Friday 5 June 2015

Wabunge waangua vilio wakiuaga mwili wa Marehemu Eugen Mwaisapo

Wabunge wa kiangua kilio wakati wanauaga mwili wa Eugen
MBUNGE  wa Jimbo la Ukonga, Eugen Mwaiposa, aliyefariki juzi mwili wake umeagwa mjini Dodoma katika viwanja vya Bunge na baadaye kusafirishwa kwa ndege kuletwa Dar es Salaam tayari kwa mazishi yatakayofanyika Jumamosi, nyumbani kwake Kitunda.

Watu mbalimbali wakiwemo wabunge, mawaziri wakiongozwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, walishiriki kuaga mwili huo huku vilio na majonzi vikitawala kutoka miongoni mwa waombolezaji pamoja na ndugu, jamaa na marafiki.

Akizungumza katika viwanja hivyo, Naibu Spika wa Bunge Job Ndugai, alisema kuwa kifo cha mbunge huyo kimeacha pigo kubwa kwa bunge wakati huu na mchango wake ulikuwa unahitajika zaidi.

Alisema kwa muda mrefu mbunge huyo aliyeingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2010 alikuwa na tatizo la shinikizo la damu. Ndugai alisema Mwaiposa alikuwa ni mbunge shupavu ambaye alijenga hoja za msingi na alikuwa na ujasiri wa kutetea hoja zake hadi mwisho bila kutetereka.

Akihubiri wakati wa kuaga mwili wa marehemu, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)  Jimbo la Dodoma, Samweli Mshana, aliwataka wabunge  kusali na kumtegemea Mungu, kwani hakuna anayejua siku yake ya kuondoka duniani.

Alisema katika kipindi hiki wabunge wanatakiwa kuwa karibu na Mungu na kuacha vitendo vibaya ambavyo havimpendezi Mungu.

"Mwalimu Nyerere aliwahi kusema heshima ya mtu itatokana  na huduma yake kwa jamii inayokuzunguka, hivyo  kwa kipindi hiki ni muda wa wananchi kulipa heshima kwa wabunge," alisema Mchungaji Mshana.

Hata hivyo alisema kama  Mbunge hujafanya vizuri katika jimbo lake ndipo  mtakimbilia kwa Sangoma ili muweze kuchaguliwa, hivyo achaneni na mambo hayo  mtumikieni Mungu simama na Mungu  ndiye jawabu la kila kitu.


Kwa upande wa wake mwakilishi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, alisema  Mwaiposa alikuwa ni mwanamke jasiri aliyethubutu na alikuwa mchapa kazi katika jimbo lake.

Alisema  aliweza kujenga hoja  zenye mashiko na kuzisimamia na kuhakikisha hoja zake zinajibiwa na  mara nyingi hakuzungumza  mambo ya ajabu, alijenga hoja za jimbo lake na maswali yenye mashiko kwa Taifa.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama, alisema  kuwa marehemu ameacha pengo kubwa  katika  bunge na wananchi wake ambao  alikuwa anawawakilisha bungeni.

Alisema serikali imepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Mbunge huyo, hivyo  ofisi ya  bunge imetoa  ubani wa shilingi milioni tano kwa  familia ya marehemu.  Mwaiposa alizaliwa Novemba  23, 1960 mkoani Kilimanjaro, alisoma shule ya msingi Nkweseto kati ya mwaka 1967 hadi 1974 na baadaye shule ya sekondari Masama mwaka 1976 hadi 1980.

 
Alijiunga na  Shule ya Biashara Shinyanga mwaka 1981 hadi 1983 na baadaye Chuo cha Eastern Southern Africana Management Institute (ESAMI) mwaka 2007 ambako alipata  cheti cha uongozi na kati ya mwaka  2006 hadi 2009 alisoma Hanns  Seidel ambako alitunukiwa cheti cha uongozi.
Kati ya  mwaka 1986 na 1992 alipata shahada  ya uzamili ya International Economic Relations katika chuo cha  Higher Economics Institute  Karl Marx Sofia Bulgaria na mwaka 2004 hadi 2007 alipata shahada ya  Uzamili katika  chuo cha  Strathclyde Glasgow nchini Scotland

No comments: