Monday, 8 June 2015

Ulimboka mwakingwe amleta mrithi wake Simba

MIONGONI mwa wachezaji wenye heshima na walioacha majina ndani ya Simba, Ulimboka Mwakingwe, Boniface Pawasa, Athuman Machupa,Emmanuel Gabriel na Juma Kaseja ni baadhi yao.
Wachezaji hao wamekuwa wakikereka na hali ya mambo inavyoendelea ndani ya Simba na wamekuwa wakikosoa sambamba na kutoa suluhisho. Ulimboka Mwakingwe ambaye kwa sasa anapiga biashara zake, amemshika mkono winga mmoja wa Morogoro na kumkabidhi kwa viongozi wa usajili wa Simba na kuwaambia: “Huyu dogo ni jembe mpeni mkataba.”
Mchezaji huyo ambaye ni winga, Emmanuel Mkumbuka, atamwaga wino muda wowote kwani Ulimboka amewahakikishia viongozi kwamba ana umri wa miaka 19 na amecheza naye Kihonda Magorofani FC ya mkoani Morogoro, hivyo wasiwe na wasiwasi naye.
Ulimboka ambaye ni mwanachama wa Simba, aliithibitishia Ukomboz blog kwamba alimpeleka mchezaji huyo ingawa amesisitiza mambo mengine ni siri lakini Mwanaspoti linajua kijana huyo aliwahi kuichezea Simba B.
Habari kutoka ndani ya Simba, zilisema Mwakingwe aliwahi kumleta mchezaji huyo katika usajili wa msimu uliopita lakini hakufuzu.
“Ni mchezaji ambaye ana uwezo ila bado mazungumzo yanaendelea na leo (jana) kulikuwa kuna kikao kwa ajili yake, kama wataafikiana basi watamsainisha,” kilisema chanzo cha habari ndani ya Simba.
Kama akisajiliwa, atakuwa wa saba mpya kusajili kikosini humo baada ya Mussa Hassan ‘Mgosi’ aliyeichezea timu hiyo miaka ya nyuma, Peter Mwalyanzi, Mohammed Fakhi, Samir Haji Nuhu, Abdullahman Mohammed na Laudit Mavugo raia wa Burundi.

No comments: