Thursday, 18 June 2015

Mafuta kupita bandari Tanga

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (EWURA), Felix NgamlagosiSERIKALI imesema inatarajia kuanza kutumia bandari ya Tanga katika kuingiza mafuta ili kupunguza msongamano na ucheleweshwaji wa upakuaji katika bandari ya Dar es Salaam pamoja na kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa nishati hiyo.
Kuanza kutumika kwa bandari ya Tanga kunatarajiwa kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mafuta, kupunguza ucheleweshwaji pamoja na kuongeza usalama wa usafirishaji wa nishati hiyo muhimu.
Akizungumza katika Mkutano wa wadau wa mafuta nchini uliofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Felix Ngamlagosi alisema tangu waanze mfumo mpya mwaka 2012 waliifunga bandari ya Tanga kupakua mafuta.


“Tulipoanzisha mfumo mpya wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja mwaka 2012 tulisitisha kuingiza mafuta katika bandari ya Tanga, na mfumo huo umekuwa na mafanikio makubwa sana,” alisema Ngamlagosi.
Alisema kwa kuwa mfumo huo umekuwa na mafanikio makubwa, wameamua kuifungua rasmi bandari ya Tanga ili ianze kutoa huduma ya kupakua mafuta na kuwa mbadala wa bandari ya Dar es Salaam.
Kutumika kwa bandari hiyo kunatarajiwa kuongeza kasi ya maendeleo katika mkoa wa Tanga, kuongeza upatikanaji wa ajira, kupunguza msongamano wa meli katika bandari ya Dar es Salaam na pia kuwa mbadala wa usafirishaji wa mizigo endapo kutatokea tatizo lolote katika bandari ya Dar es Salaam itatumika ya Tanga.

CHANZO; HABARILEO
Post a Comment