Thursday, 18 June 2015

Moto wateketeza maduka 3 jijini Dar na kusababisha hasara ya zaidi ya milioni 150.


Maduka matatu yameteketea kwa moto katika eneo la Msasani kwa Mwinyi jijini Dar es Salaam na kusababisha mshutuko mkubwa na taharuki kwa wakazi wa maeneo hayo baada ya kusikika kwa milipuko ya gesi hali iliyowalazimu wasamaria wema kuamsha majirani na wenye nyumba kwa kurusha mawe makubwa juu ya mabati ili kuokoa maisha yao.
ITV ilifika katika eneo la tukio na kushuhudia baadhi ya watu wakishuhudia moto huo ukijaribu kuzimwa na kikosi cha zima moto, huku baadhi yao wakisema kwamba baadhi ya watu walipatwa na mshutuko kutokana na moto huo kusambaa kwa kasi na kulazimu magari manne ya zima moto kuwasili katika tukio hili kupambana na moto huo.
Mlinzi aliyekuwa katika eneo la maduka hayo, alilazimika kupiga yowe usiku ili kupata msaada baada ya kupigwa na butwaa na kasi ya moto huo huku baadhi ya majirani wakisema hali ya tukio la moto huo ilishtua wengi baada ya kusikika milipuko ya gesi katika moja ya duka iliyokuwa ikitetea kwa moto na kuongeza kuwa kuchelewa kwa kikosi cha zima moto ndio iliyosababisha maduka yote matatu kuteketea na kusababisha hasara ya zaidi ya milioni.
Afisa kutoka kikosi cha zima moto Bwana Saidi Sabauri akiwa katika eneo la tukio katika jitihada za kuzima moto huo ameeleza jitihada walizofanya huku mama mwenye nyumba akisema kuwa kutokana na kusumbuliwa na magonjwa alilazimika kutambaa ili kuokoa maisha yake.

No comments: