nani Mtani Jembe 2, zimeahidi kuwatumia wachezaji wa vikosi vya kwanza, wakiwamo wale waliopo kwa kipindi kirefu na wale waliosajiliwa.”
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alitangaza viingilio vya mchezo huo akisema Jukwaa la VIP A itakuwa Sh30,000, VIP B Sh20,000, huku VIP C ikiwa ni Sh15,000.
Kwa upande wa viti vya rangi ya chungwa tiketi ni Sh15,000 huku kwa upande wa viti vya rangi ya bluu na kijani kiingilio kitakuwa ni Sh7,000.
Pia Wambura aliongeza kuwa kama ilivyo kawaida ya pambano hilo, hakutakuwa na muda wa nyongeza, iwapo timu zitakwenda sare ndani ya dakika 90, mshindi atapatikana kwa penalti.

No comments: