Klabu ya soka ya Azam ya jijini Dar es Salaam imemnasa kipa aliyewahi
kusajiliwa na timu ya Chelsea ya Uingereza, Vincent Depaul Angban (30),
raia wa Ivory Coast.
Nyota huyo amezaliwa Februari 2 mwaka 1985 na amewahi kuichezea timu ya taifa ya Ivory Coast.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana jijini, mazungumzo kati ya kipa
huyo na uongozi wa Azam yamekamilika na anatarajiwa kutua nchini wakati
wowote ili kujiunga na klabu hiyo yenye makao makuu yake Chamazi,
Mbagala pembeni kidogo ya jiji.
Chanzo chetu kimeeleza kwamba lengo la kipa huyo kusajiliwa ni
kuimarisha kikosi chao ambacho mapema mwakani kitapeperusha bendera ya
Bara katika mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho.
"Timu yetu inazidi kuimarika, tuko katika mipango ya mwisho ya
kumleta kipa wa kimataifa lakini alishawahi kupitia Chelsea," alisema
mmoja wa viongozi wa klabu hiyo ambayo ilitwaa ubingwa wa bara msimu wa
mwaka 2013/ 2014.
Kiongozi huyo alisema pia Azam iko tayari kusajili wachezaji 10 au
zaidi wa kimataifa, lakini mipango yao inashindikana kutekelezwa
kutokana na kusubiri kanuni za ligi zipitishwe.
Endapo usajili wa kipa huyo utakamilika, ushindani wa namba kwenye
kikosi hicho utaongezeka dhidi ya makipa waliopo, Aishi Manula na
Mwadini Ali.
Kabla ya kuanza kwa ligi ya Bara Agosti 22 mwaka huu, Azam pia
imeshaanza maandalizi kwa ajili ya mashindano ya Klabu Bingwa Afrika
Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) ambayo yatafanyika hapa nchini mwezi
ujao.
Klabu hiyo inayomilikiwa na mfanyabiashara maarufu nchini Said
Salim Bakhressa, imemrejesha kocha Muingereza, Stewart Hall, kuongoza
benchi la ufundi la timu hiyo.
Usajili wa kipa huyo ukikamilika, Azam itakuwa na wachezaji wanne
kutoka Ivory Coast wakiwamo mapacha, Kipre Tcheche na Kipre Balou na
Pascal Serge Wawa.
No comments:
Post a Comment