Sunday, 28 June 2015

Raia 47 wa kigeni wakuliwa mateka waokolewa huko Sudan

Raia 47 wa kigeni waliochukuliwa mateka waokolewa SudanKikosi cha usalama chapambana na kundi la wahaini wa biashara haramu ya binadamu nchini Sudan

Kikosi cha usalama kimeripotiwa kuwaachilia huru raia 47 wa kigeni waliokuwa mikononi mwa wahaini wa biashara haramu ya binadamu katika eneo la mashariki mwa Sudan.
Mkuu wa polisi mkoani Kassala, Jenerali Omar Al Mukhtar, alitoa maelezo na kuarifu kuachiliwa huru kwa mateka hao baada ya mapambano makali kati ya kikosi cha usalama na watu 10 waliojihami kwa silaha.
Al Mukhtar alifahamisha kwamba mateka hao walioachiliwa huru, wote walikuwa ni wanaume kutoka nchi ya Eritrea na Ethiopia.
Al Mukhtar pia aliwatambulisha wahaini hao waliojihami kwa silaha kuwa ni raia wa kigeni, ingawa hakubainisha asili yao wala nchi waliyotoka.

Kikosi cha usalama kilipambana na kundi la wahaini katika eneo la Bahar lililoko katika mpaka wa Sudan na Eritrea kabla ya kufanikiwa kuwaokoa mateka 47.
Visa vya biashara haramu za binadamu vimeshamiri katika maeneo ya mpaka wa Sudan, Eritrea na Ethiopia huku mamia ya raia wa kigeni wakichukuliwa mateka mara kwa mara.
Baadhi ya mashirika ya kutetea haki za kibinadamu, yamekuwa yakishutumu viongozi wakuu wa maeneo ya mipakani kwa madai ya kuhusika na biashara haramu za binadamu, ingawa Sudan inakanusha madai hayo.

No comments: