MARA ya kwanza Simba ilipomsajili, Emmanuel Okwi, aliitikisa
sana ngome ya Yanga na kusababisha kila mechi ya watani wa jadi
ilipokaribia mabeki wa Jangwani walikosa raha.
Hata hivyo, baadaye wakaanza kumwona wa kawaida ingawa bado amekuwa akiwaumiza kila timu hizo zinapokutana.
Baadaye Simba ikamsajili Amissi Tambwe na mwenyewe
akawa moto kwa Yanga balaa, kila alipokutana nao walilala na viatu,
Yanga ikafanya mambo ikamsajili Jangwani na sasa anacheka na nyavu.
Sasa Simba kwa mara nyingine imejibu mapigo kwa
kumsainisha straika ambaye huenda ujio wake usipobuma kama Dan
Ssserunkuma, Yanga watalazimika kupaki basi.
Mtihani mkubwa kwa Yanga utakuwa kwa mabeki Juma
Abdul na Oscar Joshua wanaosimama pembeni huku katikati akisimama Kelvin
Yondani na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kama kawaida huku langoni akisimama
Ally Mustapha ‘Barthez’. Yanga inafikiria kununua kipa mwingine kutoka
nje baada ya kutoridhishwa na ufanisi wa Benedicto Tinocco.
Ingawa safu hiyo imeonyesha umahiri katika siku za
karibuni, lakini kwa aina ya uchezaji wa Laudit Mavugo ambaye ni
msumbufu na mwenye uchu wa kupachika mabao watalazimika kutumia akili za
ziada.
Hata Tambwe amekiri Mavugo wa Burundi ni noma ingawa amekiri kuwa yeye ndiye aliyemshauri asaini Simba.
“Simba ni timu nzuri sana ina wanachama na
mashabiki wazuri, ila tatizo lipo kwa viongozi ambao wengi wanaonekana
kuwa wababaishaji na kama wataendelea na ubabaishaji wao hawatafika
popote, naamini Mavugo atawasaidia sana kwani ni mchezaji mzuri na
anajitambua, atasumbua sana,” alisema Tambwe.
Mavugo ambaye ni mfungaji bora wa Ligi Kuu
Burundi, amesaini mkataba wa miaka miwili Simba, anatua nchini akiwa na
rekodi ya kufunga mabao 33 katika ligi ya kwao rekodi ambayo haijawahi
kutokea Ligi Kuu Bara kwa zaidi ya nusu karne.
Si Tambwe wala Okwi ambao wameweza kufanya hivyo jambo ambalo linapandisha hadhi ya Mavugo.
Tambwe aliongeza: “Ni mzuri uwanjani hasa katika
kazi yake ya kupachika mabao, ataisaidia Simba msimu ujao bora tu
wamtumie vizuri.”
Straika huyo anatarajiwa kurejesha zama za Tambwe
alipokuwa akiichezea Simba ambayo pia ilimsajili kutoka Vital ‘O ya
Burundi na kufanikiwa kuibuka mfungaji bora katika msimu wake wa kwanza
hapa nchini.
Mavugo anasajiliwa katika kikosi cha Simba ili kuiongezea nguvu
safu ya ushambuliaji inayoundwa na Okwi, Ibrahim Ajibu, Elius Maguli na
Mussa Hassan ‘Mgosi’ ambao wote ni mahiri wa mabao.
Mwanaspoti pia imebaini kuwa Mavugo amekuwa
akiifanya timu pinzani kucheza chini muda mwingi hivyo Yanga inaweza
kujikuta kiungo wake Said Juma Makapu akicheza zaidi kwa kukaba kuliko
kupanda kutokana na uwezo mkubwa wa straika huyo katika kumiliki mpira.
Hata hivyo, rekodi ya kufungwa mabao machache
msimu uliopita imeifanya Yanga kuwa na kiburi na safu yake ya ulinzi
kutamba kuwa Mavugo hatakuwa na madhara kwao.
Beki ya Yanga kwa sasa imeongezewa nguvu ya Mwinyi Haji kutoka KMKM ya Zanzibar ambaye anamudu kucheza beki ya kushoto.
Yondani anatarajiwa kuendelea kuwepo katika nafasi
ya beki wa kati licha ya mapendekezo ya kocha kuwa akatwe huku
Cannavaro akitarajiwa kuongoza safu hiyo kumzuia Mavugo asiwe na
madhara.
No comments:
Post a Comment