Saturday, 31 January 2015

Matola aachia madaraka Simba

Klabu ya Simba imethibitisha kuachana na kocha msaidizi wa timu hiyo, Seleman Matola na kueleza kumweka hadharani mrithi wake atakayesaidiana na kocha mkuu, Goran Kopunovic wakati wowote kuanzia sasa.
Mapema jana, Rais wa Simba, Evance Aveva alieleza kupokea barua ya kujiuzulu kwa Matola na kubainisha kuwa katika barua hiyo, Matola ameeleza kutingwa na majukumu ya kifamilia hivyo hawezi kuendelea kuinoa Simba kama kocha msaidizi.
Alipotafutwa na gazeti kuzungumzia uamuzi wake huo, Matola alitaka aulizwe vizuri Aveva ndiye alitolee ufafanuzi suala hilo na si yeye kwani tayari ameachana na klabu hiyo.
Hata hivyo, kocha huyo alionekana kupoteza mvuto kwa baadhi ya mashabiki ambao mara kadhaa wamekuwa wakimshinikiza ang’atuke Simba.
Kwa mujibu wa Aveva, Simba imepokea barua ya kujiuzulu kwa kocha huyo juzi ikiwa ni siku moja baada ya Simba kuruhusu kipigo cha magoli 2-1 dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Taifa.
Pia, Aveva amekiri jahazi la timu yao kuendelea kuzama kutokana na kutoka sare mfululizo na kupoteza mechi mbili kwenye ligi na kuwa timu ya nne kutoka mwisho na pointi 13 katika mechi 11 ilizocheza.
“Ni kweli timu yetu inakwenda mrama, matokeo tunayopata hayaridhishi hata kidogo, kama uongozi tulikutana na benchi la ufundi kuhusu hali ya timu yetu ambao wametuambia ni kutokana na ratiba ya ligi kuwabana.
“Leo, kocha Goran Kopunovic anatimiza siku 30 tangu alipoanza kuinoa Simba, katika kipindi hicho ameiongoza Simba kucheza mechi kumi na kwa uwiano katika kila siku tatu wanacheza mechi moja.
“Kwa hali hii, timu inachoka, wenzetu Yanga na Azam walitolewa mapema, hivyo kupata muda zaidi wa kujiandaa tofauti na sisi ambao tumecheza hadi mwisho,” alisema Aveva.
Akizungumzia mpasuko katika klabu yao, Aveva alisema hawana mpasuko wowote na sasa wanajipanga ili kuhakikisha timu yao inarejesha makali kwenye ligi kwa kushirikiana pamoja na kuwataka mashabiki kuwa na subira.

Waliopanga mbivu za kupindua serikali Gambie waingia matatani

Rais wa Gambia
Waendesha mashtaka nchini Marekani wamewafungulia mashtaka raia wa tatu wa Marekani kwa kuhusika kwenye njama ya mapinduzi nchini Gambia.
Alagie Barrow aliye na uraia wa Marekani na Gambia alifikishwa mahakamani kwenye jimbo la Minnesota akikabiliwa na mashtaka ya kuendesha harakati za kijeshi dhidi ya nchi rafiki.
Taarifa ya mahakama ilisema kuwa bwana Barrow alishukiwa kusaidia kupanga mapinduzi hayo.
Mapinduzi hayo yalifeli wakati walinzi wa rais walipowafyatulia risasi wale waliojaribu kuendesha mapinduzi hayo ambayo baadaye walisafiri kwenda nchini Marekani ambapo walikamatwa.

Man city na Chelsea Kujua mbivu mbichi leo

Chelsea John Terry
Mshambuliaji wa Chelsea Diego Costa hatoshiriki katika mechi dhidi ya Manchester City baada ya kupatikana na hatia ya ukosefu wa nidhamu katika mechi ya semi fainali ya kombe la League Cup dhidi ya Liverpool.
Cesc Fabregas ,Branislav Ivanovic na Felippe Luis wote walijeruhiwa katika mechi hiyo ya ushindi wa kombe la League Cup na ni Ivanovic pekee anayetarajiwa kucheza leo.
mancity
Nyota wa kilabu hiyo Yaya Toure na mshambuliaji Wilfried Bonny hawatashirik baada ya imu yao ya taifa kusonga mbele katika mechi za robo fainali za Afrika hatua ambayo inawalazimu wote kusalia Afrika.

Msanii Knight akamatwa kwa mauaji

Polisi nchini Los Angeles inasema kuwa msanii wa muziki wa rap kutoka Marekani Marion Suge Knight amekamatwa kutokana na mashtaka ya mauaji baada ya kumgonga mtu mmoja na gari lake hadi kumuua na baadaye kutoroka.
Polisi wanasema kuwa bwana Knight alijibizana na watu wawili katika eneo la kuegesha magari na baadaye kumgonga mmoja wao huku mwengine akijeruhiwa vibaya.
Wakili wake anasema ilikuwa ajali na kudai kuwa mteja wake alishambuliwa na watu wawili.
Suge Knight ni mwanzilishi wa kampuni ya Death Row Records ambayo iliwazindua wasanii maarufu wa mziki wa rap akiwemo Snoop Dogg na marehemu Tupac Shakur.

Wizi wa kupindukia Wwagundulika

zitto ATAARIFA ya mwaka ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ya hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu na mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2013, imebua wizi wa kutisha wa fedha za umma uliofanywa na taasisi hizo.
Hayo yalibainika jana wakati Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, alipokuwa akiwasilisha ripoti ya kamati hiyo, ambapo alisema katika ripoti za ukaguzi kwa Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL), imebainika kuwa ililipa mabilioni ya fedha kwa ajili ya ndege iliyoikodi kutoka Shirika la Ndege la Wallis Trading Inc la China, ndege ambayo ni hewa kwa kuwa haipo nchini.
“Hadi sasa Serikali imelipa dola za Marekani 26,115,428.75, (Sh bilioni 45.17) na sasa inadaiwa dola za Marekani 23,996,327.82 (Sh bilioni 41.51), ndege hiyo ilikuwa mbovu na ilifanya kazi nchini kwa miezi sita pekee badala ya miaka sita kama mkataba wa ubinafsishwaji ulivyotaka,” alisema Zitto katika taarifa yake.
Taarifa hiyo ya PAC, ilibainisha pia kuwa katika ujenzi wa jengo la watu mashuhuri (VIP) katika Uwanja Ndege wa Kimatifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, kuna ufisadi wa takriban Sh bilioni tisa.
Ilisema pia jengo hilo lilianza kujengwa bila kibali cha Baraza la Mawaziri na kuwa thamani ya gharama za ujenzi wa jengo hilo hazijulikani kwa kuwa nyaraka muhimu hazipo.
Kwa upande wa Mamlaka ya Bandari (TPA), imebainika kutumia Sh bilioni 9.6 kwa ajili ya vikao vya wafanyakazi na mamilioni mengine kujilipa kwa ajili ya posho za safari bila kuwa na kibali kutoka serikalini.
Zitto alisema pia kamati yake imebaini kuwa misamaha ya kodi imezidi kuongezeka na kufikia Sh trilioni 1.8 mwaka 2014, huku zaidi ya Sh bilioni 80.45 za misamaha hiyo kwa mwaka zikitumika kwa njia zisizo halali.
“Mbali na hilo, pia fedha za pembejeo za kilimo zimekuwa zikitumika visivyo halali na kwa zao la korosho, zaidi ya Sh bilioni moja zilitumika kinyume cha taratibu,” alisema Zitto.
Kwa upande mwingine, ripoti hiyo imesema mifuko ya hifadhi ya jamii ipo hoi kutokana na Serikali kushindwa kulipa deni la Sh trilioni 1.87 ilizokopa.
Pamoja na hilo, taarifa ya PAC imesema pia Serikali ina hatihati katika hisa zake zilizopo katika Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), endapo hatua za kulipa deni la Sh bilioni 22 hazitachukuliwa hadi kufikia Machi 31.

Lisu atamani kwenye amri Za Mungu iongezwe amri isemayo CCM iondolewe


Wabunge wameendelea kuchangia taarifa za Kamati za Hesabu za Serikali PAC na LAAC zinazoonesha ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma. Hapa chini nimekuwekea michango ya baadhi ya Wabunge.
Lema: Haiwezekani kila siku tukija humu tunazungumzia wizi tu, inatakiwa tuzungumzie mipango ya maendeleo ya wananchi sio kila siku wizi wizi wizi unaosababishwa na CCM.
Lema: Kama ningeweza kupendekeza pia kwenye Amri Kumi za Mungu, ningependekeza iongezwe amri ya 11 inayosema 'USIWE CCM'
Lema: Katika mazingira kama haya, nathubutu kusema 'My Country is like a Getho' mambo hayaendeshwi kwa utaratibu kabisa

Esther Bulaya: "Yani watu wanagawana posho Bilion 9, na wanafunzi wanasoma kwa shida halafu mnataka tuwapigie makofi haiwezekani"
Esther Bulaya: "Hatuwezi kila siku tunakuja hapa majibu yaleyale kila siku wizi wizi wizi, haiwezekani, hawa watu washughulikiwe"

Lissu: "Kinachotufikisha hapa ni Rais kushindwa kutimiza wajibu wake wa kikatiba wa kuwawajibisha watendaji wake"

Lissu: "Tunachotakiwa kufanya hapa ni kuanza na hawa mawaziri tulionao humu ndani, tukubaliane kuwawajibisha"

Friday, 30 January 2015

Diego Costa kuikosa Man city kesho

Diego Costa
Mchezaji wa Chelsea Diego Costa amepigwa marufuku ya mechi tatu kwa kumkanyaga makusudi mchezaji wa Liverpool Emre Can.
Costa mwenye umri wa miaka 26 atakosa mechi ya wikendi dhidi ya Mancity pamoja na mechi dhidi ya Aston Villa na Everton.
Shtaka hilo ambalo Costa alilikana linatokana na kisa cha mchuano wa kombe la leage Cup raundi ya pili ambapo Chelsea iliibuka kidedea.
Costa aliyesajiliwa kwa kitita cha pauni millioni 32 ana mabao 17 katika mechi 19 za ligi ya Uingereza msimu huu.
Kisa hicho hakikuonekana na maafisa waliosimamia mechi hiyo lakini kilionekana katika kanda ya video.

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ndio mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika -Au

Rais mkongwe wa Zimbabwe Robert Mugabe, mwenye umri wa miaka tisini, sasa ameteuliwa kuwa mwenyekiti wa muungano wa Afrika-AU.
Wajumbe walimteuwa Mugabe kwa kauli moja katika mkutano wa AU unaoendelea mjini Addis Ababa-Ethiopia.
Uteuzi wa Mugabe kuongoza muungano huo mkubwa ulio na wanachama zaidi ya arubaini, sasa umeingiza doa ndani ya AU, kwani Mugabe hana uhusiano mzuri na mataifa ya Magharibi, hasa baada ya kukaa uongozini tangu Zimbabwe ilipojipatia uhuru mnamo mwaka wa 80.

Mwalimu ashikiliwa Mkoani Kilimanjaro kwa kumbaka mwanafunzi

Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linamshikilia mwalimu mmoja wa shule ya sekondari kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa kidato cha tatu na kumuumiza sehemu za siri.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Koka Moita alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 11:45 katika chumba cha maabara shuleni hapo.
Kamanda Moita alisema mwalimu huyo alimwita mwanafunzi huyo katika chumba hicho na kuanza kumtomasa mwilini na baadaye alimvua nguo kwa nguvu, kisha kumuingilia.
Alisema kutokana na maumivu aliyoyapata alipelekwa Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi kwa matibabu. Kamanda Moita alisema mtuhumiwa baada ya kutenda kosa hilo alikamatwa.
Katika tukio jingine; Faustine Macha (45) ameuawa kwa kupigwa na rungu kichwani na kuvunjwa miguu kisha kutupwa shambani.
Kamanda Moita alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 12:00 jioni katika Kijiji cha Kinango wilayani Moshi Vijijini. Alisema marehemu alipigwa na watu wawili baada kulewa na kuanza kutukanana.
Kamanda Moita alisema watuhumiwa hao wanashikiliwa kwa tuhuma za mauaji. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Kilema.

Kiongozi wa Makaburu aachiliwa Huru Afrika Kusini

Eugene Alexander de Kock
Kiongozi wa zamani wa utawala wa kiimla wa makaburu nchini Afrika Kusini na ambaye alikuwa kinara wa kuongoza kitengo hatari cha kuwatesa watu weusi, Eugene de Kock, amesamehewa, kuhurumiwa na kuondolewa gerezani.
Eugene Alexander de KOCK alikuwa akitumikia hukumu ya mauwaji na mateso kwa wakereketwa wengi wa chama cha ANC, lakini sasa waziri wa haki na sheria Nchini Afrika Kusini, Michael Masutha, amesema kuwa de Kock ameachiwa huru kwa manufaa ya umoja wa kitaifa.
Alikuwa ametubu mbele ya tume ya haki na maridhiano kwamba alikuwa amesababisha zaidi ya vifo vya watu mia moja na pia kuhusika katika vitendo vya kuwatesa watu kinyama na ufisadi, hasa akiwalenga waliokuwa wakipinga utawala wa ubaguzi wa rangi.
Kanali huyo wa zamani wa polisi aliyekuwa na mataji mengi mno alisamehewa kwa mengi ya makosa aliyofanya, lakini akazuiliwa gerezani kwa makosa dhidi ya binadamu kabla ya kufungwa jela maisha.
Tarehe ya kuachiwa huru kwake kwa sasa bado ni siri.

Awatisha watangazaji kwa bunduki bandia studioni

Mwanamume aliyekuwa ameshika bunduki bandia amekamatwa ndani ya studio ya matangazo ya televisheni nchini Uholanzi na kusababisha matangazo kusitishwa kwa muda.
Wafanyakazi waliamrishwa kutoka nje ye jengo lenye studio hizo katika eneo la Media Park mjini Hilversum.
Mtu huyo aliyekuwa amevalia suti akiwa amebeba kilichofanana na bunduki, aliingia katika studio hizo na kutaka apewe muda wa kuongea hewani.
Baadaye polisi walifanikiwa kumkamata baada ya kumshinda nguvu.
Maafisa wa polisi walisema mwanamue huyo anazuiliwa kwa kosa la kushukiwa kutoa vitisho , kumiliki silaha na kumteka mtu.
Polisi walifanya msako katika jengo hilo na kuhakikisha hali kuwa shwari.
Waziri wa usalama Ivo Opstelten alisema mshukiwa alikuwa pekee yake katika njama yake.
Nia na lengo la kitendo cha mwanamume huyo hata hivyo haikubainika. Vyombo vya habari nchini Uholanzi, viliripoti kwamba mshukiwa aliaminika kuwa mwanafunzi wa chuo cha mafunzo ya anuai na kwamba aliwapoteza wazazi wake hivi karibuni.
Mshukiwa alinaswa akisema :''vitu ambavyo nitavisema , ni mambo makubwa ya kidunia.Tulikodiwa na shirika la ujasusi.''
Barua yenye vitisho ambayo mwanamume huyo aliikabidhi kwa wafanyakazi wa kituo hicho ilionya dhidi ya mashambulizi ya bomu na uvamizi wa mitandao ikiwa angezuiwa kwenda hewani.Barua hio ilichapishwa kwenye mtandao wa kituo hicho.
Mwandishi mmoja wa habari aliyezungumza na mshukiwa huyo, alisema alidai kutoka kwa kundi la wavamizi wa mitandao, "hackers' collective"
Mwanamume huyo alikuwa amevalia shati leusi na tai huku akiwa amebeba kilichoonekana kama bunduki nyeusi na alionekana kwenye video akiwa anatembea tembea kwenye studio.
Polisi walipoingia katika kituo hicho, waliamwamrisha kuiangusha bunduki yake kitendo alichokifanya huku polisi wakimfunga pingu mikononi.

Lusinde awapongeza Polisi kwa kumpiga Lipumba

Kulikuwa  na  mvutano  mkali  sana  bungeni  wakati  wabunge  wakijadili  hoja  ya  Lipumba  kupigwa. Hapo  chini  nimekuwekea  michango  ya  Lusinde  na  Sadifa  waliyoitoa  Bungeni:
  Lusinde: Kwani kupigwa Lipumba ndiyo tatizo, wamepigwa viongozi wangapi hapa, Lipumba siyo wa kwanza kupigwa 
Lusinde: Nawapongeza Polisi safari hii kapigwa muhusika mwenyewe, ndiyo nzuri hiyo, siyo wapigwe wengine, kupigwa kazini ndiyo sawa

Lusinde: Bunge linapokwenda mwishoni wabunge wenye hali mbaya majimboni wanakuwa na hamsha hamsha ili wafikiriwe
 
Lusinde: Nawashauri wapiga debe mkiona watu wanaandamana magari hayatembei hampati pesa na nyinyi andamaneni.
  
Sadifa: Mnasema Lipumba kapigwa, hajapigwa hapo, kaguswa tu, huwezi kumlinganisha Lipumba na Kikwete.

Kipigo cha Lipumba chazua mtafaruku

http://mtanzania.co.tz/wp-content/uploads/2015/01/Pg-110.jpg
Prof Ibrahim Lipumba akiwa Kizimbani
WAKATI Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba akipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana, Bunge lilivunja kikao chake baada ya kuibuka mjadala mkali kutoka kwa wabunge wa kambi ya upinzani.
Spika wa Bunge, Anne Makinda, alilazimika kuahirisha Bunge baada ya wabunge hao wa upinzani kutaka shughuli za Bunge ziahirishwe ili wajadili kitendo cha Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam kumpiga Profesa Lipumba na wenzake.
Tukio hilo lilitokea jana saa 4 asubuhi baada ya Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), kuomba mwongozo akitaka tukio hilo lijadiliwe kwa masilahi ya taifa.
Katika mwongozo wake, Mbatia alitumia kanuni ya 47 inayoeleza jinsi mbunge anavyoweza kusimama na kuomba mwongozo kwa spika akitaka shughuli za Bunge za siku hiyo ziahirishwe ili suala muhimu lijadiliwe kwa masilahi ya taifa.
Katika mwongozo wake, Mbatia, alisema kitendo kilichofanywa na polisi hakiwezi kuvumiliwa kwa kuwa kimekiuka haki za binadamu kwa vile Profesa Lipumba na wananchi wengine walipigwa bila sababu za msingi.
“Mheshimiwa Spika, juzi Januari 27, mwaka huu kule Temeke, Dar es Salaam, Profesa Lipumba alikuwa na ratiba ya mkutano wa hadhara na maandamano.
“Lakini, dakika za mwisho kabla ya mkutano huo, polisi walizuia mkutano usiendelee na baadaye wakaamua kuwapiga raia wasiokuwa na hatia, akiwamo Profesa Lipumba, wafuasi wa CUF, watoto walio chini ya miaka mitano pamoja na waandishi wa habari.
“Mheshimiwa Spika, jambo hilo linaonyesha hali ya hatari, na mimi nilisikitika sana nikalazimika kumpigia simu Waziri wa Mambo ya Ndani kumweleza hali ilivyokuwa mbaya.
“Kibaya zaidi, polisi wenyewe wamesema walilazimika kufanya hivyo kwa sababu walipokea maagizo kutoka juu. Kwahiyo, Mheshimiwa Spika, tusipoziba ufa, tutajenga ukuta.
“Mheshimiwa Spika, ni miaka michache tu tumeshuhudia polisi wakiua raia, wakiua waandishi wa habari na raia wakiua polisi, lazima mambo haya tuyakemee kwa nguvu zote kama tunataka kujenga taifa lenye umoja.
“Kwahiyo, Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja, tuahirishe Bunge ili tujadili jambo hili lisije likajirudia tena, naomba kutoa hoja,” alihitimisha Mbatia.
Pamoja na hayo, Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, alisema kitendo cha kumpiga Lipumba kinaweza kuhatarisha amani nchini kwa kuwa anaongoza wabunge zaidi ya 30 walioko bungeni na pia ni kiongozi wa chama kinachounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Kisiwani Zanzibar.
SPIKA ATOA MWONGOZO
Baada ya Mbatia kusema hayo, wabunge wote wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni walimuunga mkono kwa kusimama.
Wakati wabunge hao wamesimama, Spika Makinda alisimama tena na kusoma kifungu cha nne cha kanuni ya 47 iliyotumiwa na Mbatia.
Katika maelezo yake, alizungumzia kifungu hicho na kusema kinaruhusu jambo la dharura kujadiliwa kama spika atakuwa ameridhika nalo. Kwa hiyo, aliagiza shughuli za Bunge ziendelee, lakini akaiagiza Serikali itoe kauli bungeni juu ya tukio hilo.
“Kanuni ya 47 kifungu cha nne, kinanipa mamlaka kuahirisha shughuli za Bunge ili jambo la dharura lijadiliwe kama nitaridhishwa nalo. Kwahiyo, naiagiza Serikali ilifuatilie jambo hili, itoe kauli kamili hapa leo na nitaruhusu mjadala,” alisema Spika Makinda na kutaka shughuli za Bunge ziendelee kama zilivyokuwa zimepangwa.
WAPINZANI WAMGOMEA
Majibu ya Spika Makinda yalionekana kuwatibua wabunge wa upinzani, kwani walianza kuzungumza bila utaratibu wakionyesha kutoridhishwa na uamuzi huo.
Kutokana na hali hiyo, Spika mara kadhaa alilazimika kusimama huku akiwaomba wakae ili shughuli za Bunge ziendelee, lakini hawakumsikiliza na badala yake waliendelea kupiga kelele.
“Jamani nawaomba mkae chini na kama mnataka kutoka nje tokeni. Nawaambia jambo hili mnalolizungumza ni kubwa sana na tumelizungumza asubuhi mimi na Mbatia, Mnyaa na Tundu Lissu, nawaomba mkae chini msitake kunifanya kama Kangaroo Court,” alifoka.
Hata hivyo, kauli hizo hazikusaidia kitu, wabunge waliendelea kupiga kelele wakitaka suala hilo lijadiliwe wakati huo.
Baada ya kelele kuzidi, Spika alilazimika kuahirisha Bunge hadi jana saa 10 jioni.
MAHAKAMANI
Jijini Dar es Salaam, Profesa Lipumba (62), alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za kushawishi wafuasi wa chama chake cha CUF kutenda kosa la jinai.
Profesa Lipumba aliyekamatwa pamoja na wenzake zaidi ya 30, alifikishwa mahakamani hapo saa 8 mchana na kusomewa mashtaka yanayomkabili peke yake mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Isaya Arufani.
Mshtakiwa huyo alifika mahakamani saa 7.45 mchana na ilipofika saa 9 alasiri, alipandishwa ukumbi namba mbili wa mahakama.
Alisomewa mashtaka yanayomkabili na Wakili wa Serikali, Joseph Maugo, akishirikiana na Wakili Hellen Moshi.
Wakili Maugo, alidai kati ya Januari 22 na 27, mwaka huu mkoani Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa mwenyekiti wa CUF, aliwashawishi wafuasi wake kufanya kosa la jinai.
Profesa Lipumba, akitetewa na jopo la mawakili watano, wakiwamo Mohammed Tibanyendera, Peter Kibatala, John Mallya na wengine, alikana kutenda kosa hilo kwa kusema ni shtaka la uongo.
Wakili Maugo, alidai upelelezi haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo na kwamba hawakuwa na pingamizi kuhusu mshtakiwa kupewa dhamana.
Upande wa utetezi uliiomba mahakama kumpatia mshtakiwa masharti nafuu kwa kuwa ana wadhamini wanaoaminika.
Hakimu Arufani, alisema mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana iwapo atasaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni mbili, na kuwa na wadhamini wawili watakaotia saini dhamana ya kiasi hicho cha fedha.
Profesa Lipumba alitimiza masharti hayo baada ya kudhaminiwa na Diwani wa Kata ya Saranga, Kinondoni, Hilda Mtiya na Mbunge wa Viti Maalumu, Kuruthum Jumanne. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 26, mwaka huu.
Wafuasi wa CUF waliofurika mahakamani hapo, walitoka mahakamani wakiwa na furaha, huku wakiimba wakati wakielekea lango la kutokea mahakamani.
Baada ya Profesa Lipumba kukamilisha taratibu za dhamana, aliwasihi wafuasi wake kuondoka katika eneo la mahakama kwa hali ya amani na utulivu, akidai wakifanya vurugu wanaweza kukamatwa. Wafuasi hao walitii amri na kutawanyika.
HALI ILIVYOKUWA
Wanachama na wafuasi wa CUF walizingira Kituo Kikuu cha Kati cha Dar es Salaam wakisubiri kujua hatima ya mwenyekiti wao, Profesa Lipumba, aliyekuwa anatarajiwa kufika kituoni hapo kuripoti kwa kosa la kuandamana bila ya kuwa na kibali.
Baada ya askari kuona umati huo, walianza kuutawanya eneo hilo kwa madai hawakutakiwa kuwapo, kauli ambayo waliitii na kuhamia ng’ambo ya barabara.
Ilipofika saa 4.42 asubuhi, Profesa Lipumba alifika akiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili T 467 BLJ hali iliyosababisha wafuasi na mashabiki wa chama hicho kutoka barabarani na kusogea jirani na lango la polisi, huku wakimpa moyo kwa kutoa salamau ya ‘haki’, wengine wakiitikia ‘sawa’.
Alipoingia ndani ya kituo cha polisi kwa ajili ya kujua hatima yake, hakukaa muda mrefu alirudi nje na kuzungumza na waandishi wa habari na kuwaeleza kuwa polisi wamemruhusu kuondoka kutokana na mashtaka yake kutoandaliwa.
“Tuliitwa kuja hapa na sisi tumetii, ila wametuomba tuje leo, kwa sababu walikuwa hawajaandaa ‘charge sheet’ kwa ajili ya kutupelekea mahakamani kwa kosa la kuandamana bila kibali,” alisema.
Profesa Lipumba, alisema kitendo cha kukamatwa ni mwendelezo wa matukio yanayofanywa na Serikali kwa ajili ya kuiminya demokrasia ya vyama vingi, ambavyo vimeonekana kuwa tishio kwa kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“CUF tuliomba kibali Januari 22, mwaka huu na kutoa taarifa kwa wanachama wetu, lakini polisi wakatoa majibu ya kukataa Januari 26, mwaka huu saa 12:30 muda ambao tulikuwa tumefunga ofisi zetu.
“Kwa muda huo naamini polisi walijua isingekuwa rahisi kuwazuia wanachama wetu kusitisha maandamano hayo, hali iliyonifanya niamini walipanga kuwadhuru wanachama wetu,” alisema Lipumba.
Alisema aliamua kuchukua busara na kwenda maeneo ya Temeke kuwazuia wanachama wao wasiandamane kama ambavyo polisi walikuwa wamewaamuru.
“Niliwaomba polisi waliokuwa pale Temeke waniruhusu nikawazuie wanachama waliokuwa uwanja wa Zakhem ambao walikubaliana na mimi, lakini tukiwa njiani kwenye mzunguko wa barabara ya Mbagala, nilisimamishwa nikawaeleza wale polisi waliokuwa pale ambao walionekana kunielewa.
“Tukiwa tunajiandaa na viongozi wenzangu kuondoka, alikuja ofisa mmoja wa polisi, mweusi hivi, ambaye alikuwa na kitambi cha bia za rushwa, akawaamuru polisi kutupiga na kutukamata… Kambaya alipigwa ngeu kichwani,” alisema.
Profesa Lipumba, alisema tukio hilo analitafsiri kama njia ya ukombozi ipo wazi kwa CUF na washirika wao wa Ukawa katika uchaguzi mkuu ujao.
“Nilijiuliza kwanini mwaka huu polisi wametumia nguvu kubwa wakati kila mwaka tumekuwa tukikutana kwa ajili ya kuwakumbuka ndugu zetu waliouawa kule Zanzibar Januari 27, 2010,” alisema Lipumba.
Naye wakili wa Profesa Lipumba, Hashim Mziray, aliyekuwa akiongoza jopo la mawakili watano kutoka vyama vinavyounda Ukawa, alisema watahakikisha wanapambana ili haki ipatikane.
Baada ya wakili huyo kuzungumza hilo, ndipo alikuja askari mmoja na kumuita Profesa Lipumba na kumrudisha tena kituoni kwa ajili ya kupelekwa mahakamani.
Ilipofika saa 7:00 mchana, Profesa Lipumba aliomba kwenda kumuona daktari wake kwa sababu tangu alipokamatwa na kuswekwa rumande juzi usiku, hakupata muda wa kuonana na daktari wake kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya ambapo alikuwa akisikia dalili za shinikizo la damu, maumivu sehemu za kichwani na kifuani.
Polisi walikubali kumpeleka kwa daktari wake wa kliniki ya Umoja wa Mataifa iliyopo Oysterbay chini ya ulinzi, wakitumia gari lenye namba za usajili PT 2566.
Alipewa matibabu na kubainika kwamba shinikizo la damu lilikuwa juu hali iliyomfanya daktari kumtaka apumzike kwa muda wa wiki mbili.
Jambo la kushangaza baada ya kutoka kumuona daktari wake, akiwa chini ya ulinzi wa polisi, Profesa Lipumba alichukuliwa moja kwa moja kwa gari hilo ambalo lilikuwa likienda kwa kasi kwa nia ya kuwakwepa waandishi wa habari na kupelekwa Mahakama ya Kisutu.
Akizungumzia kuhusu tukio hilo, kada wa CUF, Mbarallah Maharagande, alisema ameshangaa kuona namna ambavyo polisi wametumia nguvu zisizo za lazima.
“Natoa wito kwa Rais Jakaya Kikwete azungumze na watendaji wake kuacha tabia ya kuwapiga watu, kwani watakapochoka watajibu mapigo na suala hilo ni baya ukizingatia tunaelekea katika uchaguzi mkuu na upigaji kura wa Katiba inayopendekezwa,” alisema.
Salum Abdul, alisema polisi wametumia ubabe katika tukio ambalo Profesa Lipumba alikuwa ametumia busara ya kulisitisha.
Naye Shukuru Hassan ambaye amejitambulisha kama mjumbe wa serikali ya mtaa wa Buguruni Kisiwani, alisema kuwa tukio hilo ni la kudhalilisha jeshi la polisi.

SOURCE; MTANZANIA

Mtanzania Afanyiwa Unyama Huko Afrika Kusini ; Akatwa uume wake

MFANYABIASHARA aliyefahamika kwa jina la Jumanne Tevez, mkazi wa Dar es Salaam, amefanyiwa unyama baada ya kudaiwa kukatwa uume wake na wenzake.
Habari za uhakika kutoka chanzo chetu cha habari zilisema kuwa Tevez, amelazwa katika hospitali moja nchini Afrika Kusini akipatiwa matibabuChanzo chetu hicho ambacho kipo karibu na familia ya mfanyabiashara huyo, kilieleza kuwa taratibu zinafanywa ili mke wake pamoja na kaka yake waweze kusafiri kwa ajili ya kwenda kumchukua.
“Hizo taarifa ni za kweli kabisa na hivi ninavyokuambia mke wake na kaka yake wanatarajia kuondoka kesho ili wakamchukue. Amelazwa katika hospitali moja huko Afrika Kusini na hali yake si mbaya sana.
“Yule jamaa kama unavyojua alikuwa mtu wa dili wa muda mrefu, hivyo inawezekana alitofautina na wenzake ndio maana wakamfanyia kitu mbaya, si unajua hawa jama wa poda (dawa za kulevya), humalizana wenyewe tu,” kilisema chanzo hicho kilipozungumza na Uhuru, jana.
Habari zilizoandikwa kwenye mitandao ya kijamii, zilimuonyesha mfanyabiashara huyo akiwa amevuliwa nguo zote huku akiwa amefungwa kamba mikononi na miguuni.
Tevez, anadaiwa kufanyiwa unyama huo baada ya kuwadhulumu wafanyabiashara wenzake wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya.
Habari zinadai kuwa, mfanyabiashara huyo alifanyiwa unyama huo, Afrika Kusini baada ya kubainika kuficha dawa hizo.
Mfanyabiashara huyo anadaiwa kuficha mzigo aliopewa kutoka Afrika Kusini kuuleta Tanzania na kwamba baada ya kufika nchini, aliwaeleza wenzake kuwa mzigo huo umepotea.
Maelezo hayo yalionekana kuwaudhi waliompa mzigo huo, ndipo walipomuita Afrika Kusini, ambako baada ya kufika, waliamua kumfanyia unyama huo.
Picha mbalimbali zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, zinamuonyesha Tevez, akiwa na jeraha mgongoni, tumboni na jicho lake la mkono wa kushoto.
Mfanyabiashara huyo alijipatia umaarufu mkubwa jijini Dar es Salaam,baada ya kufunga ndoa na msanii maarufu wa muziki wa taarab, Isha Ramadhani ‘Mashauzi’ ama jike la Simba.
Katika nyimbo mbalimbali alizokuwa akiimba, Isha anasikika akimtaja mwenza wake huyo wa zamani waliyetengana.
Akizungumza kwa sharti la kutoandikwa jina lake gazetini, mmoja wa marafiki wa Tevez, alisema amepata taarifa hizo kupitia mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, alisema baada ya kusoma habari hizo na kuona picha, alimpigia simu rafiki mwingine wa karibu wa mfanyabiashara huyo, ambaye naye alikuwa hajapata taarifa kamili.
“Ninachoweza kukueleza ni kwamba habari hizi nimeziona pamoja na picha kwenye mitandao ya kijamii, nimejaribu kufuatilia kwa rafiki yake mwingine, ambaye yupo karibu naye sana, lakini hakunieleza ipasavyo mkasa huo.
“Hadi sasa kwa kweli tupo njia panda, inawezekana ni kweli, lakini bado hizi taarifa rasmi kutoka kwa familia wanazificha sasa subiri tuone. Cha kusikitisha zaidi baadhi ya watu wanasema amevuta (kufariki dunia), lakini yote hayo hatujathibitishiwa,” alisema.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ilisema haijapata taarifa za kuteswa kwa mfanyabiashara huyo.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa wizara hiyo, Mkumbwa Ally, alisema wizara haina taarifa hiyo na kwamba wataendelea kuzifuatilia kupitia ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini.
Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya cha Jeshi la Polisi, Godfrey Nzoa, hakuweza kupatika kuzungumzia suala hilo kwani simu yake ya mkononi ilikuwa haipo hewani muda wote.

Msafara wa Rais wa Nigeria wapigwa Mawe

Rais Goodluck Jonathan amelaumiwa kwa kukosa kudhibiti kundi la Boko Haram
Msafara wa magari ya Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan umepigwa kwa mawe na watu wanaioishutumu serikali kwa kukosa kukomesha harakati za wapiganaji wa kiisilamu wa Boko Haram.
Madirisha ya magari kadhaa kwenye msafara huo yalivunjwa kwa mawe, kabla ya polisi kuwafyatulia gesi ya kutoa machozi watau hao huku wakiwacharaza kwa mijeledi.
Shambulizi hili limefanyika katika mji wa Yola Mashariki mwa Nigeria, ambako Rais Jonathan alikuwa anaendesha kampeni yake kabla ya uchaguzi mkuu mwezi ujao.
Maelfu ya wakimbizi wa ndani wanaishi mjini Yola baada ya kutoroka vita kutoka makwao ambako Boko Haram inaendesha harakati zake.

26 wauawa Kigaidi huko Misri

Gari la kivita la Serikali nchini Misri

Takriban watu 26 wameuawa katika mfululizo wa mashambulizi yaliyofanywa na kundi la wapiganaji la Islamic State Kaskazini mwa Misri katika eneo Sinai
Gari lililokuwa na mabomu lilipiga kituo cha kijeshi kaskazini mwa Sinai katika mji wa El-Arish na kuwaua wanajeshi kadhaa. Mashambulizi mengine kama hayo yalifanyika katika mji jirani Sheik Zuwayid na mji wa Rafah katika mpaka wa Gaza.
Kundi la wapiganaji la Ansar Beit al-Maqdis ambalo ni mshirika wa wapiganaji wa Islamic State wamekiri kutekeleza shambulio hilo.
Maafisa wa jeshi nchini Misri wanasema gari hilo lililokuwa na mabomu liliegeshwa nje ya ngome ya jeshi ya El-Arish na mashambulizi yake yalilenga hoteli ya jeshi na maeneo mengine mhimu katika kituo hicho.
Hata hivyo kundi hilo lilianza kutekeleza mashambulizi yake nchini Misri tangu kuangushwa kwa utawala wa Rais aliyekuwa na msimamo mkali wa Kiislam Mohammed Morsi mwaka 2013.
Hofu imetawala katika miji kadhaa nchini Misri wiki hii kutokana na sherehe za kumbukumbu za kuangushwa kwa utawala wa aliyekuwa Rais wa Taifa hilo na aliyeondolewa madarakani mwaka 2011 Hosni Mubarak.
Eneo la Kaskazini mwa mji wa Sinai kumekuwa na hofu ya mashambulizi ya kigaidi tangu mwezi Oktobar mwakajana ambapo wanajeshi kladhaa waliuawa katika shambulio.
Jeshi kwa muda mrefu limekuwa likitekeleza opereshen maalumu ili kudhibiti hali hiyo,japo kuwa inaonekana kushindwa kudhibiti hali hiyo.
Wapiganaji wa kundi la Ansar Beit al-Maqdis ni tishio kwa sasa nchini Misri kwani wamekuwa wakiandaa mashambulizi yanayolenga vituo vya kijeshi..
Wachambuzi wa mambo wanasema mashambulizi haya yanabainisha kuwepo kwa mikakati mikali inayopangwa na kundi hilo ambayo huenda vyombo vya usalama havijabaini mbinu zao.
Kundi hili la Ansar Beit al-Maqdis ambalo kuanzishwa kwake ilikuwa ni hamasa ya kundi la kigaidi la Al Qaeda,liliamua kubadili mtazamo wake na kuanza kutekeleza na kutii amri za kundi la wapiganaji wa Islamic state lililoshamiri Iraq na Syria,na malengo ya kundi hili ni kuhamasisha watu kuasi na kuuangusha utawala wa sasa wa Rais Misri Abdul Fattah al-Sisi.
Hata hivyo mtenda naye hutendwa kwani Rais Sisi ndiye kiongozi wa kijeshi aliongoza harakati za kuuangusha utawala wa Morsi kutoka Muslism Brotherhood lakini kwa sasa harakati za kumuangusha na yeye zinaendelea.

Ajiua kisa mwanae Kupiga Picha za Uchi

Loredana Chivu ni mwanamitindo nchini Romania

Loredana Chivu ni mwanamitindo nchini Romania  katika jarida la Playboy nchini Romania.
Loredana Chivu alirarua ukurasa uliokuwa na picha yake akiwa 'amepos' katika jarida hilo la Playboy na punde babake alipogundua kuhusu picha hizo, alizongwa na mawazo na hata kumkana mwanawe.
Kwa mujibu wa mtandao wa Mirror, msichana huyo mwenye umbo la kuvutia alisema, '' babangu aliacha kuongea na mimi na kuonekana mwenye hasira sana''.
"alipogundua kuwa picha hizo zilikua zangu, alijitenga sana na kujaribu kunitenga na mimi''.
Nilidhani labda angesahau na sikudhani hata siku moja angejitoa uhai.

Loredana Chivu anasema anajuta sana kwani babake hakuwahi kuongea naye baada ya kupata picha zake
Mwanamitindo huyo Loredana Chivu mwenye mamia ya picha akiwa nusu uchi kwenye akaunti yake ya Instagram, alikuwa na uhusiano wa karibu sana na babake lakini alisema yote hayo yalibadilika baada ya babake kuona picha zake akiwa nusu uchi.
Alipokwenda kumtembelea babake miezi michache baadaye, baada ya kuamua kwamba kimya kilikuwa kimeendelea kwa muda mrefu sana, alishtuka sana kumpata babake akiwa amejitoa uhai
"nilipata akiwa na kamba shingoni akiwa ananing'inia chumbani''.
Loredana,anayeishi nchini Romania, anasema kuwa tangu kifo cha babake, amekuwa akiwaza na kuwazua kwamba aliamua kujiua kwa sababu ya mgogoro kati yetu na hasa kuhusu picha zangu zilizoziona kwenye jarida la Playboy.
''Najuta sana kwamba hakuwahi kupata muda wa kuzungumza na babangu kuhusu yaliyotokea''.
''Hakuwacha ujumbe wowote kabla ya kujitoa uhai, siku zote tulikuwa na uhusiano mzuri lakini yote yalibadilika baada ya baba kuona picha zangu nikiwa uchi. Bado inaniuma sana na singemtakia mtu yeyote kupatwa na kama yaliyonikuta''

Chelsea yampiga bei Schrulle

Andre Schurrle

Chelsea imekubali kumuuza mshambuliaji wake Andre Schurrle ili kupata ufadhili wa kumsajili Juan Cuadrado.
Hatua hiyo ya kumsajili Cuadrado mwenye umri wa miaka 26 inaweza kukamilishwa katika mda unaohitajika kwa yeye kuichezea Chelsea dhidi ya Mancity siku ya jumamosi.
Gazeti la Mail online limegundua kwamba makubaliano hayo ambapo takriban pauni millioni 60 zitatumika yanakaribia katika kipindi cha saa 24 zijazo.
Chelsea inamuuza Shurrle kwa kitita cha pauni millioni 30 huku kilabu ya Wolfburg ikimhitaji nayo Borussia Dortmund pia nayo ikimtaka.
Kocha Jose Mourinho hampendelei mchezaji huyo wa Ujerumani,lakini anatambua thamani yake katika soko la uhamisho.
Mshambuliaji huyo wa Ujerumani vilevile anataka kurudi nyumbani.

Tuesday, 27 January 2015

Lipumba atembezewa kichapo katika Vurugu huko Temeke

Habari zilizotufikia Punde:Jeshi la polisi limetumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi wa chama cha wananchi CUF waliokuwa wakiandamana kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya wenzao huko Pemba yaliyotokea mwaka 2001, Ambapomwenyekiti wake Profesa Ibrahimu Lipumba nimiongoni watu waliokubwa na kadhia hiyo ya kupigwa mabomu ya machozi eneo la Temeke jijini Dar es Salaam.Kwa habari zaidi Endelea kufuatilia taarifa zetu tutakujuza kwa kina.

Chadema yaungana na wananchi kupinga Viongozi wanaowadharau wananchi

Chama cha demokrasia na maendeleo Chadema mkoani Arusha kimesema kitaendelea kuungana  na wananchi kukemea na kukabiliana na viongozi  wanaowakejeli na kuwakatisha tamaa watanzania wanaotaka kuwekeza kwenye miradi mikubwa ukiwemo wa gesi na mafuta kwani kuendelea kuwafumbia macho ni kuendekeza umaskini.
Akizungumzia mabadiliko hayo katibu wa chama hicho Bw Kalst Lazaro amemtahadharisha Waziri Mh George Simbachawene aliteuliwa kuchukua nafasi ya Prof Muhongo aliyejizulu kuacha kuendelea kuwakatisha watanzania tamaa badala yake awape moyo na kuwasaidia kufikia ndoto zao.
 
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wamesema mtu yeyote anayekatisha wenzake tamaa badala ya kuwapa moyo ni ishara ya kutosha kuwa amepoteza sifa ya kuwa kiongozi na pia uwezo wake wa kuleta mabadiliko ni mdogo kwani hakuna lisilowezekana.

Kasisi wa Kwanza Mwanamke Aapishwa


Mchungaji Libby Lane
Mchungaji Libby Lane
KANISA moja la Kianglikana nchini Uingereza limemuapisha mwanamke wa kwanza kuwa kasisi. Mchungaji Libby Lane ameapishwa katika sherehe iliofanyika eneo la York Minster, na atakuwa Kasisi wa Stockport ikiwa ni miezi sita tu baada ya kanisa hilo kumpigia kura ili kumaliza utamaduni wake wa wanaume kuwa makasisi.
Kasisi huyo alisema kuwa iwapo uchaguzi wake utawafanya wanawake kubaini uwezo wao basi anafurahia. Hatua hiyo imeendelea kuzua hisia tofauti miongoni mwa wafuasi wa kanisa hilo la kianglikana duniani.

Ufisadi Mpya watarajiwa Kuibuliwa tena Bungeni

Zitto kabwe
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kesho itawasha moto upya bungeni wakati itakaposoma ripoti maalumu ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ikitarajiwa kuibua kashfa tatu nzito ikiwamo ya misamaha ya kodi.
Kashfa nyingine zinazotarajiwa kuibuliwa kesho ni, ufisadi katika gharama za ujenzi wa jengo la watu mashuhuri (VIP) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na uuzaji wa nyumba ya Bodi ya Korosho.
Habari zilizolifikia  jana na kuthibitishwa na Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe zilisema kuwa, tayari kamati hiyo imepokea ripoti ya ukaguzi huo ambayo inaonyesha ufisadi wa kutisha katika maeneo hayo matatu na mengineyo.
Masuala hayo matatu pia yaliibuka wakati wa vikao vya kamati za Bunge vilivyomalizika Dar es Salaam wiki iliyopita, huku bodi ya korosho ikibanwa kuhusu nyumba yake aliyouziwa Mbunge wa Kibaha Mjini (CCM), Silvestry Koka.
Kwa mujibu wa habari hizo, ripoti hiyo inayoonyesha jinsi ufisadi wa kutisha ulivyofanywa katika ujenzi wa jengo la (VIP Lounge) na Serikali inadai ilitumia Sh12 bilioni kulijenga, lakini mthamini wa majengo ya Serikali ameeleza kuwa jengo hilo lina thamani ya Sh3 bilioni.
Katika suala la misamaha ya kodi, PAC imepokea taarifa kutoka kwa CAG ikionyesha kuwa misamaha hiyo iliyokuwa imefikia Sh1.5 trilioni mpaka Juni 2013, lakini baada ya mwaka moja misamaha hiyo imeongezeka hadi Sh1.8 trilioni mpaka Juni 2014.
“Kwa mwaka moja tu, misamaha ya kodi imeongezeka kwa zaidi ya Sh300 bilioni. Kiasi hiki ni kama escrow fulani (Fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow, Sh306 bilioni),” chanzo cha habari kilidokeza.
Katika vikao vya kamati hiyo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilieleza kuwa misamaha ya kodi imepanda kutoka Sh1.4 trilioni mwaka 2012/13 hadi Sh1.8 trilioni mwaka 2013/14, chanzo kikiwa ni misamaha ya kodi katika miradi mikubwa. Ilisema kati ya misamaha hiyo, Sh676 bilioni zinatokana na misamaha ya kodi inayotokana na Ongezeko la Thamani (VAT) na kuwa hali hiyo itapungua iwapo nchi itaanza kutumia Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Pia, TRA ilifafanua kuwa mpaka sasa wafanyabiashara na kampuni kubwa zimefungua kesi katika mahakama ya rufaa wakipinga kulipa kodi ambayo inafikia Sh1.7 trilioni.
Mvutano mwingine unaotarajiwa kuibuliwa katika ripoti hiyo ni uwasilishwaji wa utata wa uuzwaji wa nyumba  ya Bodi ya Korosho.
Awali, hati ya nyumba hiyo ilikuwa ya Taasisi ya Kilimo Tanzania ambayo ilifutwa mwaka 1963, kabla ya mtu mwingine kuibadilisha hati na kuiuza kwa Koka mwaka 2011.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mudhihir Mudhihir alisema Koka aliuziwa nyumba na taasisi hiyo ambayo haikuwa mmiliki halali.
Alisema nyumba hiyo iliuzwa kwa Sh300 milioni na katika juhudi za bodi kufuatilia taratibu za kuirudisha, ikagundulika kuwa hati imeshabadilishwa, kusisitiza kuwa uuzwaji wa nyumba hiyo ulifanyika kimakosa bila kufuata sheria na taratibu.
Juzi Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alikaririwa akiwataka wananchi kutoa taarifa kuhusu makusudio ya kuuza nyumba za Serikali na mashirika ya umma, kutokana na madeni mbalimbali ili ziweze kukombolewa kabla ya kuuzwa.

PACHA WA WEMA TUERNEY AANZA KUINGIA DOA MASHABIKI WANAANZA KUMKATA


 tuerney ndio habari ya mujini kipindi hii, mwanadada huyo alianza kupata umaarufu na mashabiki wengi walianza kumkubali jinsi alivyo na namna anavyoolok like wema, but cha kushangaza umbea na udaku umeenza kusambaa kupitia mitandao tofauti ya kijamii, zimekuwa zikionekana message nyingi hususan huko insta zikimdiss mwanadada huyo, ikiwema account ya wemaauntezekiel ambayo mmiliki wa account hiyo ajulikani..

hiyo ni miongoni mwa picha iliyoenea kwenye mitandao tofauti tofauti huku watu wakidiss eti before and after, huku wengine wakisema chanzo cha kuanza kumdiss mwanadada huyo ni mara baada ya kualikwa kwenye shereh ya wema sepetu, halafu eti akakataa na kuanza kujisfia kwa watu kuwa amemkatalia, all in all mtandao wa makubwa haya utafanya jitihada ya kumtafuta mwanadada huyo na kufanya nae interview ili ukweli upate kujulika..

Chelsea na Liverpool kumenyana leo Kombe la FA

Baada ya kushindwa kutambiana katika mchezo wa kwanza wa Kombe la FA uliomalizika kwa Sare ya 1-1 Chelsea na Liverpool watakuwa dimbani Stamford Bridge  kupimana ubavu.
Mchezo huu wa nusu fainali ya pili utaamua nani anaelekea fainali itakayopigwa katika dimba la Wembley Machi Mosi.
Katika mchezo wa kwanza Chelsea walipata goli kwa mkwaju wa penati kupitia kwa Eden Hazard huku Raheem Sterling akiisawaizishia Liverpool.
Mchezo mwingine wa nusu fainali ya pili utapigwa kati ya Sheffield United na Tottenham.
Tottenham walipata ushindi katika mchezo wa kwanza kwa bao 1-0 lilikwamishwa wavuni na Andros Townsend kwa mkwaju wa penati.

Madrid yamsajili Silva

Mchezaji Lucas Silva aliyesajiliwa na Real Madrid

Kilabu ya Real Madrid imemsajili kiungo wa kati Lucas Silva kutoka kilabu ya Cruizero ya Brazil kwa kitita cha pauni millioni 9.7.
Mchezaji huyo wa miaka 21 ambaye alifanyiwa ukaguzi wa matibabu siku ya jumatatu ameweka sahihi ambayo itamuweka katika kilabu hiyo hadi Juni 30 mwaka 2020.
Silva ameiwakilisha Brazil katika soka ya chini ya umri wa miaka 21 na kuisadia kilabu yake kushinda mwaka 2013 na 2014.
Real ilimnunua kiungo wa kati mwenye umri wa miaka 16 Martin Odegaard mapema wiki hii.

Real Madrid yasaini kujenga kituo cha Michezo Tanzania

Mjumbe kutoka Real Madrid Rayco Garcia na Mkurugenzi wa NSSF,Ramadhani Dau wakitia saini Hati ya makubaliano
Klabu tajiri duniani, Real Madrid ya Hispania imesaini Hati ya makubaliano na Shirika la hifadhi ya Jamii Tanzania (NSSF) kwa ajili ya kujenga na kuendesha kituo cha michezo kitakachogharibu Shilingi bilioni 16.
Ujenzi huo utajumuisha Viwanja vitano ya Mpira wa miguu, Mabweni ya Wachezaji na Wageni, Maduka na huduma nyingine muhimu .
Pia patajengwa Uwanja wa Gofu wa Mashimo 18 utakaoambatana na ujenzi wa Nyumba za kisasa katika eneo la Ekari 400 lililopo katika Mji uliopangwa kuwa wa kisasa wa Kigamboni, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Makubaliano yalifanyika jijini Dar es Salaam muda mchache baada ya maofisa wa Real Madrid, akiwemo mkuu wa vituo vya kulelea wachezaji wa Real Madrid, Rayco Garcia,ambaye wakati wa uchezaji wake alicheza na Ronaldo de Lima, Roberto Carlos na Zinedine Zidane. Kwa sasa ni kocha wa kikosi cha timu ya Real Madrid chini ya miaka 19.
“Tumefurahishwa sana na ubia huu wa kimaendeleo utakaodumu kwa miaka 18 katika kutafuta, kukuza na kuendeleza vipaji nchini Tanzania kwa ajili ya kutafuta kucheza soka la kulipwa barani Ulaya na kwingineko duniani”, alisema Garcia.
Kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa NSSF, Ramadhani Dau, hati ya makubaliano ina sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ni kazi ya Shirika hilo kubwa Tanzania kujenga kituo hicho na sehemu ya pili itakuwa ni ya Real Madrid ikihusisha kuleta makocha, kusimamia mchakato wa kupata vijana chini ya miaka 13, 14, 15, an 16 watakaoingia katika kituo hicho na kusimamia chakula bora.
Pia itahusika na kutafuta Masoko kwa Wachezaji hao baada ya kuwatangaza kupitia Televisheni ya Real Madrid.
Pia Dau alisema uwekezaji huo utatoa fursa kwa Tanzania kupata wachezaji kwa ajili ya kushiriki kucheza kombe la dunia katika miaka ijayo ili kutimiza ndoto ya muda mrefu.
Tanzania imekuwa moja ya kivutio kikubwa barani Afrika kwa timu za Ulaya. Hiki kitakuwa ni Chuo cha pili kujengwa baada ya Klabu ya Sunderland ya Uingereza nayo kuendelea na ujenzi wa kituo kingine.
Hivi karibuni, maofisa wa Klabu ya Arsenal ya Uingereza pia walitua Tanzania kwa ajili ya kutafuta ubia wa kuuza Vifaa vyake vya michezo kama vile Jezi baada ya kugunuda kuwa wana wapenzi na mashabiki wengi
Wengine walioambatana na Garcia ni Francisco Martin, , Juan Jose Milla (makocha) na mkurugenzi wa ufundi Ruben de La Red.