Thursday 19 December 2013

WABUNGE WAUMBUANA HADHARANI


Dodoma. Wabunge jana waliumbuana kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma huku Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe akituhumiwa kuagiza kubadilishwa kwa tiketi ya ndege ya Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Joyce Mukya ili afupishe ziara yake ya kikazi huko Marekani na kwenda Uarabuni kwa shughuli binafsi.(EL).

Mbali ya Mbowe, Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi (CCM) anadaiwa kuchukua posho ya Kamati ya Hesabu za Bunge (PAC), kwa safari ya kwenda Dubai na wenzake lakini badala yake akaenda Mbeya kwenye ziara za chama chake.

Malumbano hayo yaliibuka jana baada ya Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM), kuomba mwongozo wa Spika akitaka kufahamu kauli ya ofisi yake kwa Mbowe kutumia nafasi yake kumrudisha mbunge ambaye ameshatumia fedha za Serikali.

Alidai kwamba Mbowe aliagiza Mukya aanze safari Desemba Mosi, mwaka huu kutoka New York, Marekani ili aende Dubai, Falme za Kiarabu (UAE) kabla ya kwenda Dar es Salaam, Desemba 3, mwaka huu.

Alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo jana, Mbowe alisema hawezi kuzungumza chochote kwa kuwa hakuwapo bungeni akisema alikuwa Dar es Salaam kwenye kikao.... "Siwezi kusema lolote mpaka nipate hansard (kumbukumbu rasmi ya Bunge) na kutoka kwa wabunge wangu walioko Dodoma kujua nini kimesemwa."

Akiomba mwongozo Nchemba ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM alisema: "Jambo hili limechukua taswira kama ni Bunge lote linafanya mambo haya na limevunja heshima ya Bunge. Jambo hili linatuvunjia heshima hata watu ambao tuna maadili ya uongozi na tunaliheshimu taifa letu...

"Pamoja na kuwa jambo hilo lilikuwa la binafsi, lakini kuna ujumbe tumeupata kuwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani amemzuia mbunge wake kusafiri na magazeti yakaandika kwamba wana mahusiano. Mimi sipendi kwenda kwenye uhusiano, nataka kwenye taswira ya Bunge na Taifa."

Alisema Bunge linapopanga safari za wabunge linazingatia wa chama tawala na wapinzani ili kuweka uwakilishi.

Nchemba alisema Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema, aliandika ujumbe mfupi wa simu kwa mtumishi mmoja wa Bunge akitaka kubadilishwa kwa tiketi ya ndege ya mbunge.

Aliusoma ujumbe huo: "Rejea mazungumzo yetu bwana Kabunju kuhusu mheshimiwa Joyce Mukya ambaye yupo safarini. Nitashukuru kama utambadilishia booking (safari) yake ili aweze kurudi, aondoke New York tarehe moja Desemba na kurejea Dubai baadaye ataunganisha kurejea Dar es Salaam by Mbowe kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni nakala kwa Joyce Mukya." Kabunju S. Kabunju ni Ofisa wa Bunge anayeshughulikia masuala ya usafiri.

Nchemba alisema: "Ameshakatiwa tiketi, ameziba nafasi ya kwenda kuliwakilisha taifa kule, anamwita arudi Dubai na ni mbunge viti maalumu. Je, hili lina taswira gani kwa taifa na kiti chako kinatoa kauli gani kwa watu ambao wanakwenda kutumia fedha za Serikali kwa mambo binafsi, Dubai?" alisema.

Pia alitaka kufahamu Bunge linachukua hatua gani stahiki kwa mbunge anapoingilia kazi za kiti na pia watumishi wanapoingiliwa na kubadilisha yale waliyotumwa kwa ajili ya Serikali.

Tuhuma za Zambi

Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde alisema Nchemba anaegemea zaidi wabunge wa upinzani wakati wapo wa CCM waliochukua posho.

"Mheshimiwa Mwenyekiti, yaliyosemwa na magazeti na mwombaji wa mwisho (Nchemba), alipokuwa anatoa mwongozo amejaribu kuainisha wabunge wa upande mmoja wa upinzani," alisema.

Alimtaja Zambi kuwa alichukua fedha ili kwenda Dubai na wenzake lakini badala yake alikwenda Mbeya wakati Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alipokuwa katika ziara mkoani humo. Zambi pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya.

"Tunaomba mwongozo wako namna gani hili suala litachukuliwa hatua na wala siyo kufanya propaganda za kisiasa ndani ya Bunge lako," alisema Silinde.

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Mariam Msabaha alisema kuna mambo mengi yanayofanyika ndani ya Bunge hilo lakini hayasemwi.

"Kuna watu wameandikwa ndani ya magazeti wanaiba vidani licha ya kutosemwa lakini imeonekanika huku. Mambo ya mapenzi ni ya mtu na mtu wake, humu kila mtu ana mpenzi wake," alisema.

Mwenyekiti wa PAC na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe alisema: "Kamati ya PAC ambayo inahusika na masuala ya fedha za umma tayari imeshamwomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), afanye uchunguzi kuhusiana na safari zote ili jambo hili liweze kufika mwisho."

Alisema taarifa hiyo itapelekwa kwa Spika na kama atapendezwa italetwa bungeni ili jambo hilo liweze kumalizika.

Akijibu mwongozo huo, Mwenyekiti wa Bunge aliyekuwa akiongoza shughuli za jana asubuhi, Mussa Azzan Zungu alisema: "Nimepokea miongozo yote na kiti kinasema hakina lazima ya kujibu sasa hivi, kitatoa mwongozo baada ya kufikiria na kuyatafakari hapo kitakapopata nafasi."

Hata hivyo, kabla ya kuahirisha Bunge jana mchana, Zungu alisema suala hilo ni la kiutawala na masuala yote yanayohusu masuala ya fedha yanatawaliwa na sheria na kanuni za fedha.

Sakata hilo liliibuliwa bungeni wiki iliyopita na Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy alipokuwa akichangia taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac)

KWA HABARI MOTOMOTO WAWEZA KUTUTEMBELEA kwa kubofya hapa

No comments: