Sunday 8 December 2013

WATANZANIA WAISHIO UGAIBUNI WAZUA MJADALA BUNGENI

SUALA la kuruhusiwa kwa Watanzania waishio nje ya nchi kupiga kura ya maoni ya kupitisha Katiba mpya, limezua mjadala bungeni, ambapo wabunge wengi wameonesha wasiwasi na kutaka utaratibu huo usitishwe, kwa kuwa unaweza kuzalisha mamluki na kuweka nchi hatarini.
Pia, Spika Anne Makinda na baadhi ya wabunge wazoefu akiwemo Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Muhammed (CUF), wamewaasa wabunge kuhakikisha kuwa wanaweka itikadi zao pembeni ndani ya Bunge hilo na kuungana kwa pamoja katika mchakato mzima wa upatikanaji wa Katiba mpya.
 
Aidha, bungeni hapo kuligeuka uwanja wa kusutana baada ya wabunge watokao Zanzibar kurushiana vijembe hasa baada ya kuibuka kwa mjadala wa kupinga kutumika kwa Sheria ya Uchaguzi Zanzibar na Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika uchaguzi wa kura ya maoni.
Akichangia mjadala huo bungeni hapo, Mbunge wa Same Magharibi, Anne Kilango alitahadharisha juu ya uwezo wa Serikali kuweza kuwafikia Watanzania wote wanaoishi nje ya nchi na iwapo takwimu na idadi yao halisi ipo.
“Ikumbukwe kuwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi ni wengi na wanaoishi duniani kote si hapo London pekee, humu kwenye Sheria tumesema tutaunda kamati za kura za maoni, wasimamizi je huko nako tutaweza kuunda kamati hizi duniani kote? Uwezo huo tunao kweli? Alihoji.
Kwa upande wake, Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohammed (CUF) alitahadharisha juu ya kipengele hicho kinachotoa fursa kwa Watanzania waishio nje ya nchi kupiga kuwa huenda fursa hiyo inaweza kutumiwa vibaya.
Aidha, aliwataka wabunge kutumia busara na kuweka itikadi zao pembeni wanapojadili masuala yanayohusu mchakato wa Katiba ili kutokutoa fursa kwa watu wenye nia mbaya kuliangamiza taifa.
Alisema kumekuwepo na watu ambao hawaitakii mema Tanzania na kwamba huangalia fursa yoyote ya kutokuelewana na kujipenyeza kwa ajili ya kuliangamiza taifa kwa maslahi yao.
“Haiwezekani kwa mazingira yoyote kutunga Sheria ikawa kamilifu anayeliweza hilo ni Mungu pekee, ila kama kuna makosa ni vyema kuweka uzalendo mbele bila kuingiza siasa na kuyabainisha ili yaweze kufanyiwa kazi,” alisisitiza.
Alisema haipendezi kutengeneza matabaka na makundi ndani ya chombo hicho kwa mambo ambayo yanaweza kurekebishwa na matokeo yake kuonekana kwa Watanzania wote.
“Kwa sasa kuna familia za Wazanzibari takribani 118,000 waliopo Tanzania bara na kila familia ina watoto zaidi ya wanane, Zanzibar pia kuna familia za Watanzania Bara 15,000 wanaishi huko na watoto watano kila familia, sasa kwa haya tunayoyafanya hapa jamii itaenda wapi? Alihoji.
Aliwaomba wabunge hao kuhakikisha mchakato huo hauwagawi Watanzania na kuangamiza taifa kama ilivyokuwa kwa mataifa ya Libya na Iraq ambayo kwa sasa baada ya kusambaratika maliasili zake ikiwemo mafuta zinatafunwa na wajanja. Spika Makinda naye alionesha kushangazwa na hali ya sasa ya Bunge hilo, ambapo kumekuwa na mabishano na majibizano huku hoja muhimu zinazohitaji kuboreshwa zikiachwa.
“Kuna wasomi humu ndani jamani wakiwemo wanasheria, tumieni taaluma zenu kurekebisha, tatizo la Bunge hili kila kitu kinafanyika kivyama. Kosoeni na kusema tufanye nini, sasa nyie mkilalamika mlipo humu ndani waliopo nje nao wafanye nini? Alihoji.
Mbunge wa Viti Maalum, Tauhida Gallas (CCM), alionesha kushangazwa na kauli za wabunge wengine za kupinga kutumika kwa daftari hilo la kudumu katika uchaguzi huo wakati daftari na sheria hizo ndio zilizotumika katika kupiga kura ya maoni ya kupitisha mfumo wa Serikali ya Umoja (SUK) visiwani humo.
“Masuala ya Wazanzibari tuachieni wenyewe sie tunajuana, ni Waarabu wa Pemba, hili daftari na sheria inayokataliwa vilitumika kupigia kura ya maoni ya SUK, sasa leo kwenye Katiba iweje ikataliwe, wenzetu hebu tuambieni kuna nini hapa? Alihoji.
Alisema hata suala la kulaumiwa kwa masheha halina mashiko, kwa kuwa masheha hao wamekuwa wakifanyakazi bila kuzingatia uchama hali iliyosababisha kulalamikiwa vyama vyote.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini na Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene, alisisitiza juu ya umuhimu wa suala hilo la Katiba kujadiliwa bila kuingiza vyama kwa kuwa kwa hali inayoendelea bungeni humo imeonesha kutokuwepo kwa dhamira ya kupatikana kwa Katiba ya Watanzania.
Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mohammed Mnyaa, alipinga vikali suala la kuachwa kwa Sheria hiyo ya Zanzibar katika mchakato wa Katiba kwa kuwa imekuwa ikipindisha haki ya watu wegi kushiriki kwenye uchaguzi akiwemo Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein.
Sheria hii sijui kwanini bado inafumbiwa macho, kwani kupitia Sheria hii Rais Shein ndio Rais wa kwanza duniani kutojipigia kura kwa kuwa tu haimtambui,” alisema Mnyaa.

No comments: