STRAIKA mpya wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’ aliyezifunga Yanga,
Simba na Azam msimu uliopita, amesema hana shida kabisa na nafasi
atakayopangwa kucheza Msimbazi kwani yuko fiti kucheza nafasi zote za
ushambuliaji.
Mgosi amesajiliwa na Simba akitokea Mtibwa Sugar
ya Morogoro ambako alicheza zaidi nafasi ya winga msimu uliopita licha
ya kuzoeleka kucheza nafasi ya straika alipokuwa Simba miaka ya nyuma.
Mfungaji Bora huyo wa mwaka 2010, alisema anaweza
kufanya vizuri akicheza straika, winga kwa pande zote mbili pamoja na
kiungo mshambuliaji, hivyo kocha atakavyoamua ndivyo atakavyoitumikia
timu yake.
“Sina wasiwasi na uwezo wangu, kama ulivyoona
msimu uliopita nilicheza zaidi kama winga na niliifanya kazi yangu
vizuri, kocha akiamua nicheze straika ama kiungo mshambuliaji bado
naweza.
“Kikubwa ninachohakikisha kwa sasa ni kuuweka
mwili wangu vizuri kwa ajili ya changamoto hiyo. Licha ya kwamba
nimecheza kwa muda mrefu, bado nina uwezo wa kumudu nafasi hizo zote,”
alisema Mgosi.
Straika huyo amerejea Simba miaka minne baada ya
kutimka klabuni hapo kwenda kujaribu bahati ya soka la kulipwa nchini
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kabla ya kurejea nchini na
kujiunga na Mtibwa aliyoitumikia tangu mwaka 2012.
Katika hatua nyingine, Simba imepanga kuanza
mazoezi yake Julai Mosi, lakini haijafahamika itakluwa wapi na programu
gani zitaanza na chini ya makocha wapi.
Kocha msaidizi wa Simba, Selemani Matola, alisema anachojua yeye ni kuanza mazoezi Julai ila hajajua ni uwanja gani.
“Nimeambiwa mazoezi Julai Mosi, sijaambiwa ni wapi
ndani au nje ya nchi, lakini siku zikikaribia kila kitu kitakuwa wazi
lakini kwa sasa suala hilo lipo juu ya uongozi,” alisema.
Matola alisema anaamini watafanya maandalizi
mazuri kwa ajili ya msimu ujao kwani wanachokihitaji wao ni kuona Simba
inakuwa na mabadiliko ya kufanya vizuri.
“Kila kitu kitakwenda sawa tutafanya maandalizi
kama wengine ili kuweza kuwa kwenye ushindani wa hali ya juu katika
msimu ujao wa Ligi Kuu Bara,” alisema.
No comments:
Post a Comment