Leonard Mubali ameandaa taarifa ifuatayo:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Dar es Salaam, imesema Rais Jakaya Kikwete amekubali ombi hilo la kujiuzulu kwa Mwanasheria Mkuu huyo wa Serikali.
Katika barua yake kwa Rais Kikwete, Jaji Werema amesema ameomba kujiuzulu kwa sababu ushauri wake kuhusiana na suala ya Akaunti ya Tegeta Escrow haukueleweka na umechafua hali ya hewa. Rais Kikwete amemshukuru Jaji Werema kwa utumishi wake ulioongozwa na uaminifu na uadilifu.
Baada ya uchunguzi kuwasilishwa katika mkutano wa bunge uliomalizika mwishoni mwa mwezi Novemba, kamati hiyo ilikuja na maazimio manane kuhusu taarifa ya ukaguzi maalum kuhusiana na miamala iliyofanyika katika akaunti ya Escrow ya Tegeta pamoja na umiliki wa kampuni ya IPTL.
Miongoni mwa maazimio ya bunge yaliwataja baadhi ya wanasiasa, mwanasheria mkuu, maafisa waandamizi wa serikali, majaji, wakuu wa taasisi za umma, viongozi wa dini, mawakili wa kujitegemea na watu binafsi kuhusika katika kashfa hii na hivyo kuagiza mamlaka zinazohusika kuwachukulia hatua za kisheria wahusika na wengine kuondolewa katika nyadhifa zao za kuteuliwa.
Pia maazimio ya Kamati ya kudumu ya bunge ilipendekeza kuwa, kwa miaka mingi mikataba mibovu ya kuzalisha umeme kati ya Tanesco na makampuni binafsi imeisababishia Tanesco hasara ya mabilioni ya fedha na kutishia uhai wake wa kifedha, serikali iwasilishe mikataba husika bungeni au kwenye kamati zake kwa lengo la kutekeleza vema wajibu wake wa kuimamia na kuishauri serikali.
Akaunti ya Escrow ilianzishwa katika Benki Kuu ya Tanzania ili kuhifadhi fedha, baada ya kuibuka kwa mvutano kati ya Shirika la Umeme la Tanzania, Tanesco na kampuni ya kufua umeme ya IPTL kuhusu ongezeko la mtaji wa uwekezaji, huku TANESCO ikilalamika kuwa gharama za kununua umeme kutoka kampuni ya IPTL zilikuwa za juu mno. Fedha hizo zingeendelea kutunzwa katika Akaunti hayo hadi wakati ambapo suluhisho la mvutano wa wabia hao wawili lingepatikana
No comments:
Post a Comment