Tuesday, 23 June 2015

Membe, Nikiwa rais ikulu nitazihamishiwa Chamwino

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe, amesema kama CCM kitamteua kuwa mgombea urais na kushinda katika Uchaguzi Mkuu ujao, atahakikisha Ikulu na nyumba za wizara zote zinahamia Dodoma. 

Bw. Membe ambaye ni miongoni mwa wagombea urais ndani ya CCM, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wakazi wa mkoa huo na wana CCM waliojitokeza kumdhamini.

"Hili jambo nimelifikiria muda mrefu, hayati Mwalimu Julius Nyerere, alitumia nguvu na fedha nyingi kujenga Ikulu ya Chamwino hivyo nikiwa rais, nitahamia Dodoma."Siwezi kukaa hapa peke yangu, lazima Mawaziri wangu wote nao waishi jirani na mimi," alisema Bw. Membe na kuongeza;
"Kama kuna mtu miongoni mwenu anategemea kuteuliwa katika baraza nitakalounda, ajiandae kuishi Dodoma maana nitaishi katika Ikulu aliyojenga na Mwalimu," alisema.

Aliwahakikishia wana CCM waliojitokeza kumdhamini kuwa, hawatajutia uamuzi huo; bali atatii kiu yao, kuwaletea uongozi bora na makini unaochukia rushwa na ufisadi kama alivyokuwa Mwalimu Nyerere.

Alitoa wito kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu, kuhakikisha wanamchagua yeye ambapo sera yake ya kuipeleka Tanzania katika uchumi wa viwanda unaobebwa na kilimo iko palepale.

Bw. Membe anaendelea kutafuta wadhamini mkoani Morogoro.

No comments: