Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Dr Reginald Mengi ametoa nasaha hizo
jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya kuwatangaza na kuwazawadia
washindi wa mwezi Mei wa shindano alilolianzisha la kutwiti wazo bora la
biashara, ambapo zawadi ya kwanza ya shilingi milioni 10 imechukuliwa
kwa pamoja na washiriki wawili; Ombeni Sanga kutoka Iringa na Kelvin
Laswai wa mjini Moshi.
Akiwazawadia shilingi milioni moja kila mmoja washindi wengine
ambao twiti zao ziliingia kwenye 10 bora, Dr Mengi pia aliwahamasisha
vijana wajiamini kuwa kwa kutumia fursa zinazowazunguka wanaweza
kujikwamua kiuchumi kwa vile kila mtu amezaliwa kuwa mshindi.
Ombeni Sanga alitoa wazo la kutengeneza kifaa kinachofundisha kama
mwalimu kiitwacho boxpedia, na Kelvin Laswai alitoa wazo la kutengeneza
jiko sanifu-biolite stove linalotumia kuni chache na lenye sehemu ya
kuchaji simu na redio.
Mapema Jaji Mkuu wa shindano hilo Dr Donath Olomi na majaji wenzake
Bi Maida Waziri na Dr Jabu Mwasha walisema jumla ya twita 6,800
zilipokelewa na kushindanishwa, na kuwataka watu wengi zaidi washiriki
shindano hilo linalofikia kilele chake mwezi ujao.
No comments:
Post a Comment