Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete amemteua Profesa Mussa Juma Assad kuwa Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Taarifa iliyotolewa leo, Jumatatu, Desemba Mosi,
2014 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, inasema kuwa uteuzi
wa Bwana Assad ulianza Novemba 5, mwaka huu, 2014.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa Bwana Assad ataapishwa kesho, Jumanne, Desemba 2, saa nne asubuhi, Ikulu, Dar es Salaam.
Kabla ya uteuzi wake, Bwana Assad alikuwa Profesa
Mshiriki, Idara ya Uhasibu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na anachukua
nafasi ya Bwana Ludovick Utouh ambaye amestaafu kwa mujibu wa Sheria za
Utumishi wa Umma.
Profesa Assad ni msomi, mwenye weledi, ujuzi na
uzoefu mkubwa wa uhasibu na udhibiti wa fedha ambaye ana Shahada ya
Uzamivu wa Uhasibu (PHD in Accounting) kutoka Chuo Kikuu cha
Southampton, Uingereza mwaka 2001 na Shahada ya Uzamivu katika Udhibiti
wa Fedha (MA in Financial Accounting) kutoka Chuo Kikuu cha Dublin City,
Jamhuri ya Ireland mwaka 1991.
Profesa Assad pia ana Stashahada ya Kitaaluma ya
Uhasibu (Professional Diploma in Accounting) kutoka Chuo Kikuu cha
Dublin City mwaka 1990 na Shahada ya Biashara (Bachelor of Commerce) ya
Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam mwaka 1988.
Pamoja na uzoefu wa kitaaluma, Profesa Assad anao
uzoefu mkubwa katika eneo la uhasibu na ukaguzi. Alikuwa Mwenyekiti wa
Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi (NBAA) kwa miaka saba (2007 - 2014); ni
Rais na Mjumbe wa Chama cha Wahasibu Afrika (Pan African Federation of
Accountants) tangu mwaka 2012; na ni mjumbe wa Bodi kadhaa za
Wakurugenzi nchini Tanzania.
Katika kumteua Profesa Assad kuwa Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Rais anayo imani kubwa kuwa elimu,
weledi, ujuzi na uzoefu ambao Profesa Assad anao utamwezesha kutekeleza
vema majukumu ya nafasi hiyo muhimu sana katika utawala bora wa nchi
yetu.
No comments:
Post a Comment