Wednesday, 3 June 2015

Askofu mkuu P. Bertoldi atumwa kuwa mjumbe wa amani B. Farso na Niger

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumanne, tarehe 2 Juni 2015 amemweka wakfu Askofu mkuu Piergiorgio Bertoldi, Balozi mpya wa Vatican nchini Burkina Faso na Niger, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika huko Venegono, Jimbo kuu la Milano, Kaskazini mwa Italia.
Seminari kuu ya Pio XI ilitabarukiwa na Kardinali Alfredo Ildefonso Schuster, aliyeongoza Jimbo kuu la Milano kwa muda wa miaka 25, akatangazwa kuwa Mwenyeheri na Papa Yohane Paulo II kunako Mwaka 1996. Hapa ni mahali ambapo Askofu mkuu Piergiorgio Bertoldi alipata majiundo na malezi yake ya kikasisi na hatimaye, akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Balozi wa Vatican nchini Burkina Faso na Niger. 
Kardinali Pietro Parolin katika mahubiri yake kwa namna ya pekee, amekazia wito na huduma kadiri ya tafakari inayotolewa na Nabii Yeremia aliyeweza kutekeleza utume wake kwa njia ya baraka na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kama binadamu alimwekea Mwenyezi Mungu vizingiti na vikwazo katika maisha yake, lakini akagundua na kuonja uhuru na upendo wa Mungu. Wito ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopokelewa kwa uhuru na utashi kamili. Mwenyezi Mungu daima anasubiri kwa utulivu na uvumilivu mkuu majibu muafaka kutoka kwa waja wake, kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko, kwani Mwenyezi Mungu ni muweza wa yote.
Hata leo hii, Mwenyezi Mungu anaendelea kujadiliana na waja wake anaotaka wajisadake katika wito na maisha ya kipadre na kitawa, kwa kuwapatia neema na karama kwa njia ya Roho Mtakatifu ili waweze kutekeleza dhamana na wajubu huu kwa umakini mkubwa. Askofu mkuu Bertoldi kwa kuwekwa wakfu, anapata ukamilifu wa Daraja Takatifu la Upadre ambalo lina ngazi kuu tatu yaani: Ushemasi, Upadre na Uaskofu.
Hii ni zawadi ambayo inapaswa kuboreshwa zaidi kwa njia ya sala, imani, ukarimu na upendo, tunu zinazoshuhudiwa kwa njia ya ujasiri na ukweli. Zawadi hii inapaswa kupokelewa kwa njia ya unyenyekevu ili kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, kwa ajili ya mafao na ustawi wa Familia ya Mungu. Kwa njia ya kuwekwa wakfu, sasa anakuwa ni chombo cha upendo wa Mungu.
Askofu mkuu Bertoldi ni kiongozi mwenye uzoefu katika utume na shughuli za kidiplomasia alizozifanya sehemu mbali mbali za dunia. Sasa anatumwa kama mjumbe wa amani, maridhiano na majadiliano yanayopania ustawi na maendeleo ya wengi, daima akitoa kipaumbele cha kwanza kwa uhuru wa kuabudu na haki msingi za binadamu. Anatumwa kama mjumbe anayekwenda kushiriki katika mchakato wa Kanisa nchini Burkina Faso katika kipindi hiki cha mpito, kwa kukazia majadiliano ya kidini na kitamaduni nchini Niger, ambako Wakristo bado ni wachache sana. Anatumwa kusaidia mchakato wa ujenzi wa madaraja ya ushirikiano kati ya Kanisa la Kiulimwengu na Makanisa mahalia.
Askofu mkuu Bertoldi awe kweli ni shuhuda wa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu; awe ni mjenzi na chombo cha amani kwa kujikita katika tunu msingi za Kiinjili, huku akionesha heshima kwa wote. Askofu mkuu Bertoldi aoneshe na kutoa ushirikiano na wale wote atakaokutana nao katika maisha na utume wake, akishuhudia kuwa ni mtumishi wa wote na mwaminifu kwa Kristo na Kanisa lake
Post a Comment