Mpigania haki za weusi na alama kuu ya udhalimu wa mfumo wa Ubaguzi wa Rangi nchini Afrika ya Kusini Mzee Nelson ‘Madiba’ Mandela amefariki dunia baada yakuugua kwa muda mrefu kufuatia maambukizi ya mapafu kushindwa kutengemaa kwa muda sasa. Mzee Mandela ambaye kwa miezi kadhaa sasa amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya maambukizi kwenye mapafu yake amefariki dunia nyumbani kwake ambako alipelekewa toka hospitali ya Moyo ya Mediclinic mjini Pretoria, chini Afrika ya Kusini baada ya familia yake kuomba kufanya hivyo.
Bw. Mandela (95) alikuwa Rais wa kwanza mweusi wa Afrika ya Kusini kufuatia kutokomezwa kwa utawala wa ubaguzi wa rangi uliofanywa na Makaburu kwa karibu miaka 400 ambapo watu weupe walijipa haki ya kuwatawala na kuwabagua watu weusi. Kabla ya kuwa Rais wa Afrika ya Kusini Mzee Mandela alitumikia kifungo cha miaka 27 jela ambako pamoja na kazi ngumu aliendelea kuongoza kundi la wapigania haki wengine kudai usawa, utu, na umoja wa Waafrika ya Kusini. Mandela alikuwa ni mfungwa maarufu zaidi wa kisiasa duniani ambapo harakati za kutaka afunguliwe zilipiganwa na wanaharakati sehemu mbalimbali duniani licha ya upinzani wa Serikali ya Afrika ya Kusini na Baadhi ya Nchi za Kimagharibi ambazo zilimuona Mandela kama Ghaidi na mchochezi.
Maisha yake ya awali
Mzee Mandela alizaliwa Julai 18, 1918 katika kijiji cha Mvezo mji mdogo wa Umtatu Jimbo la Cape. Akiwa ni mmoja wa watoto wa Mzee Gadla Henry Mphakanyiswa Nelson Mandela alikulia kwa mamake – mke wa tatu wa Mzee Gadla – katika kijiji cha Qunu ambako pamoja na shughuli nyingine za nyumbani alikuwa mvulana mchunga ng’ombe.
Mandela akiwa amevaa mavazi ya kabila lake la Xhosa; alitoka katika familia ya kichifu.
Kuingia Katika Siasa
Alipokuwa akiishi kwa muda na mmoja wa binamu zake Nelson Mandela
alitambulishwa kwa mwanaharakati wa chama cha ANC Bw. Walter Sisulu
ambaye baadaye walifungwa pamoja – Sisulu akitumikia miaka 25 jela.
Walter Sisulu alimtafutia kazi ya ukarani katika kampuni ya Wanasheria
ya Witkin, Sidelsky and Edelman. Akiwa hapo alifanya masomo ya elimu kwa
njia ya Posta ambapo alikuwa anatafuta shahada yake ya kwanza. Mwaka
1943 alihitimu masomo yake ya sheria na kuanza kazi kama Mwanasheria
badala ya kurudi kijijini kutumika kwa Chifu. Akiwa ameanza kazi kama
Mwanasheria Mandela aliendelea kuwa chini ya uangalizi wa Walter Sisulu
ambaye alikuwa anaendeleza harakati za kudai haki za weusi. Akikutana
mara kwa mara na wanaharakati wengine nyumbani kwa Sisulu Mandela
alikutana tena na rafiki yake Oliver Tambo. Ilikuwa ni katika mikutano
hiyo alikutana na mwanamama Evelyn Mase ambaye walianza uhusiano wa
mapenzi na baadaye kufunga ndoa yake ya kwanza Oktoba , 1944. Walijaliwa
watoto wawili wa kiume na wa kike; wa kiume Madiba “Thembi” Thembikile
alizaliwa Februari 1946 na wa kike Makaziwe alizaliwa mwaka uliofuatia
lakini alifariki miezi tisa baadaye baada ya kupata maambukizi ya
ugonjwa uti wa mgongo.
Baada ya uchaguzi wa 1948 ambapo watu weupe peke yao walishirikia
vyama vya Herenigle Nacionale Party na Afrikaner Party viliungana na
kuunda chama cha National Party ambacho kilikuwa na sera ya wazi ya
ubaguzi na kikapisha na kupanua ukali wa sera ya ubaguzi kupitia sheria
mbalimbali za ubaguzi wa rangi. Serikali ya Kikaburu ikaja na mojawapo
ya Sheria kali kabisa za kupambana na wanaharakati ambayo inajulikana
kama Ukandamizaji wa Ukomunisti ya 1950. Sheria hii ilikuwa
inashughulikia karibu mambo yote yanayohusiana na kuipinga serikali na
ikiwahusu watu wote. Migongano kati ya ANC na Serikali ya Kikaburu
ilianza kupamba moto.
Mwaka 1952 Nelson Mandela alikamatwa na utawala wa Makaburu kwa kile kilichodaiwa kujihusisha na vitendo vya Kikomunisti chini ya ile sheria iliyopitishwa miaka michache nyume. Alihukumiwa miezi tisa jela na “kazi ngumu” lakini utekelezaji wa hukumu hiyo ulisitishwa kwa miaka miwili. Lakini mwezi Disemba mwaka huo huo Mandela alipigwa marufuku kuzungumza na zaidi ya mtu mmoja kwa miezi sita. Akiwa kiongozi wa ANC hii ilimaanisha kuwa asingeweza kufanya mikutano na wanachama wake. Mwaka 1953 Mandela na rafiki yake Oliver Tambo walifungua kampuni yao ya Wanasheria katika Jiji la Johannesburg na kuifanya kuwa kampuni ya kwanza ya Wanasheria Weusi katika Afrika ya Kusini.
Walijishughulisha na malalamiko mbalimbali ya wananchi hasa yanayohusiana na ukatili wa kisiasa. Hata hivyo serikali ikitumia sheria nyingine ikalazimisha kufungwa kwa ofisi hiyo iliyokuwa na wateja wengi na kuihamisha sehemu nyingine ambapo ilikuwa ni vigumu kwa wateja kuifikia. Mwaka 1955 Mandela na wenzake walishirikiana kuandaa kongamano kubwa la watu wa Afrika Kusini ambao wanaamini katika taifa moja la watu wamoja japo wanatoka katika makabila na rangi mbalimbali. Katika kongamano hili kulisainiwa kile kinachoaminika kama mojawapo ya nyaraka muhimu kabisa za kutetea usawa na utu wa watu wote ambayo ilijulikana kama Freedom Charter. Kufananisha hii ni sawasawa na Azimio la Uhuru la Marekani au ile nyaraka ya Waingereza ya Magna Carta. Kwa Tanzania tunaweza kufananisha kabisa na Azimio la Arusha. Freedom Charter ilitengeneza ramani ya kujenga taifa la watu walio huru na sawa katika Afrika Kusini.
Migogoro na utawala wa kikaburu haikukoma. Na Mandela alizidi kuwa
na siasa za mrengo wa kushoto. Njia za amani za kupata mabadiliko ya
kisiasa zilionekana kutozaa matunda; Mandela na wenzake walianza kuamini
katika njia za kimapinduzi na za kutumia silaha. Hili lilimletea
matatizo zaidi na watawala wa Kikaburu. Hatimaye Augusti 2, 1962 Nelson
Mandela alikamatwa na utawala wa Makaburu na kushtakiwa kwa kuchochea
mgomo wa wafanyakazi na kuondoka nchini bila kibali. Mandela
alijiwakilishi mwenyewe mbele ya mahakama huku akitumia nafasi hiyo
kutoa hutuba motomoto za kisiasa dhidi ya utawala wa kibaguzi wa
makaburu. Alikutwa na hatia na kuamuriwa kufungwa miaka mitano jela;
wakati anatoka mahakamani mashabiki wake walisimama pembeni na kuimba
wimbo wa Mungu Ibariki Afrika (Nkosi Sikeleli Afrika).
Kesi ya Rivonia
Matatizo yake hayakufikia mwisho. Julai 11, 1963 polisi walivamia
shamba la Lilliesleaf – mji mdogo wa Rivonia nje ya Johannesburg) ambapo
pamoja na vitu mbalimbali waliamini walikuta ushahidi wa kutosha
kumhusisha Mandela na mipango ya kuipindua serikali. Mandela na wenzake
walitumia shamba hili kama sehemu yao ya kujificha huku Mandela
akijifanya ni mtunza bustani. Kesi hii ilikuwa motomoto kwani Mandela na
wenzake walishtakiwa kwa makosa manne yakiwa ni ya uhujumu wa miundo
mbinu ya nchi (vitendo zaidi ya 200) pamoja na kutaka kupindua serikali;
serikali ilikuwa inapendekeza kuwa wakikutwa na hatia basi wahukumiwe
kifo. Mashahidi wengi wa serikali waliitwa pamoja na lundo la ushahidi
wa picha na nyaraka kuthibitisha mashtaka ya serikali dhidi ya Mandela
nawenzake tisa.
Alisema kuwa hapiganii haki ya weusi kuwabagua weupe bali haki ya watu wote kuishi kwa pamoja kama watu wa jamii moja. Mandela alisema “This is the struggle of the African people, inspired by their own suffering and experience. It is a struggle for the right to live. I have cherished the ideal of a democratic and free society, in which all persons live together in harmony and with equal opportunity. It is an ideal which I hope to live for and achieve. But, if needs be, my Lord, it is an ideal for which I am prepared to die”. Yaani, “Haya ni mapambano ya watu wa Afrika yaliyotokana na mateso na mang’amuzi yao wenyewe. Haya ni mapambano ya kupigania haki ya kuishi. Nimelifurahia wazo la jamii ya kidemokrasia na huru, ambapo watu wote wanaishi katika amani na haki sawa. Ni wazo ambalo ninatumaini kuishi kwa ajili yake na kulitimiza. Lakini, ikibidi, mheshimiwa, ni wazo ambalo nimejiandaa kufa kwa ajili yake”.
Pamoja na utetezi wake wote timu ya
Mandela ilishindwa kesi hii na wote wakakutwa na hatia isipokuwa mmoja.
Kwa vile tayari kulikuwa na mwamko sehemu mbalimbali duniani kupinga
adhabu ya kifo Mahakama ikawaamuru Mandela na wenzake kutumikia kifungo
cha maisha na huo ndio ukawa mwanzo wa kifungo cha karibu miaka 30 jela
(ikumbukwe kesi hii ilipoanza Mandela tayari alikuwa anatumikia ile
hukumu ya miaka 5 jela). Mandela na wenzake walipelekwa katika jela ya
Kisiwa cha Robben ambako pale peke yake alitumikia miaka 18. Maisha
kifungoni Kisiwa cha Robben na kwingine.
Kisiwa cha Robben ambako Mandela alifungwa kwa miaka 18.
Mandela na wenzake walihukumiwa kazi ngumu vile vile na kweli ilikuwa
ni kazi ngumu kwani pamoja na kuponda mawe walipewa baadaye kazi ya
kuponda mawe ya chokaa. Kwa muda alikatazwa kuvaa miwani ya jua kitua
mbacho kilimsababishia ubovu wa macho ambao hakuweza kupona kabisa.
Akiwa kifungoni mamake alimtembelea mwaka 1968 na siku chache baadaye
alifariki dunia, mwaka uliofuata mtoto wake wa kwanza Thembi alifariki
katika ajali ya gari – Mandela hakuruhiswa kuhudhuria mazishi yao wote
hao. Maisha kifungoni yalikuwa magumu kwa kila kipimo licha ya maisha
baada ya miaka kuanza kuboreshwa kidogo kufuatia maandamano na harakati
za kutaka Mandela afunguliwe. Utawala wa makaburu hawakusikia la mtu
yeyote hasa kwa vile walikuwa wanaushirika wa karibu na serikali ya
Marekani na Uingereza ambazo zote zilimuona Mandela kama Mkomunisti na
Ghaidi.Mandela alitumikia pia katika magereza ya Pollsmoor huko Cape Town na Gereza kati ya 1982 hadi 1988 na baadaye gereza la Victor Verster 1988-1990 ambako kwa kiasi kikubwa alikuwa amepewa maisha ya unafuu (hapa chini akiwa na mpishi na huduma mbalimbali) kulinganisha na alivyoishi katika gereza la Kisiwa cha Robben.
Kuingia kwa F. W. de Clerk na kuachiliwa kwa Mandela
Chini ya utawala wa Pieter Botha Afrika ya Kusini ilizama katika siasa na sera za ubaguzi wa rangi. Botha aliwachukia weusi na aliamini kabisa kuwa utawala wa kikaburu utadumu kwa muda mrefu. Botha anaweza kabisa kufananishwa na aliyekuwa Gavana wa Alabama George Wallace ambaye aliapa kuwa “ubaguzi sasa, ubaguzi kesho, ubaguzi milele”; japo aliishi na kuona Ubaguzi ukifumuliwa katika jimbo lake na katika Marekani sera hizo zikitupwa katika mifumo ya utawala. Hata hivyo alikuwa ni F. W. de Clerk mwanasiasa mwingine mzungu ambaye licha ya kutoka katika chama kilichoamini katika ubaguzi wa rangi yeye mwenyewe alijikuta akiukataa kifikra kwani aliona hauwezi kudumu.
Kwa muda hivi tangu 1988 Mandela alikuwa na mazungumzo ya siri na baadhi ya viongozi wa serikali juu ya masharti ya yeye na wenzake kuachiwa huru na mwelekeo wa siasa za Afrika ya Kusini. Mazungumzo hayo yalikumbana na vikwazo vingi sana ikiwemo kutokukubaliana kwa masharti – kwa mfano serikali ilitaka Mandela asijiingize kwenye siasa na kuwa wasilazimishwe kuwa na utawala wa wengi (majority rule) masharti ambaye Mandela aliyakataa.
Uchaguzi Mkuu wa 1994
Hatimaye Afrika ya Kusini ikaingia katika uchaguzi mkuu wa kwanza huru na wawananchi wote mwaka 1994, Aprili 27. Kampeni ilikuwa na vurugu za hapa na pale lakini kwa ujumla wananchi wa Afrika ya Kusini hasa weusi walijikuta kwa mara ya kwanza wanapiga kura kumchagua kiongozi wanayemtaka. Mandela akiongoza ANC walishinda asilimia 62 ya kura na kushindwa kupata theluthi mbili ambayo ingewawezesha kuweza kubadili Katiba. Serikali yake ilikuwa ni ya umoja wa kitaifa ikitegemea kwa kiasi kikubwa baadhi ya maofis waliokuwa katika utawala wa kikaburu. De Clerk alikuwa Makamu wa kwanza wa Rais na Thabo Mbeki akiwa Makamu wa Pili wa Rais. Mandela (katikati) akiwa na Makamu wake wawili
Mandela alishaeleza toka awali kuwa atagombea kipindi kimoja tu na ndivyo alivyofanya na baadaye kumwachia Thabo Mbeki kama Rais wa Afrika ya Kusini. Baada ya kustaafu siasa Mandela aliamua kujishughulisha na program mbalimbali za ndani ya Afrika ya Kusini na kutembelea baadhi ya nchi. Hata hivyo udhaifu wa mwili uliotokana na magonjwa na uzee ulimzidia na kumfanya apunguze safari za nje. Kwa mara ya mwisho alionekana katika shughuli za hadhara katika mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2010 ambayo yalifanyika Nchini Afrika ya Kusini.
Mandela na Tanzania
Tanzania kama nchi imehusika kwa kiasi kikubwa sana katika kuuvunja vunja utawala wa kikaburu na katiak kuongoza harakati za kutaka Mandela aachiliwe huru. Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na utawala wake mara baada ya Uhuru 1961 aliazimia kutoa msaada wote unaohitajika kwa wapigania uhuru wa Afrika ya Kusini. Kama ilivyodokezwa hapo juu kuwa mojawapo ya mashtaka dhidi ya Mandela ni lile la kwenda nje ya Afrika ya Kusini bila kibali. Mwaka 1962 Mandela akitumia njia za panya alitoroka Afrika ya Kusini na hatimaye kuingia Tanganyika na kukutana na Mwalimu Nyerere ambaye aliwapa ahadi ya ushirikiano mkubwa. Mandela mwenyewe akizungumza katika dhifa aliyomwandaliwa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere mwaka 1997 Oktoba 17; alisema “Inanyenyekesha kukumbuka mchango wa Mwalimu Nyerere katika ukombozi wa bara letu na Uhuru wa Afrika ya Kusini”.
Katika kuonesha hili Mandela alichagua Tanzania miongoni mwa nchi
za kwanza kutembelea mara baada ya kuachiliwa huru mwaka 1990. Aliingia
nchini Machi 7, 1990 na kupokelewa na maelfu ya watu wakiongozwa na baba
wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere pamoja na Rais Ali Hassan Mwinyi.
Wakati anatembelea nchini kama mtu huru Tanzania ilikuwa na wapiganaji
karibu 10,000 wa Afrika ya Kusini waliokuwa wanaishi Tanzania na
kujihusisha na mambo mbalimbali. Ikumbukwe ANC ilifungua ofisi yake ya
kwanza nje ya Afrika ya Kusini Jijini Dar-es-Saalam mwaka 1961 na hii
ilichangia baadaye pia kwa ofisi za vyama vingine vya ukombozi kuchagua
Dar kama makao yao makuu.
Yote haya yalisaidia kuifanya Tanzania kuwa makao makuu ya Kamati
ya Ukombozi ya Nchi Zilizo Mstari wa Mbele ambayo kwa muda mrefu
iliongozwa na Brig. Hashim Mbita. Uhusiano huu wa karibu wa Tanzania na
Wapigania Uhuru ulithibitika zaidi baada ya Tanzania kuwapatia wapigania
uhuru hao maeneo ya mafunzo ya kijeshi na taaluma mbalimbali huko
Morogoro eneo la Mazimbu na maeneo mengine Mtwara na sehemu nyingine
nchini. Pamoja na vyuo wapigania uhuru hao walipewa maeneo ya shule za
msingi na sekondari vile vile.
Mandela ametutoka baada ya maisha ambayo ametumikia nchi yake, bara
lake na dunia kwa namna ambayo ameacha alama ya kudumu ya kukumbukwa.
Kwa mtu ambaye utawala wa kikaburu ulimnyima haki nyingi za msingi na
kumchukulia miaka ishirini na saba ya maisha yake angeweza kuwa mtu
mwenye kisasi pale aliposhika madaraka kama Rais wa nchi yake. Mtu
ambaye alinyanyaswa, kuteswa, na kushindwa hata kuhudhuria mazishi ya
mamake kwa namna ya kawaida angekuwa ni mtu mwenye kinyongo sana.
Hata hivyo Mandela alionesha huruma na msamaha wa hali ya juu sana. Aliposhika madaraka alihakikisha kuwa watu weupe wanajihisi salama na kuondoa kabisa roho ya kulipiza kisasi hasa kwa watu weusi ambao waliumia sana mikononi mwa weupe kwa karibu miaka 400. Anapoitwa “Baba wa Taifa” la Afrika ya Kusini haitwi hivyo kirahisi. Mchango wake wa pekee kwa nchi yake unamuweka katika nafasi ya pekee kukumbukwa na vizazi vingi vijavyo. Hali hii ya msamaha iligusa hata maisha yake binafsi. Pamoja na kupata habari za mkewe Winnie Mandela kukosa uaminifu Mandela bado alihakikishia kuwa anapatiwa uwakilishi wa kutosha kujitetea kwenye kesi iliyomkabili ya utekaji na mauaji. Hata baada ya kuachana naye Mandela na mkewe mpya Graca Machel – aliyekuwa mke wa marehemu Samora Machel (Rais wa Msumbiji aliyeuawa kwa njama za makaburu) – Mandelea amekuwa na mahusiano mazuri na ya utulivu na Winnie ambaye ameshiriki vilivyo katika kumuuguza Madiba.
Dunia kwa hakika imepoteza shujaa wa haki za binadamu, nyota ya Afrika na mfano wa viongozi ambao waliweka maslahi ya watu wao mbele zaidi kuliko furaha zao binafsi na za familia zao. Wananchi wa Afrika ya Kusini wanapomlilia wanaungana na mamilioni zaidi katika bara la Afrika na Dunia ambao wanakumbuka nafasi ya Mandela katika maisha yao.
Kwa Watanzania wengi hasa waliokua miaka ya sabini na themanini harakati za kutaka Mandela afunguliwe na kukomeshwa kwa utawala wa kikaburu zilikuwa ni sehemu ya maisha yao. Hawa pia wanamshukuru Mungu kwa maisha ya Mandela na wanaungana kutoa rambirambi na pole kwa familia ya Mandela na kumwombea pumziko la amani baada ya maisha ya uchovu na kazi ngumu. Watanzania wanaungana na ndugu zao wa Afrika ya Kusini katika maombolezo haya; wao wenyewe wanakumbuka vile vile jinsi walivyoondokewa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na jinsi akili ya jumla ya Taifa ilivyoguswa lakini pia kuonekana kwa kubadilika kwa taifa kwa kutokuwepo Mwalimu. Ni wazi kuwa hata Afrika ya Kusini nayo itapita huku ambapo ile Dhamira ya Taifa (Consciousness of a Nation) yaani Mandela atakuwa hayupo. Njia pekee ya kuhakikisha kuwa Afrika ya Kusini inazidi kujijenga katika maisha ya kisasa na kuinua watu wake kuelekea maendeleo ni lazima kukumbuka umoja na udugu ambao Mandela alipigania.
MUNGU AMLAZE PEMA PEPONI AMEN!!!!!!!!!!!!!!
No comments:
Post a Comment