Straike wa zamani wa Manchester United,Andy Cole
STRAIKA wa zamani wa Manchester United,Andy Cole amesema Tanzania ina vipaji vingi vya soka lakini kinachowakwamisha kucheza soka la kulipwa Ulaya ni miundombinu ya kuwatoa katika hatua moja kwenda nyingine.
Cole aliiambia Mwanaspoti kuwa,Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizojaliwa kuwa na vijana wenye vipaji vya hali ya juu lakini wanakumbana na changamoto ya mahala wanapoweza kuonyesha vipaji vyao.
Alisema vijana wengi hapa nchini wana uwezo mzuri wa soka ambao unawawezesha kucheza popote duniani isipokuwa hawapati nafasi ya kuonyesha vipaji walivyonavyo na hata wakipata muda unakuwa umekwisha.
“Ninavyojua Tanzania ina vijana wengi wenye vipaji vya kucheza soka la kulipwa popote duniani ikiwemo Ulaya, nadhani tatizo ni mahali ambapo wanaweza kuonyesha vipaji vyao ili wengine wawachukue,” alisema Cole ambaye alitwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa Man United mwaka 1999.
Alisema vijana wanatakiwa kujiingiza katika soka la kulipwa wakiwa na umri mdogo kwani hapo wanaweza kupata muda wa kujifunza zaidi kuhusu soka la kisasa.
“Naona mwanga kwamba ipo siku Tanzania itatoa wachezaji wa kulipwa watakaocheza soka la kulipwa England au Ulaya,” alisema Cole ambaye aliwahi pia kuichezea timu za Arsenal, Newcastle na Manchester City.
Cole alikuwepo nchini katika kampeni maalum ya Mimi ni bingwa yenye lengo la kuhamasisha soka Tanzania.
Hii ni mara ya pili kwa Cole kutua nchini baada ya kufanya hivyo mwaka jana alipokuja katika michuano ya kuibua vipaji vya vijana ya Airtel Rising Star.
Wachezaji kadhaa wa Tanzania wakiwemo Henry Joseph wa Simba,Nizar Khalfan na Mrisho Ngassa wa Yanga wamewahi kupata nafasi ya kucheza nje ya nchi lakini hawakuweza kucheza katika ligi kubwa kama ya England hata daraja la tatu.
Nizar amewahi kucheza soka la kulipwa nchini Canada katika klabu ya Vancouver Whitecaps kabla ya mwaka jana kurejea nchini, wakati Joseph amewahi kucheza Kongvinger ya Norway na mwaka huu akarudi nyumbani.
Ngassa alipata nafasi ya kufanya majaribio katika klabu ya West Ham lakini hakufuzu.
No comments:
Post a Comment