Saturday, 7 December 2013

Wanawake waliomuunga mkono Morsi waachiliwa




Yalikuwa maandamano yao ya kwanza kumuunga mkono Mohammed Morsi
Mahakama ya rufaa nchini Misri imeamuru kuachiliwa huru kwa wanawake, 21 wakiwemo wasichana saba waliofungwa jela mwezi jana kwa kuandaa maandamano ya kumuunga mkono aliyekuwa Rais Mohammed Morsi.
Watoto hao wamepewa kifungo cha nje cha miezi mitatu. Mahakama hiyo pia ilipunguza kifungo cha miaka 11 walichokuwa wamepewa wanawake hao 14.
Mahakama iliwapata na hatia mwezi jana ya kuwa sehemu ya kundi la kigaidi lililokuwa linatatiza usafiri wa magari, kufanya hujuma na kutumia nguvu kufanya vitendo vyao.
Hata hivyo makundi ya kutetea haki za binadamu yamekosoa hukumu hiyo.
Mmoja wa wanaharakati hao walitaja hukumu hiyo kama ya wazimu.
Wanawake hao walifikishwa mahakamani wakiwa wamevalia nguo nyeupe huku wakiwa wamebeba maua ya waridi.
Aidha wanawake hao na watoto walishiriki maandamano ya kumuunga mkono aliyekuwa rais Morsi na jamaa zao wanasema ni maandamano ya kwanza waliyowahi kushiriki na kuyaendesha bila vurugu.
Mamia ya watu wameuawa nchini Misri tangu hatua ya kumwondoa Morsi mamlakani mwezi Julai kusababisha maandamano na vurugu

No comments: