Monday 15 June 2015

Serukamba Kuzuiwa na Lowasa Kugombea Ubunge

Edward LowassaWAZIRI Mkuu mstaafu Edward Lowassa amesema huenda akamzuia Mbunge wa Jimbo la Kigoma, Peter Serukamba kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu ili amsaidie jukumu muhimu kwenye safari yake ya matumaini.
Akizungumza wakati wa kuomba udhamini kutoka kwa wanachama wa CCM mkoa Kigoma katika ofisi kuu ya CCM mkoa, Lowassa alisema Serukamba ni mmoja wa wanakamati katika safari hiyo ya matumaini.
Lowassa, anayewania kuteuliwa kugombea Urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM alisema katika safari hiyo kama mwanakamati Serukamba anayo majukumu muhimu ambayo anapaswa ayatekeleze zaidi ya kugombea ubunge.
“Ndugu zangu wananchi wa Kigoma nimekumbuka jambo moja ninaye mwana kamati ambaye ni mtoto wenu hapa Kigoma, Mbunge wenu Serukamba, yeye ni mmoja wa wajumbe katika kamati yangu alikuwa na dhamira ya kugombea tena ubunge, lakini mnaweza msimuone maana atakuwa na majukumu makubwa ya kunisaidia kwenye kamati,” alisema Lowassa.
Pamoja na kutogombea ubunge kiongozi huyo alisema Serukamba anayo dhamira ya dhati katika kuwatumikia wananchi wa mkoa Kigoma na ili kutimiza lengo hilo ameomba wasali na kumuombea sana ili aweze kupitishwa na chama chake kugombea Urais, lakini pia kushinda katika uchaguzi mkuu.
Serukamba ambaye kwa sasa anamaliza muhula wake kama Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini anatarajia kugombea tena ubunge katika jimbo la Kigoma Kaskazini.

No comments: