Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa CCM imewekeza vya kutosha
katika hujuma dhidi ya CHADEMA ikitumia baadhi ya wanachama wa zamani wa
chama hicho kuunda mgogoro na kukipasua.
Kwa sasa viongozi kadhaa wa CHADEMA wamesambaa katika majimbo 103 nchi nzima kujenga chama kwa kufuata maagizo ya Baraza Kuu lililoketi mwishoni mwa mwaka jana, kama mwendelezo wa vuguvugu la mabadiliko, na ujenzi wa chama kuelekea uchaguzi unaokuja.
Baadhi ya wanachama walioondolewa kwa tuhuma mbalimbali wamekuwa wanashirikiana na wana CCM waziwazi kusambaza maneno machafu dhidi ya CHADEMA mtandaoni na mitaani. Baadhi yao wameshiriki kutengeneza mabango na kuyapeperusha katika mikutano inayohutubiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, katika mikoa ya Shinyanga na Kigoma.
Wanapinga uamuzi wa Kamati Kuu kuwavua nyadhifa Zitto, Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba. Zitto amevuliwa wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu, Dk. Kitila amevuliwa wadhifa wa Mjumbe wa Kamati Kuu, na Mwigamba amevuliwa wadhifa wa Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha kwa tuhuma za ‘usaliti’.
Katika kumtetea Zitto na wenzake, baadhi ya wanachama wamekuwa wakitoa matamko, huku wawili wakitangaza kujiuzulu nafasi zao katika mikoa ya Lindi na Singida.
No comments:
Post a Comment