Kwa mujibu wa ratiba ya mkutano huo, leo wabunge
watachangia ripoti tatu za kamati za kudumu za Bunge zinazosimamia fedha
za umma zilizowasilishwa wiki iliyopita.
Ripoti zitakazoendelea kujadiliwa ni pamoja na ya
Kamati ya Serikali za Mitaa (Laac), ambayo inaonekana kuwagusa wabunge
wengi kutokana na kuibua ufisadi wa kutisha.
Wabunge pia wataendelea kuchangia ripoti ya Kamati
ya Bunge ya Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma inayoongozwa na
Zitto Kabwe (PAC) na ile ya Bajeti inayoongozwa na Andrew Chenge.
Baada ya kukamilika kwa mijadala hiyo, Serikali
inatarajiwa kujibu hoja mbalimbali za wabunge ambao wameonyesha
kutoridhishwa na utendaji wa baadhi ya mawaziri.
Kuendelea kuwapo kwa vitendo vya wizi, ubadhirifu
na ufisadi kwa baadhi ya wizara kunaonekana kuwachefua wabunge hata
baadhi yao kumshauri Rais Jakaya Kikwete kuwawajibisha.
Baadhi ya wabunge waliochangia Ijumaa na Jumamosi
iliyopita walimtaka Rais Kikwete kumfukuza kazi Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda. Wengine walimtaka amfukuze kazi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu, Tamisemi, Hawa Ghasia, kwa kushindwa kukabiliana na ufisadi.
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola ndiye
aliyekuwa mwiba kwa Pinda akisema amekuwa mpole na hawajibiki ipasavyo.
Alisema katika nchi nyingine, wakati Kamati za Bunge zinawasilisha
taarifa zake ndipo jicho la wananchi na Serikali linakuwa bungeni lakini
kwa Tanzania imekuwa ni tofauti.
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David
Kafulila alisema taifa lina matatizo makubwa mawili ambayo ni ukusanyaji
kodi na matumizi mabaya ya fedha.
“Tunaposema Serikali imechoka maana mbadilishe
kikosi, mpaka dakika 90 ziishe? Wabunge wa CCM mtakubaliana nami kwamba
hii ni dalili kwamba mmechoka mbadili kikosi,” alisema na kuongeza:
“Waziri Mkuu wetu tumeshamzoea kila suala
tunalomwambia anakwambia tunaangalia, tunafuatilia, tuko mbioni
yanazungumzika… tumechoka na haya.”
Alisema mawaziri mizigo walitajwa katika ziara ya
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana wako wanne lakini Pinda ndiye
namba moja.
No comments:
Post a Comment