Saturday, 7 December 2013

Kiburi kilivyoigharimu Zanzibar heroz

Ingawa wengine wanadai kwa kiburi cha Bausi ni sawa kwa maendeleo ya soka na kurudisha nidhamu kwenye soka haswa kwa nchi changa kama Zanzibar.

Zanzibar ina pointi tatu sawa na Burundi huku Rwanda ambayo haina pointi yoyote ikicheza na Eritrea leo jioni Nairobi, Katika timu zilizofanya uamuzi mgumu na kuingia kwenye Chalenji kwa kiburi ni Zanzibar. Timu hiyo ambayo si mwanachama wa Fifa iko chini ya kocha mzalendo, Salum Bausi.
Bausi alipukutisha wachezaji mahiri wa timu hiyo wanaocheza Bara ambao ni Nasoro Masoud (Simba), Abdulhalim Humoud (Simba), Agrey Morris (Azam) na Nadir Haroub Cannavaro (Yanga).
Uamuzi wa Kocha huyo ambao haukuungwa mkono na mashabiki wengi wa Zanzibar pamoja na wachambuzi wa soka walioko mjini hapa, umeonekana kuigharimu timu hiyo ambayo sasa inasubiri mbeleko ya Cecafa ili kufuzu robo fainali.
Zanzibar ina pointi tatu sawa na Burundi huku Rwanda ambayo haina pointi yoyote ikicheza na Eritrea leo jioni katika mechi ambayo timu yoyote inaweza kutengeneza pointi tatu na magoli mengi na kuzidi kuiweka Zanzibar pabaya.
Wazanzibari watasubiri mpaka mechi ya Rwanda imalizike ili kujua hatma yao.
Timu hiyo inawania nafasi moja ya mbeleko kati ya mbili zinazotolewa na Cecafa kwa timu zenye matokeo mazuri.
Uzoefu wa Cannavaro, Humoud, Agrey na Haroub umeonekana kuiponza Zanzibar ambayo kwenye mechi zake tatu imekuwa ikiyumbakwenye safu ya kiungo na beki wa kati ambapo timu imekuwa ikishindwa kucheza soka ya kasi pamoja na kujiamini.
Katika mechi dhidi ya Kenya ambayo Zanzibar ilihitaji japo sare kufuzu robo fainali ilishindwa kuhimili mikiki ambapo ilikamatwa kwenye kiungo huku mabeki wakisababisha penalti ambayo ilitokana na kukosa uzoefu, kujiamini na kubabaika.
Wachambuzi wa soka wanadai kwamba Bausi alitakiwa kuja na kukaa chini na kuwarekebisha wachezaji hao na kuwaleta kwenye michuano hiyo kwa vile ndiyo mikubwa pekee ambayo timu yake inashiriki, hivyo ilikuwa ni bora kuishinda kwa heshima ya Zanzibar.
Ingawa wengine wanadai kwa kiburi cha Bausi ni sawa kwa maendeleo ya soka na kurudisha nidhamu kwenye soka haswa kwa nchi changa kama Zanzibar.
Kocha huyo aliiambia Mwananchi kwamba:
“Sitaki kukaa na wachezaji ambao wana matatizo, niliwaondoa hao kutokana na sababu za utovu wa nidhamu na kushuka viwango.”
“Siwezi kukaa na wachezaji ambao hawaheshimu taratibu, Zanzibar ina wachezaji wengi sana. Ndio maana nimewaacha hao wa Bara ambao hawaheshimu taratibu, tunataka kutengeneza kikosi kipya.
“Kikosi nilichonacho hakina uzoefu, kina wachezaji wengi wadogo wanaocheza ligi ya ndani ndio maana hata kushinda mechi ni kitu kikubwa sana kwa Zanzibar.
“Aina ya timu tunazocheza nazo ni imara na zote zina wachezaji wazoefu, zina mazoezi na ni wanachama wa Fifa wanaopata mechi nyingi za maana tofauti na sisi,” alisisitiza Bausi.
Kocha huyo pia alilalamikia kitendo cha Cecafa kupanga mechi za mwisho kwa siku tofauti kwa madai kwamba inatoa nafasi kwa wengine kupanga matokeo.
“Sisi tumeonewa kwanini tucheze wa kwanza halafu wenzetu Rwanda wapewe siku mbili nzima za kujipanga huu ni utaratibu gani?
Unatoa nafasi ya kupanga matokeo kabisa.
“Ilitakiwa sisi na Rwanda tucheze siku moja kwenye viwanja tofauti kwa vile Kenya haina shida ya viwanja, lakini huu utaratibu si sahihi,” anasisitiza Bausi ingawa katika mechi yake na Ethiopia hakukuwa hata na kosakosa za maana langoni.
Zanzibar ilikuwa kundi A pamoja na wenyeji Kenya, Ethiopia na Sudani Kusini.
Katika mechi ya kwanza Zanzibar iliifunga Sudani Kusini mabao 2-1, ikachapwa na Ethiopia mabao 3-1 kabla ya kupoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji Kenya.
Wachezaji wanaocheza Bara walioko kwenye kikosi hicho ni Adeyun Salehe (Simba), Hamis Mcha(Azam), Awadh Juma (Simba) na Seleman Kasim (Coastal Union).
Wengine waliopo kwenye kikosi hicho ni kutoka kwenye ligi ya Zanzibar ambayo kwa mujibu wa Bausi haina ushindani wa kutosha na timu imara jambo ambalo linamfanya atumie muda mwingi kusuka timu ya Taifa kimazoezi.

No comments: