Monday 22 June 2015

Prof. Mwandosya amtaka Lowasa amuunge mkono

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya amemuomba mgombea mwenzake katika kinyang’anyiro cha kutafuta ridhaa ya kuteuliwa kuwa mgombea kupitia CCM, Edward Lowassa asisite kumuunga mkono kama walivyofanya watangaza nia wengine ili mambo yaishe mapema.
Aidha, amewaonya wanaotishia kukihama chama endapo hawatapitishwa, akisema huo ni upuuzi na pia vitisho kwa Mwenyekiti wa Chama na wanaCCM kwa ujumla, hivyo wanaojiona wao ni maarufu kuliko chama wanajidanganya.

Mwandosya alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wilayani Mbozi alipokuwa akizungumza na wanaCCM waliomdhamini katika mbio zake za urais, pamoja na wanachama wengine waliojitokeza katika Ofisi za CCM Wilaya.
Mgombea huyo alisema amefarijika kusikia anaungwa mkono na wagombea wenzake, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe pamoja na kupata taarifa za Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira naye kusema anamuunga mkono.Alisema pamoja na kuungwa mkono na wenzake hao watatu, anamuomba pia Lowassa naye kumuunga mkono ili kuipunguzia kazi Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM).

“Nimesikia Membe amesema hapa Mbeya asipopitishwa yeye basi atamuunga mkono Profesa Mwandosya, nikasikia tena na Waziri Mkuu akisema hata kama asipopitishwa yeye atafarijika kama Profesa Mwandosya atakuwa mgombea, nikasikia tena na Wassira naye kupitia kwa mtu wake wa karibu ataniunga mkono, sasa namuomba mwenzangu naye Edward au maarufu kama Edo naye aseme Profesa ndiyo wangu, ili kazi iishe na tuipunguzie kazi Halmashauri Kuu,” alisema Profesa na kushangiliwa.

Awali Profesa Mwandosya aliwaeleza wanachama hao kuwa mwaka huu wa uchaguzi ni mwaka mgumu sana kwa CCM na kuwataka wanachama kutofanya mchezo katika kujibu mapigo ya wapinzani.
“Watatuuliza kuhusu EPA, wataendelea kutuuliza kuhusu Richmond, watatuuliza kuhusu Escrow, kubwa zaidi watatuuliza kuhusu Vodacom ingawa hili halizungumzwi lakini linakuja, lazima tujitayarishe.

“Sasa nani huyo ataweza kutusafisha, wananchi wakimtazama watasema huyu atatusaidia na atajibu, kila ninakopita naambiwa na wananchi kuhusu ufisadi na rushwa vinatuumiza."

"Kama chama lazima tukabiliane na hilo na hapa hatumzungumzii mtu lazima kama chama tuyaeleze kwa wananchi. Nani atafanya hivyo wakubwa wanajua,” alisema Profesa.

Akizungumzia wanaotishia kuhama chama, alisema wanajidanganya kwani CCM ni maarufu zaidi ya mtu mmoja mmoja, akisema mtu pekee aliyewahi kuhama na kukitikisa chama alikuwa Augustine Mrema, Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani.

No comments: