Wednesday 3 June 2015

Kambi ya wapinzani wa Burundi haijafurahisha kuhusu uamuzi wa viongozi wa EAC

Kambi ya upinzani nchini Burundi imeelezea kusikitishwa kwake na matokeo ya mkutano wa dharura wa viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Jumapili ya jana nchini Tanzania ambapo viongozi wa jumuiya hiyo walipendekeza kuakhirishwa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo. Jean Minani, mkuu wa chama cha upinzani cha Front for Democracy amesema viongozi wa EAC wameshindwa kutoa kauli inayowakilisha matakwa ya Warundi wengi ambao hawataki Rais Pierre Nkurunziza agombee muhula wa tatu kwenye uchaguzi ujao.
Marais wa Kenya, Uganda, Tanzania na wawakilishi wa Rwanda na Burundi jana Jumapili Mei 31 walikutana mjini Dar es Salaam, Tanzania na kujadili kwa kina hali ya kisiasa katika nchi ya Burundi ambayo ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwenye taarifa ya mwisho ya mkutano huo, viongozi hao wamesema ili kuweza kutuliza hali ya mambo nchini Burundi, uchaguzi unapaswa kuakhirishwa kwa siku 45. Pia viongozi wa EAC wametaka mikakati iwekwe ili kutoa fursa ya kurejea nyumbani makumi ya maelfu ya Warundi waliokimbia ghasia na machafuko. Mkutano wa Dar es Salaam pia umetaka makundi yote yenye silaha Burundi kuzisalimisha ili kuepusha hatari ya kuibuka vita vya kisiasa na kikabila nchini humo.
Itakumbukwa hapa kuwa, Burundi ilitumbukia kwenye ghasia na rangaito baada ya chama tawala CNDD-FDD kutangaza kuwa Rais Pierre Nkurunziza ndiye atakayepeperusha bendera ya chama hicho kwenye kinyang'anyiro cha urais kwenye uchaguzi mkuu ujao. Maandamano ya kupinga uamuzi huo wa chama tawala yamesababisha watu kadhaa kupoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wameshindwa kutoa mashinikizo ya kisiasa kwa Rais Pierre Nkurunziza ili asigombee muhula wa tatu kwa kuchelea kuwa, hatua kama hiyo inaweza kuchafua zaidi hali ya mambo ndani ya Burundi.
Ni wazi kuwa Burundi inapitia kipindi kigumu kwa hivi sasa. Vijana wa chama tawala cha CNDD-FDD wanaojulikana kama Imbonerakure wanatuhumiwa kuwaua takriban watu 50 tangu machafuko ya Burundi yalipoanza. Wajuzi wa Mambo wanasema mgogoro wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki usipovaliwa njuga mapema, taifa hilo linaweza kurudi tena kwenye vita vya ndani; jambo linaloweza kuvuruga utulivu na amani katika eneo zima.

No comments: