Wednesday, 17 June 2015

Jaji mkuu mstaafu Agustino Ramadhani amejiunga na makada wengine wa chama cha CCM kuchukua fomu ya kuwania urais.

Hatimaye jaji mkuu mstaafu Agustino Ramadhani amejiunga na makada wengine wa chama cha mapinduzi kuchukua fomu ya kuwania urais ambapo pamoja na mambo mengine amesema amejipima na kuona anafaa kuwatumikia watazania huku akijinadi katika utumishi wake kwa umma hajawahi kushiriki au kuhusishwa kwa namna yeyote ile kwenye kashfa ya rushwa na ufisadi.
Jaji Agustino Ramadhani ambaye pia ni rais wa mahakama ya Afrika ya haki za binadamu yenye makao makuu yake jijini Arusha aliwasili makao makuu ya CCM majira ya saa sita na nusu akisindikizwa na familia yake tu na mara baada ya kuchukua fomu akifanya mkutano na waandishi wa habari na kueleza mambo mbalimbali yaliyomsukuma kuwania nafasi hiyo. 
 
Jaji Agustino pia akazungumzia namna atakanyokabiliana na changamoto za rushwa na ufisadi ambazo zinatajwa kurudisha nyuma maendeleo ya taifa kwa kiasi kikubwa huku akiahidi kama atapata ridhaa ya watanzania atahakikisha anatumia uzoefu wake wa muda mrefu katika masuala ya kisheria kutokomeza.
 
kuhusu matukio ya kinyama na kikatili yakiwemo mauaji ya albino ambayo siku za hivi karibuni yameshika hatamu na kulitia taifa doa ulimwenguni jaji Agustino amesema kuwa mambo hayo yanahitaji ushirikiano wa hali ya juu kati ya jamii na mamlaka zinazohusika ikiwemo kutoa elimu ya kutosha kuondoa imani hizo huku akionya hatakuwa na mzaha kwa watu watakaobainika kuhusika.
Jaji Agustino Ramadhani anakuwa kada wa sita wa chama cha mapinduzi CCM kuingia katika kinyang'anyiro cha kuwania urais kupitia chama hicho.

No comments: