Friday, 5 June 2015

Mh.William Ngeleja nae atangaza nia ya kuwania urais kupitia CCM.

Mbunge wa jimbo la Sengerema Mh.William Ngeleja ametangaza nia ya kugombea nafasi ya urais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania kupitia chama cha mapinduzi–CCM na kuhaidi kushirikiana na jumuiya za kimataifa katika kuendeleza mapambano dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya na ugaidi pamoja na kupiga vita maadui wa taifa, ikiwemo rushwa, ufisadi, uvivu na mmomonyoko wa maadili.
Ni kauli ya aliyewahi kuwa waziri wa nishati na madini katika serikali ya awamu ya nne inayoongozwa na rais Jakaya Kikwete, Mh. William Ngeleja akiomba ridhaa ya kuteuliwa na chama cha mapinduzi kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwezi oktoba mwaka huu, kauli ambayo ameitoa kwenye ukumbi wa benki kuu ya Tanzania jijini Mwanza.
Ni kipi hasa kilichomsukuma Mh.Ngeleja hadi kuamua kujitosa katika mbio za kuwania kuteuliwa kuwa mgombea urais kupitia chama chake.
Mh. Ngeleja amesema kuwa ikiwa atapewa ridhaa ya kuongoza nchi katika awamu ya tano, kipaumbele namba moja kitakuwa ni ujenzi wa uchumi imara kwa kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa ni nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, sambamba na kuhakikisha kuwa mazao yote makuu ya biashara kama vile korosho na pamba, yanaimarishwa kwa kuongeza tija katika uzalishaji na kuyaongezea thamani badala ya kuyauza nje yakiwa ghafi.
Katika hotuba yake iliyorushwa moja kwa moja na kituo cha luninga cha Star tv na ITV, ikiwa na kaulimbiu, “maono sahihi, mikakati thabiti na matokeo halisi, Mh.Ngeleja amesema kuwa endapo atachaguliwa kuwa rais, atahakikisha serikali yake inaanzisha skimu za umwagiliaji na kuwekeza vya kutosha katika ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji kwa kila wilaya ili kuepukana na utegemezi wa mvua peke yake.
Mkutano huo wa kutangaza nia ya kuteuliwa kuwa mgombea urais kupitia chama cha mapinduzi umepambwa na vikundi vya ngoma na kwaya.

No comments: