Kiungo wa Klabu ya Simba Jonas
Mkude anatarajiwa kwenda Afrika Kusini Alhamisi Juni 26 mwaka huu kwa
majaribio ya wiki mbili katika Klabu ya Bidvest Wits.
Akiongea na tovuti ya Simba,
Mkude alisema fursa hii ni adimu na anaamini akifanikiwa ataiwakilisha
vyema Simba na Tanzania kwa ujumla.
Akizungumzia pengo
litakaloachwa ikiwa atafanikiwa majaribio alisema “pengo langu linaweza
kuzibwa kwani Simba ina wachezaji nyota wanaojituma na wenye uwezo”
Alitumia mahojiano hayo kuwaasa
vijana mbalimbali wanaotaka kufanikiwa katika soka kujituma na kuwa na
nidhamu ili kupata mafanikio na kukuza vipaji vyao.
Raisi wa Simba Evans Aveva
alisema “Simba inamtakia kila la kheri Mkude kwenye majaribio yake
kwenye Klabu ya Bidvest Wits huko Afrika Kusini na hili liwe ni fundisho
kwa vijana wengine kuendeleza vipaji ili waweze kucheza mpira kwenye
ligi za Nchi nyingine kubwa hivyo kukuza upeo na vipaji zaidi katika
soka”.
Mkude ni zao la ukuzaji wa
vipaji vya Klabu ya Simba inaotilia mkazo kwani ni chipukizi aliekulia
katika mfumo wa Simba wa uendelezaji vipaji.
Mkude alizaliwa Desemba 3, 1992
Kinondoni B na kuanza soka lake akiwa mlinda mlango hadi kuwa kiungo wa
kutegemewa. Aidha alianza elimu ya msingi mwaka 1998 katika shule ya
Hananasif na kumaliza mwaka 2005.
No comments:
Post a Comment