Saturday, 20 June 2015

Tanzania yatajwa tena kama kinara wa ujangili


Tanzania imetajwa kwa mara nyingine kama moja ya nchi ambako ndovu wanauawa kwa wingi kwa ajili ya biashara za pembe. Wachunguzi wa kimataifa waliotumia DNA kutoka pembe za ndovu ili kutambua chanzo chake wametaja maeneo mawili ambapo mauaji ya ndovu yanafanyika kwa kiwango kikubwa.
Matokeo ya utafiti yaliyochapishwa Alhamisi yanaonyesha maeneo hao mawili ni Tanzania, ikifuatiwa na eneo la nchi kadha katika eneo la magharibi ya kati barani Afrika.
Samuel Wasser, mmoja wa waandishi wa ripoti hiyo iliyochapishwa katika jarida la Sayansi, amesema anatumai kuwa utafiti huo utawezesha maafisa usalama kuelekeza juhudi zao na kuongeza shinikizo la kimataifa dhidi ya nchi katika kupambana na ujangili.

Ukubwa wa shehena za pembe zilizokamatwa kutoka maeneo hayo - zaidi ya tani moja - inaonyesha kuwa magenge ya kimataifa yanashirikiana na maafisa wala rushwa katika nchi hizo kuendelea biashara ya pembe.
Wasser ambaye ni mkurugenzi katika chuo kikuu cha Washington, Seattle, anasema maeneo hayo yaliyotajwa, ikiwemo Tanzania, ni "maeneo moto" katika biashara ya pembe za ndovu.
Idadi ya ndovu katika maeneo hayo tayari ilikuwa inajulikana kuwa imeshuka kutoka na kuwindwa na majangili kwa maelfu katika miaka ya hivi karibuni lakini utafiti huu ni uthibitisho mwingine kuwa uwindaji haramu ni mkubwa katika nchi hizo.
Waziri wa mali asili na utalii wa Tanzania, Lazaro Nyalandu, amesema nchi hiyo tayari imechukua hatua za kupambana na ujangili, ikiwa ni pamoja na kuajiri walinzi wa wanyama pori 500, na kuanzisha kituo cha kulea ndovu watoto waliopoteza wazazi wao.

No comments: