Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Freeman Mbowe, amezungumzia hatma yake kisiasa baada ya Mahakama ya
Hakimu Mkazi Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro kumtia hatiani katika
kesi ya shambulio, akisema hajapoteza sifa ya kutetea ubunge wake
katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Mbowe alihukumiwa juzi na mahakama hiyo kwenda jela mwaka mmoja au
kulipa faini ya shilingi milioni moja baada ya kupatikana na hatia
katika kesi namba 73 ya mwaka 2011 iliyokuwa imefunguliwa na Mwangalizi
wa Ndani wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Nassir Uronu.
Hata hivyo, Mbowe alifanikiwa kulipa faini hiyo na kuepuka kwenda jela kutumikia kifungo cha mwaka mmoja.
Akiwahutubia wakazi wa mji wa Bomang’ombe uliopo wilayani hapa ja
ikiwa ni siku moja tangu mahakama itoe hukumu hiyo, Mbowe alisema:
“Nimezungumza na wanasheria makini na wameniambia kwamba siyo tu
wanataka kutetea rufaa yangu bali pia kupinga mifumo ya ukandamizaji.
Kwa hiyo wanataka kufanya hivyo pia ili kuniondolea doa la uadilifu kama
kiongozi.”
Alisema na kuongeza:
“Kuna wakati fulani nilishawishiwa nitoe hongo ili kesi hii
imalizike lakini nilikataa na nikasema siwezi kufanya hivyo. Kwangu ni
haramu kutoa rushwa na hata hivyo siwezi kuachia ubunge wa Hai, nyie
wananchi wangu mnajua, nimewauliza hapa na mmenipa ruhusa kugombea.”
Katika kesi hiyo, Nassir aliyekuwa Mwangalizi wa ndani kutoka
Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) alidai kushambuliwa kwa kipigo
akiwa katika kutuo cha kupigia kura cha Zahanati ya Kijiji cha Nshara,
kata ya Machame Kaskazini, wilaya ya Hai.
Katika mkutano huo wa jana baadhi wa wabunge wa Chadema
walihudhuria akiwamo Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, Mbunge
wa Rombo, Joseph Selasini, Wabunge wa Viti Maalum, Rose Kamili, Grace
Kihwelu, Cecilia Pareso, Joyce Mukya, Paulina Gekul na Lucy Owenya, huku
wakieleza kumuunga mkono Mbowe kutetea kiti chake cha ubunge.
Katika mkutano huo, Mbowe aliwakabidhi pia wananchi wa wilaya ya
Hai lori la tani 50 aina ya Mercedez Benz ambalo litatumika kuzoa
takataka katika maeneo yote ya jimbo hilo, ikiwa ni ahadi yake aliyoitoa
wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Kesi hiyo ya uchaguzi mkuu uliopita, imekuwa ikivuta hisia za
wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro kutokana na nguvu ya kisaisa aliyonayo
mwenyekiti huyo wa Chadema na na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni.
Katika uchaguzi huo, Mbowe aliibuka mshindi kwa kupata kura 28,585,
akifuatiwa na Fuya Kimbita (CCM) kura 23,349, Hawa Kihogo (UDP) 258 na
Petro Kisimbo (TLP) kura 135.
No comments:
Post a Comment