WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amesema wimbi la ujangili wa kutisha
lililozuka hivi karibuni la kuua wanyama hususan faru na tembo
linaelekea kutishia uhai wa wanyamapori na kupoteza ubora wa hifadhi
nchini.
Pinda alitoa kauli hiyo juzi baada ya kuhitimisha mbio za Serengeti
zilizokuwa maalumu kwa ajili ya kupinga ujangili katika hifadhi
mbalimbali za taifa.
Akisoma hotuba ya Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Paschal
Mabiti, alisema hivi karibuni kumezuka wimbi la ujangili kwa kiwango cha
kusikitisha likihusisha wananchi wageni.
Alisema utalii ndiyo sekta inayoongoza kwa kulipatia taifa fedha za
kigeni ambazo ndizo zinatumika kujenga barabara, hospitali, vyuo,
viwanja vya ndege na uendeshaji wa shughuli mbalimbali za serikali,
hivyo alimtaka kila mmoja kusimamia na hata kushirikiana katika utoaji
wa taarifa wa mauaji hayo.
“Ufanisi wa utalii unategemea sana uwepo wa wanyamapori, hasa kundi
la wanyama wanaoitwa ‘big five’ linalohusisha tembo, faru, simba, nyati
na chui, hivyo si vema wakaendelea kuachwa wakiteketea,” alisema Mabiti.
Alisema Mkoa wa Simiyu una kilomita za mraba 23,807.7 kati ya hizo
11,723.6 ni eneo la hifadhi ya mbuga za taifa ya Serengeti na mapori ya
akiba ya Maswa, hivyo alisisitiza dhana ya kuhamasisha uhifadhi wa
wanyamapori kwa kutumia shughuli mbalimbali za matamasha kama
ilivyotumika mbio za Serengeti.
Mkurugenzi wa Kituo cha Michezo cha Serengeti, Dk. Titus Kamani,
alisema ni wajibu kwa kila mwana Simiyu kutunza mazingira, kulinda
wanyama, kupinga mauaji ya albino, ili waweze kuendelea kiuchumi wakiwa
na amani.
Alisema suala la ujangili ni kubwa, hivyo si la kuachia serikali pekee ikafanya kazi hiyo.
No comments:
Post a Comment