MIONGONI mwa makocha waliokuwa wakitajwa kutua Simba ni pamoja
na Kim Poulsen ambaye ni kocha wa zamani wa Taifa Stars, lakini sasa
haitawezekana tena baada ya klabu yake ya Silkeborg IF kumgomea kuondoka
na kumwongezea donge nono ambalo Simba hawawezi kumpa.
Baada ya kuona dili la kumleta Kim limeshindikana,
vigogo hao wanaumiza kichwa kumpata mbadala wa Goran Kopunovic ambaye
alitaka wampe Dola 50,000 sawa na Sh108 milioni jambo ambalo Simba
waliligomea.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa baada ya dili la Goran
lililokuwa linampa jeuri la kutua Azam lilipogonga mwamba, aliondoka
kwenda kwao Serbia na kutuma ujumbe wa kushusha dau hilo hadi dola
25,000 (Sh 54 milioni).
Imeelezwa kwamba matajiri wa Silkeborg IF
wamemwambia Kim endapo angekuwa anatafutwa na timu ya Taifa wangekuwa
tayari kumwachia lakini sio klabu ambayo pengine itashusha sifa yake
kisoka.
Mpaka sasa viongozi wa Simba wanaendelea na
mchakato wa kumpata kocha mwingine kwani hata kumrudisha Goran
kumewagawa vigogo hao ambao wengine wapo tayari na wengine hawataki
japokuwa inasemekana uwezekano wa kumrudisha ni mkubwa kutokana na
changamoto wanayoipata ya kumpata kocha mwingine.
Wakati hayo yakiendelea ndani ya klabu hiyo kongwe
nchini, imeelezwa kwamba uongozi utapangua kamati mbalimbali ambazo
zimeonekana kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Kiongozi mmoja wa juu wa Simba, aliliambia
Mwanaspoti kuwa kamati iliyolegwa hasa ni Kamati ya Mashindano ambapo
majukumu yao mengi yatapelekwa kwenye Kamati ya Ufundi iliyo chini ya
Mwenyekiti wake, Collin Frisch ambaye kwasasa pia hupewa majukumu ya
kusainisha mikataba kwa wachezaji wapya.
“Tumejifunza mengi msimu uliopita, ndio maana
tunataka kufanya mambo yetu kwa umakini mkubwa, kuna vitu vitabadilika
ambapo Kamati ya Mashindano haitakuwa na nguvu sana kwani kila kitu kwa
asilimia kubwa kitasimamiwa na Kamati ya Ufundi inayofanyakazi kwa
ukaribu mkubwa na benchi ya ufundi.
“Mchakato wa kocha bado unaendelea ingawa Goran
baadaye aliomba kushuka bei ila viongozi tunabishana juu ya kumrejesha,
hivyo suala lake pia halijapitishwa na huo mchakato mwingine bado
unafanyiwa kazi, ujio wa Kim ni mgumu kwani hakuna fedha ya kumpa,”
alisema kiongozi huyo.
No comments:
Post a Comment