Kamati ndogo ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira inayosikiliza na kuchunguza athari zilizotokana na Operesheni tokomeza Ujangili katika maeneo mbalimbali ya nchi, imejikuta katika wakati mgumu baada ya Chama cha Wafugaji Kanda ya Ziwa kukataa kukutana nayo katika kikao kilichowashirikisha Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo, Richard Mbeho, na Katibu Tawala wa wilaya, Venant Belege, kwa madai kuwa hawana imani na viongozi hao.
Kamati hiyo ipo wilayani Biharamulo, mkoani Kagera kusikiliza na kuchunguza athari zilizotokana na operesheni hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake ambaye pia ni Mbunge wa Kahama, James Lembeli, na jana ililazimika kuzungumza na kusikiliza hoja za wafugaji bila viongozi hao kuwapo.
Mbali na kuwakataa viongozi hao, walisema uongozi mzima wa wilaya hiyo kwa kushirikiana na askari wa hifadhi ya wanyamapoli na Jeshi la Polisi, ndiyo walikuwa mstari wa mbele kuwahujumu wafugaji wakati wa operesheni hiyo.
Mwenyekiti wa chama hicho, Juvenary Mlashani, alisema licha ya Rais Jakaya Kikwete, kusitisha operesheni hiyo kutokana na baadhi ya viongozi kukiuka taratibu na madhumuni yake, jambo la kushangaza zoezi hilo kwa wilaya ya Biharamulo linaendelea.
Alisema viongozi hao wamekuwa wakipuuza kwa makusudi maagizo ya Rais Kikwete kutokana na kutafuta maslahi binafsi. Projestus Rutimwa, alisema kuwa suala la ufugaji wa ng’ombe ndani ya Hifadhi ya Biharamulo hautakwisha iwapo viongozi waliopewa dhamana na serikali wataendelea kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa wafugaji.
No comments:
Post a Comment