Saturday, 7 December 2013

KUNA TATIZO TIMU YA VIJANA YANGA……

WACHEZAJI William Lucian ‘Gallas’, Jonas Mkude, Said Ndemla na chipukizi wengine wanaotamba katika kikosi cha Simba kwa sasa, wametokana na malezi mazuri waliyopata wakiwa katika kikosi cha vijana cha klabu hiyo.

Kikosi hicho kilichokuwa kinaundwa na wachezaji wenye umri chini ya miaka 20, kilikuwa kikipata matunzo mazuri chini ya kocha Seleman Matola na viongozi wengine waliokuwa wakiitolea macho timu hiyo.

Vijana hao walikuwa wawajibikaji wazuri ndani ya timu na taratibu mmoja mmoja wakaanza kupandishwa kikosi cha kwanza na leo hii asilimia 50 ya wachezaji wa Simba wanatokana na kikosi hicho.



Tofauti na Simba, Yanga kwa upande wake haikuwa na kikosi bora kwani uongozi haukuwa karibu na timu na hata katika huduma haukuwa ukiihudumia timu ipasavyo hadi kocha Aboubakar Salum ‘Sure Boy’ akaamua kuachia ngazi.

Yanga haikuona umuhimu wa timu na badala yake ilikuwa na timu kimagumashi na ndiyo maana haikuweza kufanya vizuri katika michuano ya Kombe la Uhai mwaka jana.

Baada ya michuano ya mwaka jana, na Simba kuonekana imefanya vizuri kidogo Yanga wakashtuka na kuanza kuitazama timu kwa macho mawili lakini nguvu hiyo ya viongozi iliishia katika kuwakusanya vijana wa kuichezea timu hiyo. Unaweza kuita usajili.



Ushiriki wa mwaka huu:

Katika Kombe la Uhai mwaka huu, Yanga ilishiriki na kufanikiwa kufika fainali lakini ukweli ni kwamba pongezi za kipekee zinatakiwa zifike kwa wachezaji na makocha wao Salvatory Edward na Anthony Chibasa, Salva ni kiungo mahili wa timu hiyo wa zamani.

Viongozi wa timu walikuwa mbali na vijana wao ambao pengine wangetiwa moyo tangu zamani kama wangeuona ujio wa viongozi katika mechi zao za awali. Ishu hapa si kufika mazoezini tu na katika mechi, lakini tutazame vijana hawa wanahamasishwa vipi kuweza kupata ushindi.

Kama nguvu ya viongozi wa Yanga ingetumika tangu mechi za kwanza, bila shaka Yanga ingekuwa bingwa na sasa tungekuwa tunazungumza mengine.



Ni nani aliyekuwa akiwatembelea vijana hawa katika kambi yao pale Jangwani? Ni ahadi ipi waliyopata kama wangechukua ubingwa? Kiongozi mmoja kulundikiwa vitu vingi vya kufanya kwa vijana hawa, inasababisha wachezaji kumzoea mtu mmoja tu na kujiona si sehemu ya Yanga.

Ikumbukwe ya kwamba, kikosi hichi ndiyo kioo cha timu ijayo ya Yanga ambayo sasa inaelekea ukingoni. Hivi mkataba ya kina Mbuyu Twite, Haruna Niyonzima, Hamisi Kiiza na wengine ikiisha huku fedha ya ziada ya usajili ikikosekana Yanga itapata wapi wachezaji kama si kuwatumia vijana hawa?

Nadhani bado kuna tatizo la kiungozi katika timu ya vijana ya Yanga, kwani kocha anaonekana kama ndiye meneja anayejua matatizo yote ya kila mchezaji na kutatua au kuweka daraja la wachezaji na uongozi.

Kuna kitu Yanga inapaswa kukifanya ili iweze kufanikiwa katika soka la vijana na iweze kufanikiwa kwani kwa kuendelea kufanya mambo ya sasa hali itaendelea kuwa ya kawaida na mafanikio hayataonekana.

Viongozi wasiibuke kutoka walipojichimbia na kujisogeza kwa timu baada ya kuona inaelekea kupata mafanikio, huu ni utamaduni ambao haufai kama kweli tunataka mafanikio katika soka.

No comments: