Mkazi wa kijiji cha Karoto geita, Isaya Ngarama, amekataa
kumzika mtoto wake, Samwel Isaya (27), ambaye aliuawa na wanakijiji kwa
tuhuma za ujambazi na mwili wake kuteketezwa kwa moto.
Samwel, aliuawa akiwa na mwenzake na miili yao kuchomwa moto juzi baada
ya wanakijiji kuwahusisha na matukio mbalimbali ya uhalifu.
Tukio hilo lilitokea juzi jioni baada ya Jeshi la Polisi mkoani Geita,
kutoa idhini ya kuzikwa kwa miili ya watu hao waliouwa kikatili kwa
kipigo kikali kutoka kwa wananchi.
Baada ya mzazi huyo kukataa kumzika mtoto wake, wanakijiji waliamua
kuuzika wa mtuhumiwa mwingine ambaye hakufahamika jina na mahali
alikotoka huku wakiuacha mwili wa Samwel uliotambuliwa, uandaliwe
taratibu za mazishi na wanafamilia.
Hata hivyo, katika hali isiyotarajiwa, baba wa marehemu huyo alikataa
kata kata kuuzika mwili huo kwa madai kuwa alichukizwa na tabia ya
mwanawe ya uhalifu.
Hatua hiyo iliufanya uongozi wa serikali ya kijiji hicho ukiongozwa na
Mwenyekiti, Joel Mazemule na Ofisa Mtendaji wake, Peter Chota,
kuukubali mwili huo uzikwe kiserikali.
Baba wa marehemu huyo alifafanua kuwa mtoto wake wakati wa uhai, alikuwa
akijihusisha na udokozi na alimkemea mara kadhaa lakini hakubadilika.
Hata hivyo, uongozi wa kijiji hicho kwa kuwashirikisha baadhi ya wazee
wa kijijini hapo, walimshauri Isaya na akakubali kushiriki mazishi ya
mtoto wake kama wanakijiji wengine.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Prudenciana Protas, juzi
alithibitisha kuuawa kwa watu hao wawili wakituhumiwa majambazi na
miili yao kuchomwa moto.
No comments:
Post a Comment