Monday, 9 December 2013

MIAKA 52 YA UHURU:JK tumuenzi Mandela kwa kusamehe na kutolipiza visasi


 Rais Jakaya Kikwete akiwasalimia maelfu ya watu waliojitokeza kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam kwenye sherehe za kuazimisha miaka 52 ya Uhuru wa Tanzania bara.Picha na A.H.M


Dar es Salaam. Rais Jakaya Mrisho Kikwete amewataka watanzania kuacha tabia ya kuwa na roho ya kulipiza visasi badala yake wawe watu wa kusamehe na kusahau kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanamuenzi moja kwa moja Rais mstaafu wa Afrika Kusini Marehemu Nelson Mandela.
  • Rais Kikwete ameyasema hayo mapema leo alipokuwa akiwa hutubia maelfu ya watu waliojitokeza kwenye sherehe za kutimiza miaka 52 ya Uhuru wa Tanzania bara, sherehe zilizofanyika katika uwanja Taifa jijini Dar es Salaam jambo ambalo si kawaida yake kutoa hotuba
Rais Kikwete amesema mara baada ya Rais Mandela kutolewa gerezani  hofu ilitawala Afrika ya Kusini, watu wengi wakitambua kuwa atakapochaguliwa kuwa Rais badala ya kuijenga nchi ataanza kulipiza visasi kwa wale wote waliotumika kwa namna moja ama nyingine kumtesa yeye na watu wa nchi yake.
“Badala yake Mzee Mandela alitoa tamko la kuwasamehe wote waliohusika kuwabagua watu wa Afrika ya Kusini, na kisha aliunda tume maalumu ya maridhiano ili kujenga umoja kati ya watu wenye ngozi nyeupe na wenye ngozi nyeusi, jambo hili ni la ajabu sana” amesema Kikwete.
“Hiki ni kipimo kikubwa cha ukomavu wa kisiasa, yatupasa watanzania na viongozi mbalimbali kuenzi jambo hili la kusameheana na kutokuwa walipiza visasi, hapa tulipo wengine wanasema kabisa nikichaguliwa watanikoma….. lakini nawasihi tumuenzi Mzee Mandela kwa kuiga mambo mema aliyoyafanya ambayo hadi hivi leo yamechangia kukuza uchumi wa Afrika ya Kusini, “amesema Kikwete.
Amesema tokea enzi za TANU Tanzania imekuwa karibu sana na vyama vya ukombozi wa mataifa mengi Afrika, kikiwemo chama cha ANC ambacho kilikuwa kikiongozwa na Marehemu Mzee Mandela, hivyo aliwasihi watanzania waendeleze umoja huo .
“Kuna jambo moja ambalo hamlijui mwaka wa 1964 Mzee Mandela alikuja nchini na kufikia kwa mweka hazina wa TANU, Siro Swai, alikuwa akielekea kwenye mafunzo ya kijeshi Algeria, aliacha viatu vyake 'pea moja' akieleza kuwa atakaporudi atakuja kuvichukua lakini haikuwa hivyo, nilipokuwa waziri wa mambo ya nje, mke wa Swai alinifuata na kunieleza, nasi tulilazimika kuzirudisha kipindi hicho ambacho Mzee Mandela alikuwa Rais wa nchi hiyo tayari,” Anaeleza Kikwete.
Amesema haya yote yanatafsiri ukaribu na undugu wa hali ya juu kati ya nchi zetu mbili na ndiyo maana katika kumuenzi leo hii kwenye shughuli za kutimiza miaka 52 ya uhuru hatutakuwa na vikundi vya kutumbuiza.

1 comment:

Unknown said...

purian Baba mandela Mwenyezi Mungu akulaze pema peponi